Pages

Pages

Thursday, May 29, 2014

kinana: kuwanyang'anya wawekezaji mashamba Hanang'

Hanang. 
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana amesema wawekezaji kutoka nje walioshindwa kuyaendeleza mashamba ya ngano ya Bassotu na Wareti, wilayani Hanang mkoani Manyara, watanyanganywa mashamba hayo.
Akizungumza na wananchi wa wilaya hiyo juzi kwenye mji mdogo wa Katesh baada ya kupokewa kutoka mkoani Singida, Kinana alisema atalifikisha suala hilo kwa Rais Jakaya Kikwete ili mashamba hayo yarudishwe kwa wazawa.
Inadaiwa kuwa wawekezaji kutoka nje, ikiwamo kampuni moja ya Kenya, imekuwa ikiwakodisha wananchi mashamba hayo kulima mahindi badala ya wao kulima ngano kama mkataba ulivyosainiwa.
“Hatuwezi kukubali kuwavumilia wawekezaji walioshindwa kuendeleza mashamba waliyopewa na badala yake wanawakodisha wananchi wetu...sasa nini maana ya uwekezaji wenye tija?,” alihoji Kinana.
Alisema kuwa atalifikisha suala hilo kwa Rais Kikwete ili wawekezaji hao wanyang’anywe na kupewa wakulima wa maeneo ya Hanang’.
Aliongeza: “Mashamba haya lazima yarudishwe kwa wananchi kama wawekezaji wameshindwa kutimiza masharti ya mkataba kulima ngano.”
Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Rose Kamili aliwahi kumwomba Rais Jakaya Kikwete kuwanyang’anya wawekezaji hao mashamba kwa vile wamekiuka taratibu na kuwakodisha wananchi.
Kamili alitoa ombi hilo wakati Rais Kikwete alipofanya ziara mkoani Manyara, Desemba mwaka 2012.
“Tunataka mashamba ya ngano yaendelee kulimwa ngano na siyo wawekezaji kuyakodisha kwa wananchi ambao wanalima mahindi,” alisema Rais Kikwete katika ziara hiyo.

NDOA YA VICKY KAMATA BADO MATATANI

Dar es Salaam. 
 Suala la kukwama kufungwa kwa ndoa ya Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Vicky Kamata limechukua sura mpya baada ya mzazi mwenza wa mchumba wa mbunge huyo, kukanusha taarifa kwamba alikwenda Dodoma kwa lengo la kuomba msaada kwa viongozi wa Bunge.
Kauli ya mama huyo imezidisha utata katika sakata la kukwama kufungwa kwa ndoa hiyo iliyokuwa ifanyike Jumamosi baada ya kutokea habari kuwa mwanamke mmoja alikwenda bungeni mjini Dodoma kutaka kuonana na Spika kwa lengo la kuomba Bunge limsaidie kupata haki yake kabla ya harusi hiyo kufungwa na hivyo kusababisha harusi kutofanyika.
Kamata, ambaye alijizolea umaarufu kutokana na wimbo wake wa “Wanawake na Maendeleo” na baadaye kuingia bungeni katika uchaguzi wa mwaka 2010, alikuwa afunge ndoa na mtu aitwaye Charles Gardiner Jumamosi iliyopita jijini Dar es Salaam, lakini haikufanyika kutokana na mbunge huyo kuwa mgonjwa kiasi cha kulazwa hospitali maeneo ya Tabata.
Jana, Kinavi Dadi, ambaye ni mzazi mwenza wa Gardiner, alikanusha kufunga safari hadi Dodoma kwa lengo hilo.
“Ni kweli kwamba Charles ni baba watoto wangu, lakini sijawahi kwenda Dodoma na wala sifahamu chochote kuhusu safari hiyo. Nadhani inatosha,” alisema mama huyo na hakutaka mazungumzo zaidi.
Baadaye kidogo mmoja wa ndugu wa Kinavi, ambaye aliomba asitajwe jina lake gazetini, alikiri ndugu yao kufunga ndoa na Gardiner Juni 2004 na kujaliwa kupata watoto wawili, lakini walitofautiana na baadaye ndoa yao kuvunjwa mwaka 2012.
“Ni kweli kwamba dada yetu alifunga ndoa na Charles, lakini pia ni kweli kwamba walipeana takala halali two years ago (miaka miwili iliyopita), kwa hiyo taarifa kwamba eti amezuia ndoa isifungwe, siyo za kweli na wala huko Dodoma hajawahi kwenda,” alisema.
Alisema taarifa kwamba aliyepata kuwa mke wa Gardiner alikwenda Dodoma kuomba msaada wa Bunge zimewaumiza sana kama familia kutokana ukweli kwamba Kinavi ndiye anayefahamika kuwa mke wa kwanza.
“Ndugu yetu analia sana kutokana na kuumizwa na wale wanaomchafua. Sisi katika familia tumelelewa kwa maadili hivyo Kinavi siyo mtu wa kuzuia ndoa ya Gardiner maana walishatengana, mawasiliano yaliyopo ni yale yanayohusu watoto ambao wana haki ya wazazi wote wawili. Hatujui waliozitangaza hizo habari walikuwa na malengo gani,” alisisitiza.
Bungeni Dodoma
Wakati hayo yakiendelea, habari kutoka bungeni Dodoma zinasema mwanamke aliyedaiwa kuwa mke wa Gardiner ni ‘feki’ na alikuwa wa kutengenezwa na baadhi ya wabunge kwa lengo la kumtibulia Kamata.
Mpango huo unadaiwa kuwahusisha wabunge wanawake wanne; watatu kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) na mmoja kutoka Chadema ambao awali waliapa kwamba ndoa ya mbunge mwenzao isingefungwa.

