.

.
Monday, February 17, 2014

Dar es Salaam.
 Mwigizaji maarufu wa filamu nchini, Elizabeth Michael Kimemeta, amekiri mahakamani kuwa na uhusiano wa kimapenzi na aliyekuwa mwigizaji mwenzake, Steven Kanumba na pia kuwa ugomvi na Kanumba siku ya tukio la kifo cha mwigizaji huyo, lakini akakana mashtaka ya kumuua bila kukusudia.
Lulu ambaye yuko nje kwa dhamana anakabiliwa na kesi hiyo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, akidaiwa kumuua Kanumba bila kukusudia, kinyume cha Kifungu cha 195 cha Kanuni za Adhabu (PC), April 7, 2012, nyumbani kwa marehemu Kanumba, Sinza Vatican.
Jana Lulu alipandishwa kizimbani mahakamani hapo na kujibu mashtaka hayo kwa mara ya kwanza tangu alipofunguliwa kesi hiyo, ambapo alikana kumuua Kanumba bila kukusudia.Kesi hiyo namba 125 ya mwaka 2012 inasikilizwa na Jaji Rose Teemba.
Kukubali kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Kanumba, ni miongoni mwa mambo manane ambayo mshtakiwa huyo aliyakiri mahakamani hapo jana, kama mambo yasiyobishaniwa katika kesi hiyo.
Mambo mengine ambayo Lulu aliyakiri mahakamani hapo yaliyoko katika maelezo ya kesi hiyo ni pamoja na jina na anuani yake, kwenda nyumbani kwa Kanumba usiku wa tukio hilo, kuwa na ugomvi na Kanumba pia Kanumba kumzuia kutoka nje ya chumba alipojaribu kutoka ili akimbie.
Mengine ni kufanikiwa kutoka nje ya chumba cha Marehemu Kanumba, kumweleza mdogo wa Kanumba (Seth Bosco) kuwa Kanumba ameanguka, kukamatwa kwake na polisi eneo la Bamaga, saa 11 Alfajiri ya usiku wa tukio hilo na kwamba kweli anashtakiwa kwa kosa la kumuua Kanumba bila kukusudia.
Kama jana Lulu angekiri mashtaka hayo baada ya kusomewa, basi mahakama ingemtia hatiani na kumhukumu adhabu ambayo ingeona inafaa kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, baada ya kukana mashtaka hayo, sasa kesi hiyo itaingia katika hatua nyingine ya usikilizwaji kamili (trial), ambapo upande wa mashtaka utalazmika kuwaita mashahidi wake mahakamani ili kuthibitisha kuwa Lulu alimuua Kanumba bila kukusudia.
Pia Lulu atalazimika kujitetea yeye binafsi na pia kuwaita mahakamani mashahidi wa kumtetea na kisha mahakama itaandaa na kutoa hukumu yake.
Wakili wa Serikali, Mbogo aliiarifu mahakama kuwa wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, upande wa mashtaka utakuwa na mashahidi wanne ambao ni pamoja na Seth Bosco, Daktari binafsi aliyekuwa akimhudumia Kanumba, Dk Paplas Kageiya, Ester Zephania na Askari D/Sgt Ernatus wa Kituo cha Polisi Oysterbay.
Pia Wakili Mbogo aliwasilisha mahakamani vielelezo viwili vitakayotumika kama sehemu ya ushahidi katika kesi hiyo ambayo ni taarifa ya kitabibu ya uchunguzi wa chanzo cha kifo cha Kanumba na ramani ya eneo la tukio.
Lulu kwa upande wake, mawakili wake Peter Kibatala na Fulgence Massawe waliiarifu Mahakama kuwa wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo kwenye utetezi watakuwa na mashahidi watano na vielelezo viwili. Hata hivyo hawakutaja majina ya mashahidi hao.

0 comments:

Post a Comment