.

.
Wednesday, July 9, 2014

11:22 PM

Mmoja wa vigogo wa Friends na ambaye pia ni Katibu wa Kamati ya Usajili ya Simba, Kassim Dewji. 


FRIENDS of Simba wamesikia kelele na tambo za Yanga hasa baada ya kutua kwa Wabrazili Marcio Maximo (kocha) na Andrey Coutinho Kiungo), wamecheka sana kisha wakatamka jambo moja kwa mashabiki kwa wao kwa kusema: “Tulieni fitna zote za mpira tunazijua.”
Kundi hilo ambalo limeahidi kumaliza usajili wa Simba wiki hii na kuingiza timu kambini lipo karibu na uongozi uliopo madarakani na limetenga fungu lisilopungua Sh300 milioni kuhakikisha Simba inarudi kwenye hadhi yake. Imebainika kuwa  kambi haitakuwa karibu na macho ya Yanga wala Azam ambao ndio wapinzani wao wakubwa.
Mmoja wa vigogo wa Friends na ambaye pia ni Katibu wa Kamati ya Usajili ya Simba, Kassim Dewji, ameliambia Mwanaspoti kuwa wanasikia kelele za watani wao juu ya mambo mengi,  lakini wao wameamua kunyamaza wanafanya mambo yao kwa vitendo na majibu yataonekana uwanjani.
Dewji alisema kuwa majigambo ya Maximo na wadau wengine wa Yanga hayawatishi kwani wanachokifanya wao kwa sasa wanakijua na uongozi uliopo madarakani unajitambua tofauti na miaka ya nyuma na wana ufahamu mkubwa wa kila fitina inayofanyika ndani na nje ya uwanja kwenye Ligi Kuu Bara.
“Tunawasikia kelele zao na wala hazituumizi sisi tunafanya yetu, msimu ujao ndiyo watajua tulikuwa tunafanya nini, hatutaki kupiga kelele juu ya usajili hata kama watasema timu ni mbovu lakini kikubwa ni ushindi na mashindano ya kimataifa Simba itashiriki.
“Wanasimba wasipate taabu na ujio wa kocha wa Yanga, Maximo ni kocha mzuri lakini ni wa kawaida tu, kwa sasa tunajipanga juu ya usajili,” alisema Dewji.
Alisema kuwa baada ya Rais wa Simba, Evans Aveva kuunda Kamati zake, kila mjumbe atakuwa na jukumu la kutekeleza kazi yake aliyopewa ambapo wao wanahakikisha kumaliza suala la usajili wiki hii.
Tayari kamati hiyo imeanza michakato wa kuwasajili straika wa Kenya Raphael Kiongera anayekipiga klabu ya KCB, kipa Hussein Sharif ‘Cassilas’ wa Mtibwa Sugar Sugar, Mkenya Jerry Santo na Deus Kaseke kutoka Mbeya.
Mabeki Joram Mgeveke na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ tayari ni mali halali ya Simba.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Simba, zimesema kuwa mazoezi ya timu hiyo yataanza kesho Jumatano kati ya viwanja vitatu vilivyopendekezwa ambavyo ni Kunduchi, Chuo Kikuu na Chuo cha Sheria.
Amissi Tambwe, Joseph Owino na Donald Mosoti wao imeelezwa watawasili siku yoyote kwani suala lao la usafiri linashughulikiwa.

0 comments:

Post a Comment