.

.
Wednesday, August 20, 2014

11:01 PM
WAANDISHI wawili wa habari wa Kampuni ya New Habari (2006), wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha wakikabiliwa na kosa la kupokea rushwa ya sh.150,000 kutoka kwa mmiliki na Chuo cha Savana Bridge, kilichopo jijini hapa.
Waandishi hao, Isack Longwe (28) mkazi wa Tegeta, Tanki bovu na Fredy Okoth (36) mkazi wa Kimanga Tabata jijini Dar es Salaam, wanadaiwa kushawishi kupatiwa sh. laki tatu ili waharakishe usajili wa chuo hicho kwenye Baraza la Taifa la Vyuo vya Ufundi (Nacte).
Walifikishwa mahakamani jana na kusomewa mashtaka  mawili ya kushawishi na kupokea rushwa na Mwanasheria wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru), Vailet  Machali mbele ya Hakimu Mkazi, Rose Ngoka.
Alidai kuwa washtakiwa hao walikamatwa Agosti 16 mwaka huu mchana, baada ya kupokea kiasi hicho cha fedha ikiwa ni sehemu ya sh. 300,000 walizokuwa wameshawishi kupatiwa.
Akiwasomea maelezo ya kosa, Ngoka aliieleza mahakama hiyo kuwa washtakiwa wote kwa pamoja mnamo Agosti 14 mwaka huu, wakiwa Jiji la Arusha walimshawishi mmiliki ambaye pia ni Mkuu wa chuo hicho, Mselemu Kombe kuwapatia sh. 300,000, ili wakaharakishe usajili wake Nacte.
Katika shtaka la pili, washtakiwa hao walidaiwa kuwa Agosti 16 mwaka huu, majira ya mchana, walipokea rushwa ya sh.150,000 toka kwa Mselemu kwa lengo hilohilo.
Ngoka alidai kuwa washitakiwa hao walifanya makosa hayo huku wakijua wao kama waandishi wa habari hawawezi kufanya shughuli za usajili wa chuo.
Hadi Tanzania Daima linaondoka mahakamani hapo, waandishi hao walikuwa rumande ya mahakamani hapo wakisubiri kupata wadhamini wawili wenye vitambulisho na mali isiyohamishika yenye thamani ya sh. milioni moja, vinginevyo wangepelekwa gereza la Kisongo hadi Septemba 2, mwaka huu, shauri hilo litakaporudi kwa ajili ya kutajwa.

chanzo tz daima

0 comments:

Post a Comment