.

.
Wednesday, June 18, 2014

Mpango kabambe waja Mwanza, ArushaSERIKALI imeipa kazi ya kuandaa mpango kabambe (Master Plan) wa mipango miji kampuni ya kimataifa ya Surbana International Pty Ltd ya nchini Singapore kwa ajili ya majiji ya Arusha na Mwanza.
Kampuni hiyo inatakiwa kukamilisha shughuli hiyo ndani ya miezi 13 tangu kusainiwa kwa mkataba huo.
Mkataba huo ulisainiwa wiki iliyopita jijini hapa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Alphayo Kidata na Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Kong Wu Mun.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo na Waziri wa Nchi wa Mambo ya Nje na Mambo ya Ndani wa Singapore, Masagos Zulkiflg walikuwepo kushuhudia tukio hilo la utiaji saini.
Akizungumza mara baada ya kusaini mkataba huo, Kidata alisema tukio hilo ni mwendelezo wa mchakato uliokuwa umeanza kufuatia mkataba wa makubaliano ambao Wizara ya Ardhi ilisainiana na Singapore Desemba 2013 kwa niaba ya Tanzania.
Alisema lengo la kuanzisha mradi huo ni kuwezesha miji iliyopangiliwa vizuri na yenye maendeleo na kuondokana na msongamano wa magari pamoja na nyumba zisizokuwa na mpangilio jijini Arusha.
“Kuwepo kwa mpango huu kutawezesha kwa kiasi kikubwa sana kuishi katika mpangilio unaohitajika na kuchangia nchi kupata maendeleo kwa kuwa na miundombinu ya kutosha katika maeneo yenye mpangilio,” alisema Kidata.
Alisema kuwa wanatarajia kusaini mkataba na kampuni ya China kwa ajili ya kuandaa mpango kabambe kwa ajili ya mikoa ya Lindi na Mtwara ambayo inatazamiwa kukua kwa kasi kubwa kutokana na kugunduliwa kwa nishati ya gesi.
Zulkiflg alisema kuwa nchi yake imejikita katika kusaidia mataifa yanayoendelea, hasa kwa kuwasaidia kuandaa uwepo wa mipango miji jambo alilodai kuwa litaharakisha maendeleo kwa kuhamasisha uwekezaji toka mataifa mbalimbali

0 comments:

Post a Comment