Wednesday, May 28, 2014

. MADAKTARI WAKUNA VICHWA KUREJESHA AFYA YA MTOTO NASRA


Nasra akiwa katika hospitali ya mkoa wa Morogoro.

MTOTO mwenye umri wa miaka minne aliyefungiwa ndani ya boksi kwa zaidi na miaka mitatu mkoani Morogoro, amehamishiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa ajili ya uchunguzi na tiba zaidi huku wataalamu wakikuna vichwa namna ya kumrudishia afya yake. Imeelezwa jopo la madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali ya binadamu wakiwemo wataalamu wa saikolojia, wanahitajika kwa ajili ya kumwezesha mtoto huyo mwenye ulemavu kuwa katika hali ya kawaida.

Aidha, pamoja na uhitaji wa jopo la wataalamu hao, mtoto huyo ambaye amelazwa katika wadi ya watoto, atahamishiwa katika wadi maalumu ya watoto wenye utapiamlo awe karibu na uangalizi wa lishe baada ya kubainika ana udhaifu mkubwa wa lishe.

Wakizungumza na gazeti hili jana jijini Dar es Salaam kwa nyakati tofauti hospitalini hapo, Daktari Bingwa wa Watoto wa MNH, Dk Mwajuma Ah- mada alisema mtoto huyo hajazidiwa kuumwa.

Alisema walimpokea juzi usiku na hatua za awali zilizofanywa ni pamoja na kuchukua baadhi ya vipimo kwa ajili ya uchunguzi.

“Mtoto aliletwa hapa jana (juzi) usiku, baadhi ya vipimo vimechuku- liwa, vingine atafanyiwa leo (jana) ikiwa ni pamoja na kumfanyia huduma ya kum scan (kumwingiza kwenye mashine maalumu) mwili mzima ili tufahamu tatizo na tiba sahihi,” alisema Dk Ahmada.

Alisema huduma ya tiba kwa mtoto huyo siyo ya daktari bingwa mmoja bali inahitaji jopo la wataalamu waki- wemo wa mifupa, saikolojia, viungo na magonjwa mbalimbali ya binadamu kumsaidia mtoto huyo.

“Kwa sasa hatuwezi kusema lolote kubwa kuhusu mtoto huyo ndio kwanza kafika na ndiyo tuko kwenye hatua ya awali ya kuchukua vipimo, na leo atafanyiwa huduma ya kumulikwa mwili mzima ili tujue tunaanzia wapi”, alisema Dk Ahmada.

Alisema pamoja na kusubiri majibu ya vipimo, hatua wanayochukua ni ya kumhamishia kwenye wadi ya watoto wenye utapiamlo, ili kutibu maradhi hayo ambayo ndio yameonekana awali, kwani mtoto amekosa lishe na viru- tubisho muhimu vya awali.

Alifafanua, katika hatua hiyo ya awali, mtoto huyo atakuwa akipewa maziwa ya lishe na kuendelea na tiba ya dawa za kuua vijasumu kutokana na kusumbuliwa na vichomi.

Akizungumzia kwa ufupi ikiwa mtoto huyo anaweza kurejea katika hali ya kawaida kwa viungo kunyooka na kutembea, Dk Ahmada alisema pamoja na kusubiri majibu ya vipimo, lakini pia tiba ya mtoto inategemea zaidi historia ya mtoto mwenyewe.

