Pages

Pages

Wednesday, October 31, 2012

MWENYEKITI WA BUNGE AKAMATWA NA TAKUKURU KWA TUHUMA ZA RUSHWA

Azzan Zaungu
MMOJA wa Wenyeviti wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu pamoja na makada wengine wa CCM, juzi usiku walikamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Dodoma kwa tuhuma za rushwa.

Habari zilizopatikana mjini hapa juzi usiku zinasema, Zungu alikamatwa saa 4.30 katika moja ya vituo vya mafuta akidaiwa kujaribu kutoa rushwa ya Sh100,000 kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa uchaguzi wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM.

Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Dodoma, Eunice Mmari, jana alikiri kuwakamata baadhi ya watu wakijihusisha na vitendo vya rushwa akiwamo Zungu.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mmari alidai kuwa vijana wake walimtia nguvuni Zungu juzi saa tatu usiku katika Hoteli ya Golden Crown akiwa na wapambe wake wakiendelea kugawa fedha kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Wazazi.
Alisema taarifa za Zungu kudaiwa kugawa fedha hizo walizipata juzi mchana na kuanza kufuatilia nyendo zake ambazo zilionyesha kuwa na dalili zote za rushwa.
“Tuliweka mitego yetu kila mahali ndipo tukabahatika kukutana naye katika eneo la hoteli hiyo akiwa na magari mawili, moja ikiwa ni teksi ya kawaida na nyingine ikiwa ni Prado ambayo ndiyo ilisadikiwa kubeba pesa,” alisema Mmari.
Kamanda huyo alidai kuwa kiasi cha fedha kilichokuwa kikitolewa na Zungu kilikuwa Sh100,000 kwa kila mjumbe ili kumshawishi ampigie kura.
Hata hivyo, alisema hawakuweza kumkamata moja kwa moja akitoa na hata fedha hizo hawakuzikamata kwani maofisa wa Takukuru walizingira gari dogo wakati fedha hizo zinasadikiwa zilikuwa katika Prado ambalo baada ya vurugu hizo lilitokomea kusikojulikana.
Akizungumzia madai hayo Zungu alisema: “Kwanza niseme kuwa si kweli kwamba nimekamatwa nikitoa rushwa, nilikuwa katika kituo kimoja cha mafuta wakaja watu ambao walisema wana shaka na gari langu.”
Aliendelea: “Samahani, halikuwa gari langu, bali ilikuwa ni teksi, mimi nikawaruhusu, wakaingia wakafanya ukaguzi na waliporidhika wakaniachia nikaondoka.”

Taarifa za awali

Zungu alikuwa mmoja wa wagombea wa nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec) kupitia Wazazi katika uchaguzi uliofanyika jana mjini Dodoma.
Habari zilizopatikana mapema jana zilisema baada ya kukamatwa, Zungu alipelekwa Ofisi ya Takukuru Mkoa wa Dodoma ambako alihojiwa hadi saa nane usiku alipoachiwa baada ya kuwekewa dhamana na Mbunge wa Bukene (CCM), Selemani Zedi.
Habari hizo zinaeleza kuwa baada ya kukamatwa, gari alilokuwamo lilifanyiwa upekuzi kabla ya kupelekwa Ofisi za Takukuru, pamoja na makada wengine wa CCM ambao walikamatwa kwa tuhuma hizohizo.
Kamanda Mmari pia alithibitisha kukamatwa kwa makada wengine watano ambao aliwataja kuwa ni Yahaya Danga, Busuro Pazi na Frank Mang’ati ambao alidai kwamba walikuwa wakimsaidia Zungu katika mpango wake huo.
Mbali na watu hao, Takukuru ilimtia mbaroni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Mbeya, Fatuma Kasenga ambaye anadaiwa kukamatwa akitoa rushwa ya chakula kwa wajumbe.
Alisema alikamatwa katika Hoteli ya Kitoli, Barabara ya Iringa saa tisa usiku.
Alisema kuwa watuhumiwa hao kwa pamoja waliachiwa kwa dhamana na kwamba uchunguzi unaendelea.
Katika hatua nyingine, Mmari alisema kuwa taarifa walizokuwa nazo ni kuwa mgombea wa nafasi ya Uenyekiti wa Jumuiya hiyo, Abdallah Bulembo alikuwa akitoa rushwa zaidi.
“Tatizo ni kwamba wanazungumza lakini hawatoi ushirikiano, maana kama wangetoa ushirikiano tungeweza kuwakamata kwa urahisi,” alisema Mmari.
 
Bunge hawajui

Akizungumzia kukamatwa kwa mbunge huyo, Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alisema Ofisi ya Bunge haikuwa na taarifa zozote kuhusu kukamatwa kwa mbunge huyo.
“Ndugu yangu, ndiyo nasikia kutoka kwako, sisi hatuna taarifa hiyo. Ni vigumu kuzungumzia jambo ambalo sijalisikia. Hata hivyo, nakushukuru sana kwa taarifa,” alisema Joel.
 
