.

.
Sunday, February 16, 2014


Rais Jakaya Kikwete.
 
BAADHI ya wafanyabiashara wa mikoa ya Kaskazini pamoja na kumpongeza  Rais Jakaya  Kikwete, lakini wamemtaka awataje mapapa 40 wa ujangili aliobainisha Jijini London, kwani ndiye Amiri Jeshi Mkuu na hakuna kitu kilicho na mamlaka juu yake.

Walisema alipokabidhiwa uongozi aliapa kuilinda na kuitetea katiba ya Tanzania pamoja na kuhakikisha ustawi wa raia  na rasilimali za taifa.http://4.bp.blogspot.com/-ES7OJbdHpOU/Uoya4tg3ZuI/AAAAAAAAAYg/oURQr7dITBY/s1600/1_kenya_elephant_mountain_bull_FB_620x465.jpg
Walitoa maoni hayo walipozungumza na NIPASHE kuhusu  kauli yake Jijini London wakati wa  mkutano ya wanyamapori na kwenye mahojiano maalumu na televisheni ya CNN ya  Marekani  na Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC.
 
Mwenyekiti mstaafu wa Chama cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima (TTCCIA) mkoa wa Kilimanjaro, Patrice Boysafi, akizungumzia maelezo ya Rais alisema :
 
“Yeye ni mlinzi mkuu wa katiba, watu na rasilimali za nchi hii yakiwamo meno ya tembo, alitakiwa aamuru  mapapa wa ujangili wakamatwe na kufikishwa mahakamani”.
 
Alisema Rais yuko juu ya mamlaka yote ndiye  Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, hivyo hana na sababu ya kumuogopa mtu anatakiwa ataje watuhumiwa hao wanaofahamika kuwa ni waharibifu wa mali za umma.
 
“Ni kiongozi mkuu ana mamlaka nikisikia  amesema anawajua mapapa wa ujangili tulitegemea  atoe amri  ya kuwakamata na kuwashitaki maana ndiye Amiri Jeshi Mkuu, hana cha kuficha wala kuhofia,” alisema Boysafi.
Alihoji  kama wanafahamika kwa nini hadi sasa mtandao haujavunjwa? Ni nini kinakwamisha kama wanafahamika?
 
 Boysafi alisisitiza kuwa  kuwa wanajulikana, idadi yao pamoja na viongozi wao, hivyo Rais alitakiwa kutoa maagizo kwenye vyombo vya dola ili washughulikiwe  siyo katika televisheni wala redio za kigeni au kwenye majukwaa ya jumuiya ya kimataifa. 
 
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TTCIA Arusha Adolf Ulomi, alisema  wanatarajia  kuona hatua zikichukuliwa baada ya Rais kueleza kuwa wafanyabiashara hiyo wanafahamika.
 
Alisema kwa kuwa watuhumiwa wanajulikana na kiongozi wao yuko Arusha, wanategemea kuona polisi na vyombo vya dola vikichukua hatua ya kuwakamata , kushtakiwa, kuvunja mtandao na kukomesha ujangili.
 
Kwa mujibu wa Ulomi, kama jambo linafahamika ni wazi wana usalama wako porini wanawatafuta majangili hao na wanachotaka ni  wakamatwe na washtakiwe.
 
Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCIA Mkoa wa Kilimanjaro, Boniface Maliki, akizungumzia kadhia hiyo ya ujangili alisema,  Rais alitoa taarifa hizo baada ya gazeti la Daily Mail la London kuripoti ujangili, lakini hakuwahi kuzizungumza humu nchini.
 
Alisema inaelezwa kuwa vigogo wa biashara hiyo wako Arusha lakini habari zinafahamika baada Daily Mail kuishambulia Tanzania…  kwanini taarifa  hazikuwahi  kutolewa kabla? Na kuuliza mbona  maelezo hayakupatikana akiwa nchini?
 
Alisema wafanyabiashara wanataka kuona ushahidi wa mambo yaliyozungumzwa London ukibainisha watuhumiwa na hatua zikichukuliwa dhidi ya majangili waliochafua sifa ya taifa.
 
Kuhusu kuomba msaada jumuiya ya kimataifa, walisema si jambo baya lakini kwa vile walilenga kupata  vifaa vya kisasa na vyenye  teknolojia  ni jambo jema.
 
Kwa upande wa utendaji, alisema hakuna haja ya kuomba msaada nje kwa kuwa wapo watendaji wanaoweza kukamilisha operesheni za ulinzi wa wanyamapori kinachotakiwa ni utashi wa kisiasa.
 
Wafanyabiashara  wengine  walimpongeza Rais Jakaya Kikwete,  kwa kugundua mtandao wa  majangili 40, wakiongozwa na kinara aliyeko mkoani Arusha na kushauri akamatwe bila kujali.
 
Diwani wa Kata ya Mererani, Justiny Nyari , ambaye pia ni mfanyabiashara wa madini, alimpongeza Rais kwa jitihada za kufuatilia na kugundua mtandao  huo.
 
Alisema  Rais anastahili pongezi kwa sababu bila kufuatilia huwezi kugundua mtandao huo na kueleza kuwa maelezo hayo ni kweli kwa vile ni Rais Kikwete ana mamlaka makubwa ya  nchi.
 
Mfanyabiashara  mwingine Aisha Juma, anayemiliki  duka la nguo na viatu jijini Arusha, alisema kauli ya Rais  ni nzito hivyo kinachotakiwa ni mtuhumiwa awe amejulikana , kukamatwa na kuchukuliwa hatua.
 
Alimpongeza Rais kwa kugundua mtandao huo na kutaka mtuhumiwa namba moja akamatwe na ajulikane  ili umma umtambue na sio kuzungumza  na kuacha suala hilo kuishia hewani. CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

0 comments:

Post a Comment