Mlezi azungumza Kwa upande wake, mlezi wa mtoto huyo , Josephina Joel akizungumza na gazeti hili wadini hapo alisema mtoto anaendelea vizuri ingawa juzi alikuwa na homa.

Hata hivyo alisema imeshuka, na kwamba kadri siku zinavyosonga, anaona uchangamfu wa mtoto.

Msanii mwingine Bongo Movie afariki dunia


Rachel HauleIKIWA zimepita siku chache tangu msiba wa mwigizaji na muongozaji filamu za Kibongo, Adam Kuambiana, mwigizaji mwingine, Rachel Haule ‘Recho’, amefariki dunia jana asubuhi.
Inaelezwa kifo cha Recho kimesababishwa na uzazi, ambapo alijifungua kwa upasuaji na mtoto kufariki. Kutokana na hali hiyo, alilazwa chumba maalumu cha uangalizi ‘ICU’ na baadaye kufariki dunia.
Mwenyekiti wa Bongo Movie, Steve Mengele ‘Steve Nyerere’, alisema msiba upo Sinza kwa Remmy jijini Dar es Salaam kwa mjomba wa marehemu.
Hata hivyo, Steve alisema wapo katika mchakato wa kuiomba familia kumzikia hapa jijini Dar es Salaam, ili wadau mbalimbali wa filamu waweze kushiriki mazishi yake, badala ya kwenda Songea kama wanavyotaka.
Recho alianza rasmi kuingia katika sanaa ya maigizo mwaka 2009, katika kikundi cha Mburahati, kabla hajajiingiza rasmi kwenye uigizaji wa filamu.
Moja ya sifa zilizomfanya kujulikana, ni tabia ya kupendelea kuvaa nguo fupi, jambo ambalo alipohojiwa, alisema zinamfanya ajisikie huru na amani pindi anapofanya shughuli zake.

Saturday, May 17, 2014

Biashara ya vyuma chakavu yaharibu barabara

BAADHI ya wananchi wilayani Hanang’, Manyara wameanzisha biashara ya uuzaji vyuma chakavu na kusababisha uharibifu wa miundombinu hasa ya barabara.
Mkuu wa Wilaya ya Hanang’, Christine Mndeme, alibainisha hayo juzi alipozungumza kwenye baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya na kueleza kuna watu wameanzisha biashara hiyo ambayo imekuwa ikichangia uharibifu  wa miundombinu.
“Biashara ya vyuma chakavu imeanza kushamiri mjini kwetu, serikali inahangaika kuboresha miundombinu ya barabara, watu wanaiharibu kwa kung’oa vyuma katika maeneo kadhaa na kwenda kuuza. Tusaidiane kudhibiti hali hii, ili kukomesha uharibifu wa miundombinu,” alisema.
Mndeme alibainisha kwamba kuna watoto walioanzisha zoezi la kulenga shabaha kwenye nguzo za umeme, jambo ambalo ni hatari kwao na kwa mji mzima kutokana na athari za umeme zitakapotokea pindi wanapolenga shabaha vikombe vinavyoshikilia kwenye nguzo hizo.
Mbali na hilo, alihimiza suala la usafi na kusema mazingira ya mji huo ni machafu hasa maeneo ya katikati ya stendi ambapo mapipa ya kuhifadhia takataka yanajaa bila wahusika kuyafanyia usafi na kusababisha harufu mbaya.

