Dar es Salaam.
Mwigizaji maarufu wa filamu
nchini, Elizabeth Michael Kimemeta, amekiri mahakamani kuwa na uhusiano
wa kimapenzi na aliyekuwa mwigizaji mwenzake, Steven Kanumba na pia kuwa
ugomvi na Kanumba siku ya tukio la kifo cha mwigizaji huyo, lakini
akakana mashtaka ya kumuua bila kukusudia.
Lulu ambaye yuko nje kwa dhamana anakabiliwa na
kesi hiyo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, akidaiwa kumuua
Kanumba bila kukusudia, kinyume cha Kifungu cha 195 cha Kanuni za Adhabu
(PC), April 7, 2012, nyumbani kwa marehemu Kanumba, Sinza Vatican.
Jana Lulu alipandishwa kizimbani mahakamani hapo
na kujibu mashtaka hayo kwa mara ya kwanza tangu alipofunguliwa kesi
hiyo, ambapo alikana kumuua Kanumba bila kukusudia.Kesi hiyo namba 125
ya mwaka 2012 inasikilizwa na Jaji Rose Teemba.
Kukubali kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Kanumba,
ni miongoni mwa mambo manane ambayo mshtakiwa huyo aliyakiri mahakamani
hapo jana, kama mambo yasiyobishaniwa katika kesi hiyo.
Mambo mengine ambayo Lulu aliyakiri mahakamani
hapo yaliyoko katika maelezo ya kesi hiyo ni pamoja na jina na anuani
yake, kwenda nyumbani kwa Kanumba usiku wa tukio hilo, kuwa na ugomvi na
Kanumba pia Kanumba kumzuia kutoka nje ya chumba alipojaribu kutoka ili
akimbie.
Mengine ni kufanikiwa kutoka nje ya chumba cha
Marehemu Kanumba, kumweleza mdogo wa Kanumba (Seth Bosco) kuwa Kanumba
ameanguka, kukamatwa kwake na polisi eneo la Bamaga, saa 11 Alfajiri ya
usiku wa tukio hilo na kwamba kweli anashtakiwa kwa kosa la kumuua
Kanumba bila kukusudia.
Kama jana Lulu angekiri mashtaka hayo baada ya
kusomewa, basi mahakama ingemtia hatiani na kumhukumu adhabu ambayo
ingeona inafaa kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, baada ya kukana mashtaka hayo, sasa
kesi hiyo itaingia katika hatua nyingine ya usikilizwaji kamili (trial),
ambapo upande wa mashtaka utalazmika kuwaita mashahidi wake mahakamani
ili kuthibitisha kuwa Lulu alimuua Kanumba bila kukusudia.
Pia Lulu atalazimika kujitetea yeye binafsi na pia
kuwaita mahakamani mashahidi wa kumtetea na kisha mahakama itaandaa na
kutoa hukumu yake.
Wakili wa Serikali, Mbogo aliiarifu mahakama kuwa
wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, upande wa mashtaka utakuwa na
mashahidi wanne ambao ni pamoja na Seth Bosco, Daktari binafsi aliyekuwa
akimhudumia Kanumba, Dk Paplas Kageiya, Ester Zephania na Askari D/Sgt
Ernatus wa Kituo cha Polisi Oysterbay.
Pia Wakili Mbogo aliwasilisha mahakamani vielelezo
viwili vitakayotumika kama sehemu ya ushahidi katika kesi hiyo ambayo
ni taarifa ya kitabibu ya uchunguzi wa chanzo cha kifo cha Kanumba na
ramani ya eneo la tukio.
Lulu kwa upande wake, mawakili wake Peter Kibatala
na Fulgence Massawe waliiarifu Mahakama kuwa wakati wa usikilizwaji wa
kesi hiyo kwenye utetezi watakuwa na mashahidi watano na vielelezo
viwili. Hata hivyo hawakutaja majina ya mashahidi hao.
0 comments:
Post a Comment