.

.
Thursday, January 2, 2014

10:10 AM



Waziri Mkuu mstaafu na mbunge wa Jimbo la Monduli,Mh. Edward Lowassa akizungumza katika tafrija aliyoiandaa kwa wananchi wake na wageni mbalimbali ya kuukaribisha mwaka mpya 2014,iliyofanyika nyumbani kwake Ngarashi Monduli.Pembeni yake ni mkewe mama Regina Lowassa.

Waziri Mkuu mstaafu na mbunge wa Jimbo la Monduli,Mh. Edward Lowassa akiwasalimia wageni waalikwa waliofika kwenye tafrija hiyo aliyoiandaa kwa wananchi wake na wageni mbalimbali ya kuukaribisha mwaka mpya 2014,iliyofanyika nyumbani kwake Ngarashi Monduli.

Waziri Mkuu mstaafu na mbunge wa Jimbo la Monduli,Mh. Edward Lowassa (katikati) akizungumza na Naibu Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Mh. Goodluck Ole-Medeye wakati wa tafrija hiyo iliyofanyika nyumbani kwake Ngarashi Monduli. 


Chanzo- Mwananchi

Monduli. Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ametangaza kuanza rasmi kwa safari aliyoiita ya matumaini ya ndoto zake, ambayo amesema itatimiza ndoto za Watanzania za kupata elimu bure, maji safi na maendeleo ya uhakika.
Akizungumza katika ibada ya shukrani na kuupokea mwaka mpya, katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT),Usharika ya Monduli Mjini, Lowassa bila ya kutaja safari hiyo ni ipi, aliwashukuru watu wote kutoka maeneo mbalimbali nchini, ambao walimsindikiza katika ibada hiyo.
Lowassa alisema anaamini watu hao waliofika, wana uhakika wa ushindi katika safari hiyo kwa kumtegemea Mungu.
“Nimefarijika sana leo kuwaona hapa marafiki zangu wengi. Ninapowatazama hadi machozi yananitoka na kwa uwezo wa Mungu tutashinda kwani nyote mnajua nia na ndoto yangu,’’ alisema Lowassa na kupokelewa na sauti za shangwe kanisani.
Licha ya kutoweka bayana, Lowassa amekuwa akitajwa kuwa ni mmoja wa wanasiasa wanaowania kumrithi Rais Jakaya Kikwete baada ya kumaliza kipindi chake cha uongozi mwakani.
Azungumzia Katiba Mpya.
Akizungumzia Katiba Mpya, ambayo mchakato wake sasa unaelekea katika Bunge Maalumu, licha ya kuipongeza Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba alisema ana wasiwasi juu ya muundo wa Serikali Tatu.
“Nina wasiwasi na huu muundo, ni vyema viongozi wa dini, kuliombea taifa tupate Katiba bora kwani maoni ya watu asilimia 40 ambao hawakutaka muundo wa Serikali Tatu lazima yatazamwe,” alisema Lowassa.
Ibada katika Kanisa hilo, ambayo iliendana na harambee ya kuchangia hosteli na zaidi ya Sh89 milioni kupatikana, iliongozwa na Kaimu Askofu wa KKKT, Usharika wa Kaskazini Kati, Solomon Masango.
Katika mahubiri yake, Kaimu Askofu Masango alimtakia kila la heri Lowassa katika safari yake hiyo akisema anamtambua kuwa ni kiongozi bora.
Hafla ya nyumbani
Akizungumza katika hafla aliyoandaa baadaye nyumbani kwake, Lowassa alirudia kauli yake ya kuanza safari.
Waliohudhuria halfa hiyo ni pamoja na wabunge wengi wakiwa wa CCM, wenyeviti wa CCM, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Wenyeviti wa CCM, Mgana Msindai kutoka Mkoa wa Singida, Mwenyekiti wa Wenyeviti wa UVCCM, Manka Dilu kutoka Mkoa wa Mara na Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Wanawake wa CCM, Diana Chilolo pia kutoka Mkoa wa Singida, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Manyara, Lucas ole Mukusi ambaye ndiye katibu wa wenyeviti wote wa CCM.
Wengine waliohudhuria ni wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec), mikoa mbalimbali ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM na viongozi wa dini mbalimbali. Pia alikuwapo aliyekuwa mgombea urais wa Kenya katika uchaguzi uliopita, Profesa James ole Kiapi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Lowassa alisema ndoto ya elimu bure, ajira kwa vijana, kuondoa umaskini zitafanikiwa baada ya kuanza safari yake hiyo hapo jana.
Alisema wakati ukifika wa kutangaza rasmi nia hiyo, ataeleza mengi na akawataka wanaomuunga mkono wasiwe na shaka... “WanaCCM msiwe na shaka, tutavuka kwa nguvu zetu... wingi wenu huu unanipa faraja kuwa katika safari yetu na kwa kumtegemea Mungu tutashinda.”
Lowassa aliwataka waungane na kaulimbiu yake, ‘Tulifurahi pamoja, tulihuzunika pamoja na tutashinda pamoja’ na baada ya kusema maneno hayo, alipokewa kwa sauti za CCM... CCM... CCM.
Waalikwa wazungumza
Akizungumza katika hafla hiyo, Msindai ambaye aliwaongoza wenzake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja na Onesmo Nangole wa Mkoa wa Arusha alisema wanamuunga mkono, Lowassa katika safari yake hiyo.
Alisema anamfahamu Lowassa kwa muda mrefu na kumwelezea kwamba ni kiongozi bora mwenye uamuzi na kwamba haoni sababu ya kutokumuunga mkono.
Mgeja alisema anawashangaa watu wachache ambao wameanza tabia ya kulazimisha watu kuwachagulia marafiki na kuwachafua wengine.
Alisema hakuna ambaye hafahamu kuwa Lowassa ndiye tumaini la Watanzania akisema jina lake linatajwa kila kona kwa kuwa ana uwezo na sababu za kuwa kiongozi wa Taifa.
Mgeja alionya kuwa kuna kundi la watu linalodhani kuwa CCM ni mali ya viongozi kitu ambacho alisema si sahihi, bali ni mali ya wanachama ambao alisema ndiyo wenye uamuzi.
Nangole alisema Lowassa ni kiongozi msikivu na makini ambaye ni tegemeo la Watanzania katika kuwaunganisha kuwa kitu kimoja.
Wakizungumza katika hafla hiyo, viongozi hao wa CCM, walisema wanamuunga mkono Lowassa kutokana na uwezo mkubwa alionao.
Manko kwa upande wake alisema UVCCM ina imani kubwa na Lowassa kwani ni mmoja wa makada wa CCM wenye historia ndefu katika chama hicho.
Kwa upande wake, Mbunge wa Chemba Kondoa (CCM), Juma Nkamia alisema Lowassa sasa ni sawa na Simba na kusema wanaomchukia walie tu kwani ni kiongozi bora.
Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM, Hussein Bashe aliwataka wananchi wa Monduli kutunza heshima ya Lowassa na kwamba kazi nyingine watafanya wao.
Alisema safari ya Lowassa ndiyo, imeanza inawezekana na kwamba alipoanguka mwaka 2008, ilikuwa ni mipango ya Mungu kuwezesha safari hiyo. “Lowassa ana sifa zote za uongozi... tunachokiomba kwenu ni ushirikiano tu.”

0 comments:

Post a Comment