UFISADI BIL. 200 BoT: Vigogo waunda zengwe kukwepa

Reginald Mengi, Nimrod MkonoMKAKATI wa kuwanasua vigogo wa serikali wanaotuhumiwa kuhusika katika kashfa nzito ya ufisadi wa dola za Marekani milioni 122 (sawa na sh bilioni 200) katika akaunti ya Baraza la Usuluhishi la Migogoro ya Kibiashara (Escrow) ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), umeanza kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
Waraka ambao umeandikwa na mtu anayejitambulisha kama mhasibu wa Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco), unawataja Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi na Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono, kuwa ndio wanaeneza tuhuma hizo kwa lengo la kuwachafua Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wake, Eliachim Maswi.
Huu ni mnyukano unaotokana na tuhuma za Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), kuhusu vigogo sita wa serikali wakiwemo mawaziri kadhaa aliodai wamehusika na ufisadi wa fedha hizo zilizokuwa zimewekwa katika akaunti ya Escrow.
Kafulila aliwataja Waziri Muhongo na Katibu Mkuu wake, Maswi, Waziri wa Fedha Saada Mkuya, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Benno Ndullu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema na Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Mhandisi Felchesmi Mramba.
Alisema kuwa ufisadi huo ni lazima mbivu na mbichi zifahamike, na kwamba haungi mkono uamuzi wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wa kuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza suala hili kwa kuwa linagusa mamlaka kubwa katika dola, badala yake iundwe Kamati Teule ya Bunge.
Katika kile kinachoonekana kama mkakati wa kuhamisha hoja ya msingi, jana ulisambazwa waraka kwenye mitandao ya kijamii ukiwa umeandikwa kwa utaalamu wa hali ya juu ukisomeka “Sakata la IPTL mchezo wa wanasheria na wafanyabiashara”.
Mwandishi wa waraka huo anasema; “Mimi ni Mtanzania mwajiriwa wa Tanesco, kwa muda mrefu nimekuwa nikilifuatilia suala la IPTL linavyokwenda na linavyojadiliwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo bungeni.
“Naomba niwaeleze kwamba suala hili naona wengi hawalielewi, bali wanaongea kwa jazba na ushabiki kwa kitu wasichokijua kabisa na huenda labda wanatumiwa na watu wenye maslahi na Shirika letu la Tanesco,” alisema.
Alifafanua kuwa suala la Tanesco, IPTL na akaunti ya Escrow ni la kisheria zaidi na si suala la kisiasa, na kwamba tusipokuwa makini tutajikuta tunaingia katika masuala yasiyokuwa ya msingi na tukajuta baadaye.
“Mimi kama Mhasibu wa Tanesco, nakumbuka Escrow ilifunguliwa tarehe 5 July, 2006 wakati mkataba wa IPTL na Tanesco uliingiwa mwaka 1995 na lengo lake lilikuwa ni kuweka fedha za Capacity charges ambazo zilikuwa na mgogoro kutokana na Tanesco kupinga gharama hizo, lakini wakati huo huo walikuwa wakitumia umeme wa IPTL.
“Hata hivyo, IPTL tangu kuazishwa kwake ilianza kuingia kwenye mgogoro kutokana na wanahisa wenyewe kutokuelewana, sababu kubwa ikiwa ni kutokuaminiana hasa katika suala la mapato.”
Aliongeza; “Kampuni ya Merchmar iliyokuwa inamilikiwa na mwekezaji ambaye ni Rais wa Malaysia aliyekuwa na hisa asilimia 70 wakati mzawa Kampuni ya VIP Engineering aliyekuwa akimiliki hisa asilimia 30, kutokana na mgogoro huo wa kutokuelewana kwa wanahisa, Serikali ilimteua RITA mwaka 2011 kufilisi na kuuza mali zote za IPTL na baadaye kulipa madeni yanayodaiwa kampuni hiyo ya IPTL.
“Kwamba, hata hivyo bila serikali kushirikishwa huku IPTL ikielewa fika kwamba iko chini ya mfilisi, waliamua kuuza baadhi ya hisa zake kwa Benki ya Standard Chartered ya Hongkong.
“Wakati hayo yakiendelea, ghafla benki hiyo ya Standard Chartered ilifungua kesi tarehe 7 May, 2002 dhidi ya Serikali ya Tanzania bila kesi hiyo kusajiliwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania.
“Kutokana na kesi hiyo kushindwa kusajiliwa Tanzania, Benki ya Standard Chatered ya Hongkong hawana mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo. Tarehe 5, Septemba 2013, hukumu ilitolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania ya kuiondoa IPTL chini ya ufilisi wa RITA.”