Rushwa CCM

Chaguzi za jumuiya za CCM zimekuwa zikilalamikiwa kugubikwa kwa vitendo vya rushwa na hata juzi baadhi ya wajumbe wa mkutano wa wazazi walilalamikia kuwapo kwa fedha nyingi kwenye uchaguzi huo.
Chaguzi nyingine zilizolalamikiwa kwa rushwa ni zile za Jumuiya ya Vijana (UVCCM) na Umoja wa Wanawake (UWT).
Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akizungumza na wajumbe wa jumuiya hizo mbili kwa nyakati tofauti, alisema vitendo vya rushwa vinavyokithiri katika chaguzi za chama hicho, vinatishia uhai wake na kuwataka wanaCCM kubadilika.
Akifungua mkutano wa Jumuiya ya Wazazi jana, Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal pia alizungumzia rushwa: “Hakuna sababu ya kumchagua kiongozi kwa kuwa tu amekupa kitu kidogo! Hakuna sababu ya mgombea kuamini kuwa ukitoa hongo na rushwa ndiyo utachaguliwa.
“Muda wa kampeni umekwisha na sasa mmebakiza saa chache mpigiwe kura. Sitegemei kuwa mtawapa tena nafasi wapambe wenu kujihusisha na vitendo vya rushwa ndani ya ukumbi wa mkutano.”
Mmoja wa wajumbe alimwambia mwandishi wetu juzi usiku kwamba rushwa iliyokuwa ikitolewa ni Sh100,000 kwa kila mjumbe, lakini fedha hizo zilikuwa zikitolewa kwa awamu, ya kwanza walipewa Sh70,000, wakati kiasi kilichobaki cha Sh30,000 walitarajiwa kupewa jana.
 
Nje ya ukumbi

Eneo linalozunguka Ukumbi wa Chuo cha Mipango ulikofanyika uchaguzi huo, jana lilihanikizwa na nyimbo za hamasa kuanzia saa 1.30 asubuhi zikitoka kwa wapambe wa wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi.
Wapambe hao walikuwa wakiimba na kuzunguka nje ya uzio uliozunguka ukumbi huo, huku wakiwa wamevalia fulana zenye picha za wagombea wanaowaunga mkono na kubeba  mabango yenye picha za wagombea hao.
Msafara wa mgombea wa uenyekiti, John Barongo ulioongozwa na pikipiki, magari madogo kwa makubwa na basi lililokuwa na wafuasi wake, uliwasili na kulakiwa na kundi la vijana waliokuwa wakimuunga mkono. Katika msafara huo, alikuwapo kada mkongwe wa CCM, Mzee Job Lusinde.
Baadaye, takriban dakika saba hivi, uliwasili msafara wa mgombea mwingine wa kiti hicho, Martha Mlata na wapambe wake na baadaye msafara wa Bulembo, hali iliyosababisha eneo hilo la nje ya uzio kushindwa kukalika kutokana na pilikapilka za kampeni za dakika za mwisho.
Shamrashamra hizo zilikoma baada ya kuwasili kwa Dk Bilal ambaye alifungua mkutano huo, kisha kukabidhi kazi ya kuuendesha kwa wasimamizi wa uchaguzi ambao ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Zakia Meghji.
Habari tulizozipata wakati tukienda mitamboni zinasema, Bulembo alikuwa akielekea kushinda nafasi ya uenyekiti akiwaacha mbali wenzake Mlata na Barongo.
Katika nafasi ya makamu mwenyekiti, uchaguzi huo ulitarajiwa kurudiwa baada ya wagombea wote kutofikisha nusu ya kura.

chanzo cha habari: gazeti la mwananchi

KASHFA YA TUHUMA ZA RUSHWA ZAIKUMBA YAIKUMBA SOKO JIPYA LA NMC


 Kashfa ya tuhuma za rushwa yaibuka katika soko jipya la NMC baada wafanyabiashara wadogowadogo (machinga) kulalamikia ugawaji wa kinyemela kwa baadhi ya maeneo kwa watu ambao siyo wamachinga wa katikati ya jiji kama ilivyokuwa lengo la kuhamishwa kwao.





Wakizungumza na waandishi wa habari sokoni hapo kwa hasira, baadhi ya wafanyabiashara hao waliokosa maeneo ya kuuzia na matokeo yake kuuza nje ya soko huku wakifukuzwa mara kwa mara na mgambo wa jiji, walisema kuwa ndani ya soko kuna baadhi ya maeneo yameshikwa na watu wasio wamachinga.





“Kama mnavyoona ndugu waandishi, ndani ya soko kuna baadhi ya maeneo yako wazi (hayatumiki) lakini sio kama hayana watu, kuna watu lakini siyo wamachinga bali wametoka mbali na kushika maeneo ndani ya soko huku wahusika tunauza nje baada ya kukosa maeneo huko ndani ya soko” alisema mmoja wao Scola Clement, na kuongeza


“Pia ugawaji wa meneo haya kulitawaliwa sana na rushwa kwani katika ugawaji wa maeneo ukiwa na mkono mfupi( usipotoa hela) hutapewa eneo bali utazungushwa hadi utaamua mwenyewe kutoa hela upate eneo baada ya kushuhudia mwenzako aliyetoa hela amepewa eneo haraka, mbali na hilo pia katika kugawa maeneo haya siyo yote yalikuwa wazi bali kuna baadhi yalikwisha gawiwa kabla hata ya tangazo rasmi kutoka”





Aliongeza kwa kusema kuwa “baada ya tangazo kutoka tulipoenda kushika maeneo baadhi ya maeneo tuliambiwa yamekwisha chukuliwa wakati ndio siku ya kwanza tena alfajiri, matokeo yake leo hii yale maeneo tuliyokuwa tunaambiwa yamekwisha chukuliwa leo wahusika ambao ni wafanyabiashara wakubwa mijini na wengine ni wa masoko mengine wanatuuzia yale maeneo kwa shilingi laki tatu(300,000) kama siyo walipewa maeneo haya kwa rushwa ni nini” alihoji.





