.

.
Thursday, January 30, 2014

Hali ya usalama Tarime imezidi kutoweka baada ya jambazi lisilofahamika likiwa na bunduki ambayo haijafahamika aina yake kuendelea kuua watu kwa risasi hasa wa jinsi ya kiume, ambapo idadi ya waliouawa imefikia saba hadi sasa na inadaiwa huwaua watu na kupotea bila kutambuliwa.
Jambazi hilo lisilofahamika liliua watu hao usiku wa Januari 27, mwaka huu katika maeneo ya Nkende likianza na kumuua Mwendesha Bodaboda, Juma Marwa Mkazi wa Nkende mjini Tarime akiwa anaelekea nyumbani kwake ambaye alikufa akiwa hospitali akipatiwa matibabu.

Mganga wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime, Marco Nega alisema tangu Januari 27 hadi sasa hospitali imeendelea kupokea watu waliouawa na majeruhi ambao wamefanyiwa uchunguzi na kugundulika wakiwa wamejeruhiwa kwa risasi katika sehemu mbalimbali za mwili na kwamba watu wapatao 7 wamekwisha kufa mpaka sasa.
“Tumepokea maiti za watu na majeruhi na tumewafanyia uchunguzi wakagundulika wana majeraha ya risasi sehemu mbalimbali za mwili, ambapo tayari watu saba wamekufa wengine wamekufa wakiwa njiani wakienda kwenye matibabu Musoma, marehemu hadi ni saba,” alisema Nega.
Waliojeruhiwa wakosa huduma ya X-ray
Watu waliojeruhiwa wameshindwa kupatiwa huduma ya X-Ray kutokana na Hospitali ya Wilaya kutokuwa na huduma hiyo kwa muda wa zaidi ya miezi 3 na kusababisha wagonjwa kusafirishwa kwenda Musoma na Mwanza kwa matibabu, ambapo Samweli Richard amekufa akiwa njiani kuelekea Musoma kwenye matibabu ikiwamo huduma hiyo ya X-ray.
Hospitali ya Wilaya yashindwa kutoa huduma
Huduma kwa wagonjwa mbalimbali katika Hospitali ya Wilaya imeshindwa kuendela vilivyo baada ya kupatwa na misiba miwili ya watumishi wawili, ni baada ya waume zao kuuawa na jambazi hilo lisilofahamika.
Awali Januari 26 jambazi hilo lilimuuwa Robert Kisiri (45) mkazi wa Mugabiri ambapo Mstaafu wa JWTZ Zacharia Mwita(58) na Erick Makanya (25)wote wakazi wa Kijiji cha Mogabiri Kata ya Kitare Wilayani Tarime walikutwa wakiwa wameuawa na miili yao ikiwa na majeraha ya risasi mbavuni kushoto na mgongoni.
Pia jambazi hilo liliwajeruhi watu watano kwa risasi ambao ni Mgosi Marwa Mkazi wa Mogabiri, Joseph Richard Mkazi wa Rebu, Gastor Richard Mkazi wa Rebu, Juma Mwita Mkazi wa Mogabiri na Mkandarasi Binafsi wa ujenzi, Mwasi Yomami ambao kati ya hao wawili wamefariki wakati wakipatiwa matibabu.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya, Justus Kamugisha amesema wamemkamata mtu mmoja anayeshukiwa kuwa mhusika wa mauaji ambaye yuko chini ya ulinzi kwa mahojiano na kwamba anazidi kuongeza vikosi vya doria kuimarisha ulinzi na usalama na kuwasaka wahalifu.
Wananchi wacharuka
Wananchi Mjini Tarime waliitaka polisi kuhakikisha jambazi hilo linapatikana vinginevyo walitaka polisi kuwakabidhi bunduki ili waweze kumsaka jambazi huyo.
‘Kamanda kashindwa kazi haiwezekani mtu mmoja aue watu 7 ndani ya siku mbili, huu ni uzembe wa polisi katika kuimarisha ulinzi, tunaomba tukabidhiwe bunduki tulisake jambazi,” alisema mwananchi mmoja

0 comments:

Post a Comment