.

.
Sunday, November 4, 2012

8:56 AM
WATU wawili wamekufa katika matukio mawili tofauti, mkoani Mara, akiwemo mwanafunzi mmoja wa shule ya msingi aliyebakwa na kisha kunyongwa kwa kutumia gauni lake na watu wasiofahamika na mwili wake kutupwa kwenye pagale.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, Absalom Mwakyoma, alisema kuwa matukio hayo yalitokea Agosti 30, mwaka huu katika maeneo tofauti mkoani humo.
Kamanda Mwakyoma alisema kuwa, katika tukio la kwanza, mwanafunzi mmoja aliyekuwa anasoma darasa la sita katika Shule ya Msingi Makoko, aligundulika akiwa amekufa na kisha mwili wake kutupwa kwenye pagale eneo la Darajani.
Alisema kuwa uchunguzi wa awali uliofanywa na polisi, pamoja na daktari ulionyesha kuwa mwanafunzi huyo alibakwa na kisha kunyongwa kwa gauni lake alilokuwa amevaa, na watu wasiojulikana.
Kamanda Mwakyoma alisema kuwa, kwa maelezo ya wazazi, binti huyo alitoweka nyumbani kwao siku mbili kabla ya mwili wake kuokotwa katika pagale.
Aidha, aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo, ili wale waliohusika katika kufanya ukatili huo waweze kubainika na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Katika tukio la pili, mwanaume mmoja, Kizwere Ndege (47), aliyekuwa anatembea kwa miguu, amefariki baada ya kugongwa na basi la Kampuni ya Bunda Express, eneo la Iramba, Wilaya ya Butiama
Alisema kuwa basi hilo lilikuwa likiendeshwa na dereva Ramadhan Karimu mkazi wa Mwanza, na kwamba chanzo cha ajali hiyo kinaelezwa kuwa ni mwendo kasi.

CHANZI CHA HABARI: GAZETI LA TANZANIA DAIMA

0 comments:

Post a Comment