Mfanya biashara mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Mussa Hamis alizidi kusisitiza kuwa rushwa ilitawala katika ugawaji wa maeneo hayo “mimi kama mimi naamini rushwa ilitawala sana kwani mbali na baadhi ya maeneo kupewa watu ambao siyo wahusika na leo kuja kutuuzia, pia kuna baadhi ya watu wamepewa maeneo makubwa ya mabanda mawili na zaidi, wengine madogo ya banda moja huku wengine wakipewa eneo lisilotosha hata kibanda 1”





Mussa alisema kuwa pamoja na halmashauri ya jiji kusikia kilio chao cha kupatiwa eneo la kufanyia biashara na kupewa eneo hilo lakini bado wako hatarini kupata magonjwa ya mlipuko hasa katika msimu huu wanaotarajia mvua, nah ii ni kutokana na soko hilo kutokuwa na huduma muhimu za kijamii na miundombinu huku wakiambulia kuahidiwa bila utekelezaji.





Aliongeza kuwa soko hilo jipya ni sawa na voda fasta kwani halikuwa na maandalizi yoyote kimiundombinu ikiwemo dampo kwa ajili ya taka zinazozalishwa sokoni hapo, choo, maji safi, pia hadi sasa hakuna ulinzi wa mali zao na wateja wao, ambapo pia alilalamikia swala la lango kuwa moja linalotagemewa kwa kutoka na kuingia sokoni hapo ambapo huhatarisha maisha ya wafanyabiashara hao pindi janga likitokea.





Akijibu tuhuma hizo afisa habari wa halmashauri ya jiji la Arusha, Ntagenjwa Hoseah alikanusha vikali ugawaji wa maeneo katika soko hilo kuhusishwa na maswala ya rushwa ambapo katika swala la miundombinu alisema kuwa halmashauri iko katika maboresho ya miundombinu ya soko hilo huku akisema kuwa kwa sasa wafanyabiashara hao wanatumia choo cha soko la krokon lililoko pembezoni mwa soko hilo jipya la NMC.







SERIKALI IUNGE MKONO MASOKO YA CHAKULA DUNIANI

Mkurugenzi wa shirika la chakula duniani (FAO) Jose Graziano da Silva wakati wa kikao kwenye makao makuu ya FAO Italy. 
 
Idara ya Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO linazitaka serikali kuunga mkono masoko ya kilimo  ili kukabiliana na ongezeko la bei ya chakula duniani.

Akizungumza  Jumanne mjini Roma katika maadhimisho ya  siku ya chakula duniani  mkurugenzi mkuu wa idara hiyo  Jose Graziano  da Silva amesema,   ni muhimu kuimarisha usimamizi wa chakula kwa sababu hakuna nchi pekee inayoweza kujitosheleza  katika dunia ya leo ya utandawazi.

Aliwaambia mawaziri kutoka nchi 20 waliohudhuria  kikao hicho kuwa ipo haja ya kuibuka  kwa mtizamo mpya wa dunia unaoratibiwa kimataifa kwa kupashana habari na kuwa na uwazi katika masoko, ili kukimu mahitaji ya dunia ya chakula.

Aidha shirika hilo limesema  mashirika ya kilimo ya kijamii ni muhimu kwa sababu yana malengo ya kuimarisha jamii zake kwa kutumia raslimali ilizonazo kwa maslahi ya kijamii. FAO linakisia kuwa watu milioni 870 hukabiliwa na  njaa duniani, idadi inayosema ni ya juu mno, ingawa imeshuka kutoka watu bilioni moja mapema miaka ya tisini.

LONDON KUFANYA MKUTANO WA MALENGO YA MILENIA

Njaa ni tatizo kubwa sana barani Afrika

Mkutano unafanyika leo mjini London kujadili mkakati mpya wa utakaotumika baada ya ule wa malengo ya milenia.
Malengo hayo yaliwekwa mwaka elfu mbili kuimarisha maisha ya watu katika nchi maskini na walitumai kuwa yangefikiwa mwishoni mwa mwaka 2015.
Aidha malengo hayo yananuia kukabiliana na maswala kama viwango vya umaskini, magonjwa , njaa na ukosefu wa elimu lakini mafanikio yamekuwa kidogo sana ikilinganishwa na matumaini ambayo watu walikuwa nayo.
Waziri mkuu wa Uingereza, David Cameron, anafanya mazungumzo na Rais Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia na Rais Susilo Bambang Yudhoyono wa Indonesia, wenyekiti watatu wa jopo la umoja wa mataifa litakalopewa jukumu la kuweka mkakati mwingine mwaka 2015 kwa sababu ya malengo ya milenia.

WATOTO WPOTEZA MAISHA BAADA YA KULIPUKIWA NA BOMU

Watoto watano ,watatu wakiwa wa familia moja wamekufa Wilayani Karagwe mkoani Kagera.

