MATUMAINI ya kumpata mshitakiwa namba moja katika kesi ya
kusafirisha wanyama hai wakiwamo twiga wanne kwenda nchini Qatar,
Kamran Ahmed, yameyeyuka baada ya jana mshitakiwa huyo kutofika tena
mahakamani.
Mshitakiwa huyo amekuwa hafiki mahakamani kwa mara ya nne sasa
huku kukiwa hakuna taarifa rasmi za kutofika kwake kutoka kwa wadhamini
wake wala wakili wake, Edmund Ngemela.
Kesi hiyo ilikuja kwa kutajwa jana mbele ya Hakimu Mkazi, Simon
Kobelo, anayesikiliza shauri hilo na baada ya mshitakiwa huyo kushindwa
kufika mahakamani.
Mahakama imepanga kuanza kusikiliza kesi hiyo mfululizo Mei 6 na 7 mwaka huu.
Wakili wa Serikali, Patrick Mwita, aliiambia mahakama jana kuwa
mshitakiwa huyo hakufika mahakamani na kusisitiza hati ya kukamatwa
iendelee kuwa pale pale kama ilivyoamuliwa na mahakama.
Tayari upande wa mashitaka umeanza kufuatilia anwani za wadhamini
wa mshitakiwa huyo, ili wakamatwe kutokana na kutofika mahakamani kutoa
taarifa juu ya mshitakiwa huyo kama masharti ya dhamana yanavyoagiza.
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Hawa Mang’unyuka, Martin Kimath na Michael Mrutu ambao wote wako nje kwa dhamana.
Washitakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kusafirisha wanyama hao hai
Novemba 26, mwaka 2010 kwenda Qatar kupitia Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), wanyama wanaodaiwa kukamatwa maeneo ya
Mto wa Mbu, Elboret na Engaruka wilayani Monduli, mkoani Arusha.
Wanyama hao wenye thamani ya sh milioni 170.5 wanadaiwa kusafrishwa
kwenye maboksi marefu ndani ya ndege kubwa ya jeshi la Qatar.
0 comments:
Post a Comment