.

.
Wednesday, July 2, 2014

Na Bertha Mollel
 
ALIYEWAHI kuwa mlinzi wa Rais wa zamani wa Gabon, Omar Bongo, Jin Yung Kim, ameanza kuwanoa walimu wa mchezo wa taekwondo mjini Arusha katika mafunzo yaliyoanza juzi.
Awali Shirikisho la Taekwondo (TTF), lilitegemea washiriki 30 kutoka mikoa ya Kilimanjaro, Simiyu, Kagera, Mwanza, Dar es Salaam, Arusha pamoja na Serengeti, lakini hadi mafunzo hayo yanafunguliwa, washiriki walikuwa ni 17 tu, hivyo 13 walikuwa bado kuripoti.
Mafunzo hayo ya siku 12 yaliyozinduliwa na Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi, ni sehemu ya mikakati ya kuleta mageuzi ya mchezo huo nchini.
Mafunzo hayo yataendeshwa na mtaalamu wa Shirikisho la Taekwendo la Dunia (WTF), kutoka Korea ya Kusini, Jin-Yung Kim na kuratibiwa kwa upande wa utawala na Samwel Mwera wa TOC na Makamu Mwenyekiti wa TTF, Joseph Chuwa kwa upande wa ufundi.
Akizindua mafunzo hayo, Bayi aliupongeza uongozi wa TTF kwa kufanikisha mafunzo hayo sio tu kuanza kwa muda uliopangwa, pia kwa ushirikiano na WTF, kumpata mkufunzi kijana na mahiri kutoka Korea ya Kusini, Jin Yung Kim.
“Nimefahamishwa, Kim ni mtaalamu, mpiganaji na mkufunzi mzuri vile vile kwa kutambua vipaji vya wachezaji wa mchezo wa taekwondo.
“Umahiri wake huo, ndio uliomfanya wakati fulani hapo nyuma kuwa mlinzi wa Rais wa Gabon, marehemu Omar Bongo. Ni matumaini yangu mtafaidika na mafunzo yake,” alisema Bayi.
Alisema mara ya mwisho anakumbuka mafunzo kama hayo yalifanyika jijini hapa mwaka 2006, kwa WTF kumleta mkufunzi Sang Min– Baik kutoka Korea ya Kusini.
“Ndugu Makamu Mwenyekiti (Chuwa), mafunzo haya ni ya gharama yanayogharimiwa na Olimpiki Solidarity kupitia Kamati ya Olimpiki Tanzania, nashauri washiriki watakapomaliza mafunzo haya, wawe na chachu ya kuuendeleza mchezo wa taekwondo katika maeneo na mikoa yao wanayotoka,” alisisitiza Bayi.
Aliwaomba TTF kuweka jitihada kubwa katika kuwekeza kwenye shule kwa vijana wadogo, ambao ni rahisi zaidi kuwafundisha kwa kuwa na unyumbufu mkubwa.
Aliwaomba TTF kuandaa mashindano ya mara kwa mara ya taekwondo kwa ngazi mbalimbali, hasa kuhusisha klabu au mashirikisho ya mikoa kama yapo, kwani bila kufanya hivyo, uongozi hauwezi kutambua matunda ya walimu hao wanaonolewa.
Chanzo, tanzania daima

0 comments:

Post a Comment