.

.
Sunday, February 16, 2014

11:06 AM


Photo: African elephant TEMBO AKIONYESHA ISHARA YA HATARI KWAKE.

Meno ya Tembo yanayosakwa na wafanyabiashara wakubwa huku soko lake likitajwa kuwa nchini China.

SINGIDA/MTWARA.

IKIWA ni muda mfupi baada ya Rais Jakaya Kikwete kukiri kuwa vita dhidi ya ujangili ni tatizo sugu linaloielemea Tanzania, Jeshi la Polisi mkoani Mtwara na Singida linawashikilia watu wanne kwa tuhuma za kukutwa wakisafirisha nyara za Serikali.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Maisha Maganga alisema kuwa jeshi hilo limewakamata watu watatu wakiwa na meno ya tembo 58 yenye uzito wa kilogramu 130.6 yenye thamani ya Sh700.3 milioni.


Kamanda alieleza kuwa watuhumiwa hao walikamatwa saa 11:00 alfajiri katika Kijiji cha Chungu Kata ya Nanyumbu, Wilaya ya Nanyumbu Mkoa wa Mtwara wakiwa katika kizuizi cha barabara ya Mtambaswala – Mangaka wakielekea jijini Dar es Salaama.


“Tunawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kupatikana na nyara za Serikali ambazo ni meno ya tembo 58 yenye uzito wa kilogramu 130.6 na thamani ya 700.3 milioni, ambapo ni sawa na tembo 29 waliouawa yakiwa ndani ya gari aina ya Toyota Land Cruiser,” alisema Kamanda Manganga.


Alisema mbinu waliyotumia watuhumiwa hao ni kukata sakafu ya gari ya chini ya kiti cha nyuma ya dereva na kutengeneza tanki la bandia na kuweka meno hayo kisha kuweka kapeti juu yake.


Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Hamidu Ngunde (40) dereva, Geraldat Lukas (36) dereva na Boniphace Kosan (29) wote wakazi wa jijini Dar es Salaam na kusema kuwa gari iliyotumika kusafirisha meno hayo ni mali ya Hilali Rashid.


Wakati huo huo, Kamanda wa polisi Mkoa wa Singida, Geofrey Kamwela, alisema wamefanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja, Februari 13 mwaka huu saa 2.30 asubuhi katika kizuizi cha Mazaoa ya Misitu na Chakula kilichopo katika Kijiji cha Ukimbu Kata ya Mgandu, tarafa ya Itigi, Wilaya ya Manyoni.


Alisema mtuhumiwa huyo alikuwa akitumia gari aina ya Toyota lenye namba T.797 CQL kusafirisha nyara za Serikali kutoka Kijiji cha Mwamangembe kwenda Itigi Mjini.


“Nyara alizokamatwa nazo mtuhumiwa zilikuwa zimewekwa kwenye mabegi mbalimbali ya nguo,” alifafanua. Kamwela alisema uchunguzi wa awali, umeonyesha kuwa vipande hivyo 21 vinakadiriwa kuwa vya tembo wanne, vina uzito wa kilogramu 49 na thamani ya Sh43.1 milioni. MWANANCHI.

0 comments:

Post a Comment