Ni baada ya kulipukiwa na bomu la kutupwa kwa mkono wakati walipokuwa wakichezea Bomu hilo lililookotwa kwenye vyuma chakavu na kudhani kuwa ni mpira.

Tukio hilo lilitokea Juma tano majira ya asubuhi huko Wilayani Karagwe mkoani Kagera Magharibi mwa Tanzania wakati watoto walipokuwa wakichezea kitu mfano wa mpira mdogo ,ambacho baadaye kilikuja kutambulika kuwa lilikuwa Bomu la kurushwa kwa mkono.
 Mkuu wa Wilaya wa Karagwe Bi Darli Rwegasira amesema kuwa watoto hao walilipukiwa na Bomu hilo ambapo watatu kati yao walikufa papo hapo huku wawili wakifia hospitalini.
Kwa Mujibu wa Mkuu huyo wa Wilaya, awali mzazi wa watoto hao amekiri kuwa aliliona bomu nyumbani kwake hapo juzi ambapo watoto wake walikuja nalo baada ya kuliokota huku wakidhani kuwa ni mpira.
Naye Kamanda wa Polisi mkoani Kagera Philipo Kalangi alisema kuwa utafiti waliofanya umeonyesha kuwa Bomu hilo lililookotwa na kijana mmoja ambaye alikuwa akikusanya vyuma chakavu kwa lengo la kuviuza hapo wilayani karagwe.
Bomu hilo lilikuwa mojawapo katika vyuma alivyokuwa ameokota na baadaye watoto hao walienda kulichezea nyumbani kwao na hatimaye kusababisha maafa hayo.
Mkuu huyo wa Polisi mkoani Kagera alidokeza kuwa uchunguzi unaendelea ili kujua kwa undani Bomu hilo lilitokea wapi na iwapo kama kuna mabomu mengine yanayoweza kuwa yamebaki katika maeneo mbali mbali hapo Wilayani Karagwe.
Mkuu huyo wa Polisi hakuweza kukiri wala kukana moja kwa moja kuhusisha Bomu hilo Kama matokeo ya uwepo wa wakimbizi wa Rwanda waliowahi kuishi Wilayani hapo mwaka 1994 baada ya mauaji ya kimbari nchini Rwanda ambapo Wilaya ya Karagwe ni moja ya wilaya zilizopokea wakimbizi wengi kutoka nchini Rwanda.
Uchunguzi zaidi unaendelea huku ukiwahusisha wataalam wa milipuko kutoka Polisi na jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.

TAHADHARI YA UGONJWA MPYA KWA WATANZANIA

                           Bendera ya Tanzania

                            TAHADHARI YA UGONJWA WA MARBURG

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, imepokea taarifa kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), tarehe 20 Oktoba, 2012 kuhusu ugonjwa wa Marburg ambao umejitokeza katika nchi jirani ya Uganda. Maeneo yaliyokumbwa na ugonjwa huo ni Wilaya ya Kabale, Kanda ya Kusini Magharibi ya nchi, na wilaya hii inapakana na Rwanda. Mpaka tarehe 24 Oktoba 2012, takriban watu 13 wamepata maambukizo na 6 wamepoteza maisha..

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa tahadhari ya Ugonjwa huu kwa wananchi wote, katika mikoa yote ya Tanzania na hasa wale waliopo katika mikoa ambayo inapakana na na nchi jirani ya Uganda (Mikoa ya Mara, Mwanza, Kagera na Kigoma).

Marburg ni ugonjwa wa hatari unaofanana na Ebola na unasababishwa na virusi vijulikanavyo kwa lugha ya kitaalam “Marburg Virus”. Ugonjwa huu ni miongoni mwa magonjwa yajulikanayo kwa ujumla kama Homa za Virusi zinazosababisha kutokwa damu mwilini, (Viral Haemorrhagic Fevers). 

Chanzo kamili cha virusi vya ugonjwa huu haki­julikani. Hali inayosababisha mlipuko wake pia haijulikani. Ugonjwa huu hauna tiba wala chanjo.

Dalili kuu za ugonjwa huu
 ni pamoja na Homa kali, inayoambatana na kutokwa damu katika matundu yote ya mwili yaani pua, njia ya haja kubwa na ndogo, mdomoni, masikioni, machoni, hali inayopelekea kifo kwa muda mfupi. Kipindi cha kuonekana kwa dalili za ugonjwa ni kati ya siku 3 hadi 9 baada ya kupata maambukizi.

Ugonjwa huu unaenea kwa urahisi sana na ha­raka kutoka mtu mmoja hadi mtu mwingine iwapo mtu atakuwa karibu na mgonjwa na kugusana na mate, damu, mkojo, machozi, kamasi, maji maji mengine ya mwili, ikiwa ni pamoja na jasho au kumgusa  mtu aliyekufa kwa ugonjwa wa Marburg.Ugonjwa huu pia unaweza kuenezwa iwapo mtu atagusa nguo au mashuka ya mgonjwa wa Marburg.

