MVUTANO wa muundo wa serikali mbili au tatu uliogubika Bunge Maalumu,
umelifanya Baraza la Mahusiano ya Dini mbalimbali kwa Amani Tanzania
(IRCPT), kutaka kura ya maoni ifanyike ili wananchi waamue muundo wa
muungano.
Baraza hilo limebainisha kuwa viongozi wa dini watakubali kupiga kura
ya maoni kuhusu mapendekezo ya Katiba ambayo yamezingatia maoni
yaliyotolewa na wananchi.
Msimamo wa baraza hilo umo ndani ya kitabu cha mapendekezo kwa
wajumbe wa Bunge Maalumu kuhusu rasimu ya Katiba, walichokisambaza juzi
kwa wajumbe wa Bunge Maalumu.
Mratibu wa baraza hilo, Thomas Goda, alisema miongoni mwa taasisi
zinazounda baraza hilo ni Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), Baraza
la Kikistro Tanzania (CCT), Baraza la Makanisa ya Kipentekosti Tanzania
(BMKT), Tanzania Asian Development Association (TADA) na Tanzania
Episcopal Conference (TEC).
Goda, alisema kuwa wajumbe wa baraza lao walikutana Machi 26, mwaka
huu jijini Dar es Salaam ambapo waliijadili na kuichambua rasimu ya
Katiba inayojadaliwa hivi sasa na wajumbe wa Bunge Maalumu.
Alisema baada ya kujadili na kuchambua rasimu hiyo wamebaini giliba
za kisiasa, malumbano, jazba, tofauti za kiitikadi na kutozingatia
kanuni ndizo zimetawala majadiliano ya Bunge Maalumu hivyo kutia doa
safari ya kupatikana Katiba yenye kujumuisha makundi mengi.
Alibainisha kuwa wameandika kitabu chenye kurasa 12 kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza zilizo na mapendekezo 14.
Tanzania Daima Jumapili, imepata nakala ya kitabu hicho ambacho
katika ukurasa wa sita pendekezo namba moja linawataka wajumbe waheshimu
rasimu ya Katiba iliyobeba maoni ya wananchi na kuifanyia kazi kwa
lengo la kuiboresha.
Pendekezo jingine ni kuwataka wajumbe wajadiliane kwa upendo,
kuheshimiana na kuthaminiana bila kuathiriwa na mawazo pandikizi,
masilahi binafsi, vyama, kabila au eneo la mjumbe.
Katika ukurasa wa nane wa kitabu hicho, 3.1, baraza hilo linataka
wananchi waachiwe waamue kwa kupitia kura ya maoni juu ya muundo wa
serikali.
Mapendekezo hayo pia yanataka Katiba itatambue uwepo wa mamlaka ya
Mungu, sifa za rais awe mwana ndoa, ndoa ni kati ya mume na mke, itoe
mwongozo wa matumizi ya rasilimali za taifa na ukusanyaji kodi, rais
anayemaliza muda wake aondolewe kinga kama sehemu ya kujenga uadilifu na
uwajibikaji.
Katika ukurasa wa 11 kitabu hicho kinataka kiongozi aliyefukuzwa au
kujiuzulu kwa kukiuka miiko na maadili ya uongozi asigombee na
asiteuliwe tena katika nafasi yoyote ya uongozi.
Mengine ni katiba itenganishe kuingiliana kwa mihimili mikuu mitatu
ya dola; Serikali, Bunge na Mahakama (uteuzi wa wabunge watano usifanywe
na rais, mawaziri wasiwe wabunge).
Katiba itambue kwa makusudi kuwepo uwakilishi wa baraza la viongozi
wa dini na wazee wenye busara kuishauri serikali mambo ya kisheria na
mambo yote nyeti ya kitaifa.
Viongozi wote wanaoteuliwa au kuchaguliwa nafasi ya uongozi, uadilifu
wao lazima uthibitishwe na Tume ya Maadili kabla ya kuteuliwa au
kuchaguliwa.
Naye mjumbe wa baraza hilo, Ali Mose, alisema wameingiwa na wasiwasi
mkubwa kama Katiba iliyotarajiwa itapatikana, kwakuwa watu wameweka
mizizi ya kiitikadi ambayo inakwamisha wajumbe kusikiliza hoja za upande
mwingine.
Alisema kuna hatari ya kupatikana kwa Katiba isiyoyaunganisha makundi
yote, jambo ambalo ni hatari na doa, kwa kuwa Katiba inajengwa katika
misingi ya maridhiano.
‘Viongozi wa dini tuna jukumu la kuwaunganisha wajumbe ili maridhiano
yafikiwe na taifa lipate Katiba nzuri itakayowafurahisha Watanzania
wote,” alisema.
0 comments:
Post a Comment