CHAMA cha Ushirika cha Wakulima wa Korosho Tandahimba – Newala
(Tanecu) kinatarajia kuzindua maghala ya kuhifadhia korosho katikati ya
mwezi huu ikiwa ni hatua za awali za ujenzi wa kiwanda cha kubangua
korosho nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Tanga baada ya ziara ya
kutembelea kiwanda cha kusindika maziwa cha Tanga Fresh, Mwenyekiti wa
chama hicho, Yusuph Nannila, alisema Rais Jakaya Kikwete ndiye
atakayefungua maghala hayo.
Alisema hatua iliyofikiwa mpaka sasa ni kukamilika kwa hatua za
mwishoni za maghala hayo ambapo kwa upande wa ujenzi wa kiwanda,
wameshapokea michoro na kwamba kiwanda wanatarajia kujengwa kwa ubia
kati ya chama chake na Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB).
Nannila alikipongeza Kiwanda cha Tanga Fresh kwa kumudu ushindani wa
soko la ndani wakati korosho zinategemea zaidi soko la nje ambalo
halina uhakika na halimnufaishi mkulima.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji wa Ng’ombe wa Maziwa, Rajabu Kihara,
alisema siri ya mafanikio waliyopata katika chama hicho mpaka
kuanzisha kiwanda ni ushirikiano mzuri na wanachama wao pamoja na
uaminifu wa viongozi wao.
0 comments:
Post a Comment