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, imechukua hatua zifuatazo katika kukabiliana na tishio la ugonjwa huu:
  • Kutoa taarifa ya tahadhari ya ugonjwa huu kupitia kwa Waganga Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya. Aidha taarifa hii pia imejumuisha namna mgonjwa anavyoweza kutambuliwa (Ainisho la Ugonjwa),  “Fact sheet” ya ugonjwa, Mwongozo kwa watumishi wa afya wa namna ya kuchukua sampuli na vipeperushi vinavyoelezea ugonjwa huu.
  • Kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huu kupitia kwa Wataalamu wa Afya katika Mikoa, Wilaya na maeneo ya mipaka. Aidha watalaamu hawa wa Afya pia wanatoa elimu kwa wananchi kuhusu dalili za ugonjwa huu ili endapo ugonjwa huo utatokea uweze kutolewa taarifa mapema.
  • Kupeleka vifaa kinga kwa ajili ya watumishi wa afya
Wananchi wanashauriwa kutokuwa na hofu kwani mpaka sasa hakuna mgonjwa yeyote aliyeripotiwa nchini. Wananchi wanashauriwa kutoa taarifa kwenye kituo cha huduma za afya kilicho karibu mara watakapoona mgonjwa yeyote atakayehisiwa kuwa na dalili za ugonjwa huu.
Taarifa  hii imetolewa na Kitengo cha mawasiliano ya Serikali

HALL KULAMBA DAU NENE AZAM

Wachezaji wa Azam wakimbeba juu kocha wao Stewart Hall baada ya kuwaongoza kutwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi kwa kuifunga Jamhuri ya Pemba katika fainali iliyofanyika Januari 12 Uwanja wa Amaan, Zanzibar. Picha na Jackson Odoyo.  

KOCHA Stewart Hall anatarajiwa kusaini mkataba mpya na timu ya Azam FC wakati wowote kuanzia sasa, hatua itakayomfanya kuingia kwenye orodha ya makocha wa klabu wanaolipwa vizuri barani Afrika.

Hall, raia wa Uingereza anatarajiwa kuwasili leo tayari kusaini mkataba mpya, akichukua nafasi ya Boris Bunjak aliyejiunga na Azam kuchukua nafasi ya Mwingereza huyo kabla naye kutimuliwa Jumatatu wiki hii.

Kutimuliwa Bunjak, raia wa Serbia kulikuja siku mbili tangu Azam kunyukwa 3-1 na Simba na kuporomoka kutoka nafasi ya pili ya msimamo Ligi Kuu mpaka ya nne.

Rais wa Sofapaka, Elly Kalekwa aliimbia Capital Sport kuwa, Azam wamemwomba radhi Hall na kumwahidi mkataba mnono ambao wameshindwa kumzuia.

"Sikupenda kuondoka kwake, lakini siwezi kumzuia. Azam wamempa mkataba unaofanya kuwa miongoni mwa makocha wanaolipwa zaidi Afrika."
"Kwanza walimwambia [Hall] wangependa kuendelea kuwa naye na kumwomba radhi kwa kufukuzwa kulikotokana na mapendekezo ya wachache," alisema rais huyo wa Sofapaka.

"Hall ni mweledi, tangu alipoingia mkataba na sisi. Azam walipomfuata alinipa taarifa na baada ya majadiliano tumekubali aende," Kalekwa alisema kwa huzuni.

Naye Bunjak alisema amepokea uamuzi huo kwa shingo upande na mshangao mkubwa hasa ukizingatia kuwa sababu ni matokeo ya kufungwa na Simba.

Bunjak alisema ameiongoza Azam kwa mafanikio kabla ya kucheza na Simba, akishinda mechi tano, sare tatu na kubaki nafasi ya pili kipindi kirefu.
Hata hivyo, Bunjak amesema anakubali hatua iliyochukuliwa dhidi yake, lakini akihoji vigezo vilivyotumika mpaka akafukuzwa.

ìHakuna timu isiyofungwa, kufungwa ni sehemu ya mchezo na ndiyo mpira wenyewe," alisema Bunjak.
"Haiingii akilini kama kigezo ni kufungwa na Simba. Inawezekana ni uamuzi tu uliokuwapo hasa kwa vile wanasema, "kocha anaajiriwa ili afukuzweî,î alisema Bunjak.

Alisema ni vigumu kumfukuza kocha kwa kufungwa mechi moja. "Ina maana timu hii (Azam FC) haitakiwa kufungwa hata mchezo?"

Bunjak alisema inashangaza kocha anatimuliwa kutoka timu iliyo nafasi ya pili kwenye msimamo, tena ikiwa na mechi moja pungufu ya nyingine.

ìNimekubali, wamenilipa fedha zangu, sina jinsi kwa sasa nasubiri kurejea nyumbani Serbia siku mbili zijazo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Bodi ya Azam, Hall atawasilileo kutoka Kenya na anatarajia kuanza kazi kesho katika mechi dhidi ya Coastal Union Uwanja wa Chamazi.

WANAFUNZI KADHAA WAJERUHIWA KWA KUPIGWA MABOMU NA POLISI HUKU WENGINE 3 WAKIKAMATWA KWA KUANDAMANA HADI KWA MKUU WA MKOA

mwanafunzi wa shule ya Kinyaki aliyekamtwa kwa amri ya mkuu wa mkoa,  baada ya kuandanama kushinikza mwalimu mkuu kuondolewa shuleni kwao
MKUU wa Mkoa wa Arusha Magesa Mulongo amewasweka rumande wanafunzi watatu wa Shule ya Sekondari Kimnyaki kwa kutoridhishwa na maelezo ya sababu za  maandamano yao na wanafunzi wenzake hadi Ofisini kwake.
Wanafunzi hao waliokamatwa wakati wakijieleza kusudio la maandamano yao ni pamoja na Ezekiel Memiri, Losijaki Lunde, na Meshack Lomnyaki ambapo walisema kuwa wamekuwa wakinyanyaswa na walimu wao shuleni ikiwemo kuwafanyisha kazi za nyumbani kama ma-house girl.

