.

.
Sunday, August 10, 2014


Wanawake wanaoendesha magari katika Jiji la Arusha, wamekumbwa na hofu kutokana na kuibuka watu  wasiojukikana ambao wanawashambulia kwa risasi.
Washambuliaji hao ambao hutumia pikipiki, katika siku saba wamemuua mwanamke mmoja na kuwajeruhi wanne kwenye matukio tofauti lakini bila kuiba chochote.
Mwanamke aliyeuawa ni Shamim Rashid, mkazi wa Sakina baada ya kupigwa risasi alipokuwa akijiandaa kuingia nyumbani kwake juzi , tukio ambalo limekuja takriban siku tatu tangu mwanamke mwingine, Frola Porokwa kunusurika kifo.
Porokwa mke wa mkurugenzi wa Shirika la Pingos a Forums, Edward Porokwa, alipigwa risasi akiwa jirani kuingia nyumbani kwake kwake pia eneo la Sakina, iliyompata pembeni ya kifua na kutokea mgongoni.
Katika matukio yote mawili, watuhumiwa hao hawakupora chochote huku wakitoweka na pikipiki zao aina ya boxer .
Wakizungumza na mwananchi Juzi katika msiba wa Shamin, baadhi ya waombolezaji walitaka Jeshi la Polisi kuimarisha uchunguzi juu ya matukio hayo.
“ Tunaimani na jeshi letu litawakamata wahusika, lakini jambo hili linatutia hofu wanawake kuendesha magari usiku,”alisema Khanifa Haji.
Kufuatia matukio hayo Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, limeanza msako mkali dhidi ya watuhumiwa hao.
Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Liberatus Sabas alisema katika kukabiliana na uhalifu huo  jeshi lake , Serikali kwa kushirikiana na wadau wataweka Kamera maalumu zenye uwezo za kubaini vitendo viovu kwenye sehemu mbalimbali ili iwe rahisi kuwakamata wahusika.
“Msako mkali umeanza na tuna uhakika wa kuwakamata watuhumiwa hawa na wengine,”alisema.
Wakati huo huo, polisi imefanikiwa  kumkamata Adam Mussa Pakasi mkazi wa Siwandeti wilayani Arumeru akiwa na  bunduki iliyotengenezwa kienyeji inayotumia risasi za Shotgun,risasi 38 na ganda moja la risasi iliyotumika pamoja na mafuta ya kusafishia bunduki.
Sabas alisema matukio ya uhalifu yanayohusiana na kupotea kwa maisha ya watu ni miongoni mwa mambo nyeti yanayochunguzwa kwa umakini na tahadhari.

0 comments:

Post a Comment