.

.
Friday, November 28, 2014

2:11 AM
http://dewjiblog.com/wp-content/uploads/2014/08/215.jpg
Dk Margaret Zziwa.


Dar es Salaam.
 Bunge la Afrika Mashariki limemsimamisha kwa siku 21 Spika wake, Dk Margaret Zziwa huku likifufua hoja ya kumwondoa kiongozi huyo madarakani ambayo iliwekwa kando Aprili 1, mwaka huu.


Kadhalika, Bunge hilo liliafiki hoja iliyotolewa na mbunge kutoka Tanzania, Abdullah Mwinyi ya kumzuia Dk Zziwa kujihusisha na shughuli zozote za nafasi ya Spika mpaka hapo uchunguzi dhidi ya tuhuma dhidi yake utakapokuwa umekamilika na kuwasilishwa bungeni.


Uamuzi wa Bunge hilo ulifikiwa juzi mchana, ikiwa ni hitimisho la mkutano wa saa nne ambao ulimchagua mbunge kutoka Uganda, Chris Opoka-Okumu kusimamia mchakato wa kumwondoa Dk Zziwa madarakani kwa mujibu wa kanuni za uendeshaji wa Eala.

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgMcREAJO2eHsa90YMaEJ5X2MWlCh2Hrt0LdmpFwZNjvTApab4mYYdp36L8509fI3L4eLIxR7LRPl-D7_IhoHvQ2Cf0mwKkOr5RiraLp1i_mSYXTuGE2EvrCID7fvK9kcZY4hMilT9cbKkL/s640/shy-rose.jpg 
Shy-Rose Banji.
Taarifa ya kusimamishwa kwa Zziwa imewekwa katika tovuti ya Eala ikionyesha chini ya uongozi wa Okumu, Kamati ya Sheria, Kanuni na Haki ya Eala imepewa siku 21 kuchunguza tuhuma zinazomkabili ili kubaini iwapo alikiuka sheria na kanuni za uendeshaji wa Bunge kiasi cha kusababisha taasisi hiyo kushindwa kutekeleza wajibu wake.


Msemaji wa Eala, Bobi Odiko aliliambia gazeti hili jana kuwa kusimamishwa kwa Spika Zziwa kunamaanisha kwamba Bunge hilo halitaweza kukutana tena kwa siku chache zilizobaki hadi pale kamati itakapokuwa imemaliza kazi yake.


“Siwezi kusema kwamba lini Bunge litakutana na kukutana kwake kutategemea mambo mengi ikizingatiwa kwamba Spika amesimamishwa, kwa hiyo tusubiri siku hizo 21 zipite ili kamati ikamilishe kazi yake,” alisema Odiko.


Habari zaidi kutoka Nairobi ambako Bunge hilo linaendelea na vikao vyake zinasema uamuzi wa kumweka kando kisha kuanza kumchunguza Dk Zziwa uliibuliwa Jumanne jioni muda mfupi baada ya spika huyo kuamua kuahirisha kikao baada ya kutoa uamuzi ambao haukukubaliwa na wabunge karibu wote waliokuwamo ukumbini. Uamuzi huo ni wa kutangaza kufuta mchakato wa kumwajibisha Mbunge wa Tanzania, Shy-Rose Bhanji uliofikiwa katika kikao kilichomalizika mjini Kigali, Rwanda.


mwishoni mwa Oktoba, 2014 kwa maelezo kwamba uwasilishaji wa hoja husika na mchakato wa majadiliano haukuzingatia kanuni.


Badala yake, Zziwa alisema taarifa rasmi za mjadala huo zitakuwa moja ya nyaraka za siri za EALA hatua iliyopingwa na wabunge wengi.


Shy-Rose anatuhumiwa kufanya vurugu na vitendo vingine vya ukiukwaji wa maadili wakati wa ziara ya viongozi waandamizi wa EALA katika Makao Makuu ya Jumuiya ya Ulaya (EU), Brussels, Ubelgiji.


Wakati wa kikao cha Kigali, ilitolewa hoja ya kumvua ukamishna wa Bunge hilo lakini uamuzi haukufanyika baada ya kukosekana kwa akidi ya wabunge kutoka Tanzania.


Kwa mujibu wa kanuni za EALA, hoja hiyo ilipaswa kuwa ya kwanza katika kikao cha sasa na ilipaswa kuendelezwa katika hatua ya wabunge kupiga kura, suala ambalo halikufanyika kutokana na uamuzi wa Dk Zziwa kutangaza kufuta mchakato wa hoja hiyo.


Baada ya Bunge kuahirishwa Jumanne jioni, wabunge karibu wote walikutana juzi asubuhi na kuandika waraka kwa Katibu wa EALA ambao ulisainiwa na wabunge 33 kati ya 44 wa kuchaguliwa, wakimtaka afike katika ukumbi ili waweze kufanya uamuzi wa kumchunguza spika.


Katibu wa EALA, alifika ukumbini hapo juzi saa 6.30 mchana, hatua iliyowezesha kufanyika kwa mchakato wa kumchagua, Okumu kisha kutolewa kwa hoja ya kufufua mchakato wa kumchunguza kisha kumwondoa madarakani Dk Zziwa.


Naye Mwanasheria wa EALA alisema asingeweza kutoa mwongozo kwa wakati huo mpaka akasome kwanza hansard, hivyo walikubaliana kukutana juzi asubuhi ambapo alitoa mwongozo uliowawezesha wabunge kusaini waraka wa kumwita Katibu wa EALA. Uamuzi huo ulifanywa mbele ya mawaziri wa nchi zote, isipokuwa Rwanda ambayo haikuwa na mwakilishi.


MWANANCHI

0 comments:

Post a Comment