.

.
Thursday, August 14, 2014


timu ya maveterani ya Kivale fc ya jijini Dar (wenye jezi ya blue) wakichuana vikali na timu ya Ushirika ya Moshi (wenye njano) kwenye fainali ya bonanza la maveterani iliyofanyika katika uwanja wa sheik Amri Abeid ya ARUSHA
 
Na Bertha Ismail - Arusha

Timu ya Ushirika ya mjini Moshi imefanikwa kuwa washindi katika bonanza la maveterani baada ya kuichapa timu ya Kivule ya jijini Dar- es-salaam kwa magoli 2-0 katika uwanja wa Sheik Amri Abeid ya jijini Arusha.

Bonanza hilo lililoandaliwa na timu ya maveterani ya jijini Arusha “All Stars” lilihudhuriwa na timu sita za maveterani kutoka mikoa mbalimbali ya hapa nchini ambapo walishindana katika kusakata soka huku wenyeji Arusha wakionekana kutamba dakika za awali na baadae kuzidiwa nguvu na timu za wageni na kuzima ndoto za kutwaa ubingwa.

Katika bonanza hilo, timu za maveterani zilizokuwa kundi ‘A’ ni pamoja na timu ya Mwanza Veterani “Mwanza starehe”, Dar-es-salaam “Kivule” pamoja na Dodoma Veterani, huku zilizokuwa kundi ‘B’ ni pamoja na Arusha All Stars, Ushirika na Namanga Veterani.
Michuano hiyo iliyokuwa ikichezwa kwa dakika 30 ilifunguliwa dimba na wenyeji, Arusha all stars na Namanga ambapo timu ya Arusha ilifanikiwa kuichapa Namanga kwa magoli 2-0, mechi iliyofuatiwa na timu ya Kivule ya Jijini Dar na kuichapa Dodoma Veterani kwa goli 1-0.
Timu ya Namanga ilizidi kuonewa baada ya kushuka dimbani na timu ya Ushirika ya Moshi na kugaragazwa 1-0, ambapo Timu ya Dodoma walitoshana nguvu na timu ya Mwanza Veterani baada ya kumaliza mchuano bila kufungana, na baada ya mchuano huo timu ya Arusha all Stars ilishuka dimbani tena kuminyana na timu ya Ushirika ya Moshi lakini wenyeji hao walionekana kuzidiwa nguvu na majirani zao baada ya kufungwa goli 1-0.
Baada ya michuano hiyo kila kundi lilitoa mshindi, ambao ni Arusha All Stars pamoja na Mwanza Starehe na kushuka dimbani ambapo Arusha ilifanikiwa kuichapa Mwanza 1-0, huku Kivule ya Dar-es-salaam ikishuka Dimbani na timu ya Ushirika ya Mjini Moshi ambapo Kivule ilizidiwa nguvu dakika za mwisho na kuchapwa magoli 2-0 mfululizo.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa waandaji wa bonanza hilo, Laurence Sabuni, alisema kuwa kufuatia ushindi huo wa Timu ya Ushirika ya Moshi itazawadiwa kikombe kikubwa huku mshindi wa pili ambae ni Kivule ya jijini Dar-es-salaam ikizawadiwa kikombe kidogo ambazo hata hivyo hadi bonanza linafikia tamati majira ya saa 12:30 jioni vikombe hivyo havikuwasili eneo la tukio.
Wakizungumzia Matokeo hayo, Tumaini Andrew wa timu ya Ushirika Pamoja na Joseph Mbewa wa timu ya Kivule ya Dar walisema kuwa matokea hayo ni ya haki wala hakuna wa kumlaumu kwani katika mashindano yeyote ile kuzidiana kupo hivyo kutumia udhaifu wa mwenzio kupata ushindi ni sawa zaidi kuliko kutumia ubabe kununua ushindi.
Aidha bonanza hilo la maveterani hufanyika kila mwaka mwezi wa nane kwa kuzunguka mikoa mbalimbali kwa lengo la kuwaenzi maveterani watatu (Francis Lungu, Judicate Estomili, Amani Mwalim) wa timu ya All stars waliofariki mwaka 1999 kwa ajali mbaya ya gari eneo la Mwanga mkoani Kilimanjaro walipokuwa wakitokea jijini Dar-es-salaam kwenye mashindano ya maveterani wa mikoa mbalimbali hapa nchini na wengi kujeruhiwa.
Mwisho……..
 
 

0 comments:

Post a Comment