Maandamano ya wanafunzi hao yalikuwa na lengo la kushinikiza Mkuu wao wa shule ya kinyaki mwalimu Mariam Chamle kuondolewa kwa kuwa chanzo cha matatizo shuleni hapo ikiwemo kushusha kiwango cha taaaluma shuleni hapo.

Mmoja wa wanafunzi hao, Meshak Lonyaki ambaye ni kaka mkuu wa shule hiyo alisema kuwa walimu wao wamekuwa chanzo cha wao kufeli kwa kutokuwafundisha darasani badala yake wanadai hela ya kuwafundisha masomo ya ziada(tution) na kuwatoza shilingi 10,000.

Mbali na hilo pia wanafunzi hao walisema  kuwa katika mtihani wao wa mock ya form two baadhi ya wanafuzi walirudishwa majumbani kwa kudaiwa michango midogomidogo na kutofanya mitihani huku baadhi yao wakirudishwa ingawa walilipa lakini muhasibu hakuwaandikia hivyo kutakiwa kuwasilisha risiti huku wanafunzi wenzao wakiendelea na mitihani na wengine waliopoteza risiti hawakufanya mitihani. 

mkuu wa mkoa wa Arusha, Magessa S. Mulongo(kushoto) akiwa n La Kamanda wa operesheni maalum wa jeshi la polisi, peter Mvula(katikati) pamoja na kamanda wapolisi mkoa wa Arusha Liberatus Sabas (kulia) wakiwasikiliza wanafunzi wakijieleza. (hawapo pichani)
Katika maelezo yao, Mkuu wa Mkoa alisema kwamba ni makosa makubwa kwa wanafunzi kukaidi ama kushindwa kufuata maagizo ya shule hasa yaliyoandikwa katika fomu zao za kujiunga na shule kwa kufuata masharti ya kulipa ada ambapo aliamuru wakamatwe.

“Askari kamata hawa jamaa weka ndani hawana heshima hata kidogo,haiwezekani wakaufanya mkoa wa  Arusha kama kiwanja cha michezo kwamba kila anayehitaji kucheza anaruhusiwa kufika, haya mambo hayawezekani hata kidogo, hivyo hawa watakiona cha mtema kuni na wakome kufika hapa… lazima utaratibu ufuatwe ili kila mmoja apewe haki ya kusikilizwa”alisema Mkuu wa Mkoa na kuongeza:

“Tena nataka kuchukuwa nafasi hii kupiga marufuku maandamano yote ya wanafunzi katika Jijini la Arusha, siwezi kukubaliana na suala hili hata kidogo, kuna viongozi wa serikali wapo shuleni,nyinyi mko huku,Mkuu wa Wilaya ya Arumeru yuko huko tayari kwa ajili ya kuwasiliza mmekimbilia kwa Mkuu wa Mkoa tena bila vibali vya maandamano”

Aliishia hapo mkuu huyo bila kutatua kero za wanafunzi hao zaidi ya kuwakamata waliojieleza, na kuwataka wanafunzi hao warudi shule haraka na wakichelewa atachukua maamuziya kufunga shule hiyo.

 Awali kabla ya wanafunzi hao kufika Ofisi ya mkuu wa mkoa walikutana na vikwazo vya Askari wa Jeshi la Polisi kwa kupigwa mabomu ya machozi mfululizo na kusababisha baadhi yao kujeruhiwa ambapo hata hivyo awali kamanda wa operesheni maalum wa jeshi la polisi, Peter Mvula alikana wanafunzi hao kupigwa mabomu hadi mmoja wao alipotoa moja ya bomu ambalo halikulipuka walilorushiwa ndipo walipokubali.
mmoja wa wanafunzi akionyesha moja ya bomu waliloliokota lililorushwa na polisi lakini halikulipuka, ikiwa kama ushahidi kuwa walipigwa mabomu ya machozi
Maandamano hayo  yaliyoanza juzi yana lengo la kumshinikiza Mwalimu Mkuu wa shule hiyo ya Kinyak aondolewe kwa kile walichodai kwamba anachangia kudidimiza maendeleo yao kitaaluma na kwamba anafurahia matokeo mabaya ya wanafunzi hao.
Baada ya Jeshi la Polisi kufanikiwa kuzuia maandamano hayo siku ya kwanza ya octoba 30 siku inayofuata wanafunzi hao walibuni njia nyingine ya kuandamana na kufanikiwa kufika katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Arusha pamoja na kupigwa mabomu ya machozi na kusababisha wengine waliojeruhiwa kurudia njiani.
“Jana Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Nyerembe Munassa alifikia shuleni kwetu akatuambia kwamba angekuja kesho (yaani leo) kutusikiliza, tukamsubiri hadi saa nne bila mafanikio ndipo tulipobuni njia nyingine ya kuandamana, tukaamua kuondoka shule mmoja mmoja mpaka katikati ya mji, ndipo tulipokutana na askari hao ambapo walianza kuturushia mabomu ya machozi sisi tukawa tunanawa huku tukiendelea kuja ”alisema Ezekiel Memiri





