NCHIMBI: TUMEKUBALI KUWAJIBIKA KWA MAKOSA YALIYOFANYWA NA POLISI
ALIYEKUWA Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi amesema yeye pamoja na mawaziri wenzake watatu walikubali kuwajibika kutokana na makosa yaliyofanywa na askari waliokuwa wakitekeleza Operesheni Tokomeza Ujangili.
Dk Nchimbi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini (CCM), alisema kuna uhalifu wa hali ya juu katika mbuga za wanyama, ambao baada ya miaka 10 unaweza kumaliza wanyama kwenye mbuga hizo.
Akizungumza na wakazi wa Manispaa ya Songea kwenye Viwanja vya Kiblang’oma, Kata ya Lizaboni Songea katika kilele cha maadhimisho ya miaka 37 ya CCM, alisema Serikali ilifanya uamuzi wa kuwasaka majangili na kuwatokomeza.
Alisema katika operesheni hiyo, wananchi wapatao 11 na askari sita waliuawa jambo lililosababisha matatizo makubwa...
“Baada ya kuonekana raia wamefariki kukatokea ushawishi wa kutaka baadhi ya watu wabebe dhamana ya askari ambao walionekana hawajatekeleza majukumu yao inavyotakiwa.”
Alisema yeye na wenzake waliwajibika baada ya kutafakari kazi inayofanywa na askari katika nchi hii kwani wanalala usiku na kung’atwa na mbu kwa ajili ya wananchi, pia wanapambana na majambazi na hata kupoteza maisha wakati mwingine wakati wakilinda raia.
Hata hivyo, alimshukuru Rais Kikwete kwa kumpa heshima kubwa ya kumsaidia katika kipindi cha miaka minane na kuwatoa hofu watu wa Songea kwa kuwahakikishia kuwa kasi ya maendeleo katika jimbo lake haitapungua.
Uteuzi wa Dk Nchimbi na mawaziri wengine Khamisi Kagasheki (Maliasili na Utalii), Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na Dk David Mathayo (Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi) ulitenguliwa mwishoni mwa mwaka jana baada ya malalamiko ya wabunge kutokana na matatizo yaliyojitokeza kwenye Operesheni Tokomeza.
0 comments:
Post a Comment