Tuesday, October 30, 2012

WATANZANIA JENGENI UTAMADUNI WA KUTEMBELEA MAKUMBUSHO YA TAIFA KUJUA NA KUONA HAYA................

wafahamu, waone na wajue ndege na wanyama wa hifadhi zetu kwa kuona Taswira zao
wajue na Waone binadamu wa kale



AUAWA KWENYE GHASIA KENYA


Ghasia zilizuka baada ya kifo cha Kwega mjini Kisumu

Mwanasiasa wa Kenya Shem Kwega ameuawa huku mke wake akijeruhiwa mjini Kisumu Magharibi mwa Kenya.
Bwana Kwega alikuwa mshirika wa karibu wa waziri mkuu, Raila Odinga, anayegombea urais.
Polisi waliwarushia gesi ya kutoa machozi waandamanaji waliokuwa wanaelezea kero lao kuhusu mauaji hayo wakidai kuwa yalikuwa mauaji ya kupangwa.
Hali ya taharuki inatanda nchini Kenya kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika mwezi Machi.
Zaidi ya watu 1,000 waliuawa kwenye ghasia za baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2007 zilizofuatia uchaguzi uliozua utata mkubwa kuwahi kushuhudiwa nchini Kenya tangu uhuru.
Wiki jana kiongozi wa mashtaka katika mahakama ya kimataifa ya ICC, Fatou Bansouda alielezea wasiwasi kuhusu tatizo la vurugu nchini humo.
Mahakama ya ICC itawafungulia mashtaka washukiwa wanne wa ghasia hizo za baada ya uchaguzi akiwemo naibu waziri mkuu Uhuru Kenyatta ambaye pia anawania urais kwa kuhusika na ghasia hizo.
Bwana Kwaga na mkewe walipigwa risasi na washukiwa waliokuwa wanaendesha pikipiki.
Aidha marehemu Kwega alikuwa mfanyabiashara maarufu ambaye alikuwa anagombea kiti cha ubunge kwa chama cha waziri mkuu.
Ingawa polisi wangali wanashuku kuwa huenda kilikuwa kitendo cha wizi, lakini wafuasi wake wanaamini kuwa yalikuwa mauaji ya kupangwa.

ZANZIBAR WALALAMIKIA UNYANYASAJI WA POLISI


BAADHI ya wananchi wa Zanzibar, wamelalamikia kile walichokielezea kuwa ni ukiukwaji wa haki za binadamu, unaofanywa na polisi katika operesheni ya  kuwasaka wahalifu na watu wanaotuhumiwa kuchochea vurugu visiwani humu.
Operesheni hiyo inafuatia matukio ya  uvunjifu wa amani ulioambatana na uharibifu wa mali hasa baada madai ya kutoweka ghafla kwa Kiongozi wa Taasisi za Kiislamu, Sheikh Farid Hadi Ahmed,  Oktoba 16 mwaka huu.
Jana zaidi ya watu 50 walikutana na waandishi wa habari na kulalamikia  vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu katika operesheni ya kuwasaka watuhumiwa.
Kwa mujibu wa watu,  kijana mmoja aliyetambuliwa kuwa ni Hamad Ali Kaimu, amekufa  baada ya  kupigwa na askari wa vikosi vya usalama katika operesheni hiyo.
Miongoni mwa waliozungumza na waandishi ni, baba mzazi wa kijana huyo, Ali Kaimu mkazi wa eneo la Nyerere, ambaye alidai kuwa mtoto wake alipigwa hadi kufa akiwa mikononi mwa polisi na kwamba tukio hilo lilitokea Oktoba 27, mwaka huu.
Kaimu alisema kitendo hicho hakikubaliki na kwamba hatua lazima zichukuliwe dhidi ya wahusika.
Baba huyo wa marehemu, alisema alimuona mtoto wake akiitwa na polisi wakati akienda kuchunga ng’ombe na kwamba baadaye askari walianza kumpiga kijana huyo akiwa mbele ya macho yake.
“Mwanangu aliniita baba njoo uchukue mzigo wangu na nikuonyeshe nilipomfunga ng’ombe wangu na nilipokwenda polisi na mie wakaniangushia kipigo kikali sana. Mwanangu alikuwa na Sh50,000 za kununulia godoro na alitaka kunipa lakini walikataa asinikabidhi” alisema baba huyo kwa huzuni.
Alisema kijana wake alikamatwa na siku ya Sikukuu ya Idd El Hajj na  wakati akichunga ng’ombe huko Magomeni.
Kaimu alisema siku ya pili alipigiwa simu akiitwa katika katika Kituo cha Polisi cha Madema na alipokwenda alitakiwa kwenda katika Hospitali ya Mnazi Mmoja kuchukua  mwili wa mtoto wake.
“Walinipigia simu nikachukue maiti yangu na mimi nikagoma  kwa sababu wamemchukua mwanangu akiwa hai na nikawaambia munikabidhi mwanagu akiwa hai vipi watanipa mwanangu maiti,” alihoji mzee huyo.

WATU TISA WASHIKILIWA KWA TUHUMA ZA UJANGILI



Watuhumiwa wa ujangili wakiwa chini ya ulinzi na nyara walizokamatwa nazo eneo la Hifadhi ya Bonde la Yaeda Wilayani Mbulu mkoani Manyara juzi, ambapo nyara hizo zina thamani ya Sh3.2 milioni.

WATU tisa  wanaodaiwa kuwa majangili wamekamatwa na polisi, mkoani Manyara kwa tuhuma za kukutwa na silaha aina ya short gun na  nyara za Serikali.
Wanadaiwa walikutwa na nyumbu watano na kanga watatu  wote wakiwa na thamani ya Sh3.2 milioni waliokuwa wamebebwa kwenye magari mawili.
Inadaiwa kuwa watu hao walikamatwa juzi kwenye pori la Hifadhi ya Bonde la Yaeda Chini, wilayani Mbulu  na mmoja wao alikuwa na sare  tatu  za  mavazi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).  
Mkuu wa Upelelezi na Makosa ya Jinai mkoani Manyara, Benedict Msuya alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kudai kuwa watu hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani pindi uchunguzi wa tukio hilo utakapokamilika.

Msuya alisema watu hao walikamatwa baada ya raia wema kutoa taarifa kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Mbulu (OCD), George Kyando ambaye alituma polisi waliowakamata watu hao wanaodaiwa kuwa ni majangili.
Alisema watuhumiwa ni pamoja na mkazi wa Geita mkoani Mwanza aliyekutwa na sare za JWTZ.
Mmoja niu mkazi wa  Shinyanga wakati wengine watatu ni wakazi wa Kijiji cha Dominiki mkoani Singida.
Msuya alisema kuwa watuhumiwa wengine wa tukio hilo ni  wakazi wa Mkoa wa Singida.
Alisema watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na bunduki aina ya short gun na risasi zake tano yenye namba  Mark 1V, mapanga sita, visu vinne na tochi kubwa tatu, sufuria tano na madebe mawili ya unga wa mahindi.
Alisema pia waliyakamata magari mawili aina ya Land Rover. 
Naye,Ofisa Wanyamapori wa wilaya hiyo, Allan Shanny alisema magari hayo yalikuwa yamebeba wanyama pori waliouawa wakiwamo nyumbu watano na ndege watatu aina ya kanga wenye thamani ya Sh3.2 milioni.
Shanny alisema hali ya ujangili Bonde la Yaeda chini ni kubwa hususani kwa wanyama kama tembo wanaouawa kwa ajili ya kitoweo na pia uharibifu wa mazingira unafanywa na wawindaji haramu.

ZIARA YA MEMBE MKOANI MBEYA


Mhe. Bernard K. Membe (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akisaini kitabu cha wageni jana katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, wakati akiwa katika ziara ya siku mbili Mkoani humo.
Mhe. Waziri Membe akifafanua kuhusu mgogoro wa Mpaka wa Ziwa Nyasa kati ya Tanzania na Malawi mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama chini ya Uenyekiti wa Mhe. Abbas Kandoro, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoani Mbeya wakimsikiliza kwa makini Mhe. Waziri Membe (hayupo pichani).
Wilayani Kyela, Mbeya

Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Mhe. M. Malenga akimkaribisha Mhe. Waziri Membe (wa pili kulia), wakati alipotembelea Ofisi yake jana Wilayani Kyela.  Mhe. Membe yupo Mkoani Mbeya kwenye ziara ya kikazi ya siku mbili, ambapo anatarajiwa kutembelea maeneo ya ufukwe wa Ziwa Nyasa. 


Wajumbe mbalimbali waliohudhuria Mkutano wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Kyela (hayupo pichani).



Balozi Irene Kasyanju (wa pili kushoto), Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Balozi Dkt. Mohamed Maundi (kushoto), Mkurugenzi wa Chuo cha Diplomasia - Kurasini wakisikiliza maelezo ya Mhe. Malenga kuhusu Wilaya ya Kyela.
Safari ya kuelekea kwenye mpaka wa Mto Songwe

Mkuu wa Wilaya ya Kyela akiuongoza msafara wa Waziri Membe kuelekea kwenye mpaka wa Mto Songwe uliopo kati ya Tanzania na Malawi.
Mhe. Waziri Membe na msafara wake wakiwa wamesimama kwenye mpaka wa Mto Songwe.
Waziri Membe akiangalia Mto Songwe, huku akitafakari mpaka kwa vile hapo aliposimama kwa ufupi ni nchini Malawi ambapo wananchi wa pande zote wanapishana kuendelea na shughuli zao za kawaida (angalia alama ya tundu lililoko chini ya fensi - kulia).
Mhe. Waziri Membe akiongea na Wajumbe wa msafara wake akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Abbas Kandoro (mwenye shati jeupe mbele ya Waziri), Balozi Irene Kasyanju (wa pili kushoto), Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria kwenye Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Balozi Dkt. Mohamed Maundi (kushoto), Mkurugenzi wa Chuo cha Diplomasia - Kurasini.  (Picha hii na Mbaraka Islam)
Makazi ya wananchi wa Malawi kando ya Mto Songwe ambapo mmoja wa wananchi anaonekana akifua nguo (pichani - upande wa kushoto; ng'ando ya mpaka kwa upande wa Malawi) wakati wengine (kulia) wanaonekana wakiendelea na shughuli zao za kawaida huku wakiwa tayari wamevuka ng'ando ya mpaka kwa upande wa Tanzania.  
 
Picha, maelezo na Woinde shizza