Waraka huo unaongeza kuwa IPTL imenunuliwa na mwekezaji mwingine ambaye ni Pan Africa Power Solution (PAP) ambaye ndiye mmiliki halali wa IPTL, na kwamba amenunua hisa zote za Merchmar asilimia 70 na 30 za VIP.
Hukumu hiyo ilitolewa na mhimili mwingine wa dola ambao ni mahakama chini ya Jaji Utamwa ambaye aliamuru mali zote za IPTL zilikabidhiwe kwa PAP.
“Vile vile katika hukumu hiyo iliamuriwa fedha zilizokuwa katika akaunti ya Escrow nazo zitolewe na walipwe haki yao IPTL. Baada ya hukumu hiyo, wizara iliandika barua ya kuomba mwongozo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali juu ya uamuzi huo, na jibu ni kwamba wizara, BoT na Tanesco walitakiwa kutii uamuzi wa mahakama na kwa vile hakuna aliye juu ya sheria,” ulisomeka waraka huo.
Pamoja na mengi yaliyotajwa mle, anatuhumiwa mwanasheria wa Tanesco, Nimrod Mkono kuwa amekuwa akitumia fedha nyingi, lakini hadi sasa Tanesco haijawahi kushinda kesi hiyo ambapo tangu mwaka 2008, alikuwa akitumia sh bilioni 10 kila mwaka na hadi kufikia mwaka 2013 alikuwa ametumia sh bilioni 52. Serikali imekwishamlipa sh bilioni 35 na zilizobaki zimelipwa na Tanesco.
“Sasa mgogoro unaoanza ni pale alipokuja Waziri Muhongo na Katibu Mkuu, Maswi ambao pamoja na kwamba wanatoka mkoa mmoja wa Mara, lakini walimpinga waziwazi bila kuficha kwamba hawapo tayari kuona akiendelea kutafuna fedha za Tanesco namna hiyo na kusisitiza kutompatia kazi hiyo tena.
“Kama watu wanaweza kufanya tathmini ya haraka au uchunguzi wa kawaida tangu mwanasheria huyu asimamishwe kufanya kazi na Tanesco, mambo mengi yamekuwa yakizushwa pasipo na maana wala msingi wowote, mbona Mkono wakati anatafuna fedha za Tanesco suala la IPTL lilikuwa kimya,” unahoji waraka huo.
Unaongeza kuwa nguvu ya suala la IPTL na kumpinga Prof. Muhongo imezidi kuongezeka pale Mengi anapodai amenyimwa kuwekeza kwenye gesi.
“Hivi nani amemnyima Mengi kuwekeza kwenye gesi? Aende akachukue fomu ya kuwekeza, mbona haendi? Yeye anachotaka ni kuwa dalali ashike vitalu halafu akatafute wawekezaji ili afaidike yeye na mke wake Jaquiline, lakini Muhongo anakataa hilo, anataka dalali wa kuwaleta wawekezaji liwe Shirika la Taifa la Mafuta (TPDC),” aliandika.
Mwandishi anaongeza kuwa; “nimemtaja Mengi kwa kuwa sisi wafanyakazi wa Tanesco tunaelewa kwamba hao wote wameungana dhidi ya Prof. Muhongo kwa kuwa wanamuona amewanyima ulaji na kuanza kupambana naye kupitia wabunge na vyombo vya habari.”
Akizungumza kwa njia ya simu kuhusu tuhuma hizo, Mkono alisema hashangazwi na ujumbe huo unaoweza kuwa umetumwa na mahasimu wake kisiasa na kibiashara.
“Kuna baadhi ya wakubwa pale Wizara ya Nishati hawapendi ukweli… mwaka jana nilihoji kuhusu malipo ya fidia kwa wananchi wa Buhemba kutokana na athari walizopata kufuatia uwekezaji feki wa Kampuni ya Meremeta.
“Nikasema kwanini fedha zao zilielekezwa kufidia Kiwira, lakini wananchi wangu wanyimwe, hapo likawa kosa, nikaibua vidonda vya wakubwa na chuki zikaanza. Mfano mtu anasema nimefilisi BoT au Tanesco, kwanza namshangaa, je mimi nilienda BoT au Tanesco kuiba?”  alihoji.
Alisema kampuni yake ya uwakili ni ya kimataifa, na amekuwa akifanya kazi na taasisi hizo kwa maadili makubwa, tena akishirikiana na mawakili wengine toka nchi za India na Marekani.
“Na kesi zote tumekuwa tukishinda kwa kulisadia taifa, leo ukifika wakati wa kutakiwa kulipwa gharama zetu ndio mambo yanazushwa… kama nimeiba au kufilisi waende polisi au kwa vyombo husika si kwa kunitukana.
“Sijawahi kumlazimisha mtu au kampuni kufanya kazi ya kutetea taasisi yake, bali wanakuja wenyewe wakijua uwezo wangu katika taaluma hii, iweje waanze kuhoji gharama baada ya kumaliza kazi?” alisema.
Alisema kuwa hashangai kuona haya kwa sababu ndani ya wizara hiyo kuna watendaji aliowaita wababe na wasiopenda kuona Watanzania wengine wakishiriki katika shughuli za uchumi.
Hata hivyo, Mengi hakupatikana kujibu tuhuma hizo na hivyo juhudi za kumtafuta zinaendelea.
Dk. Slaa alivaa Bunge
Akizungumza na gazeti hili kuhusu waraka huo, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, alisema tatizo hilo limetokana na Bunge kugeuka kichaka cha kuficha uozo kwa kukataa pendekezo la kuundwa Kamati Teule kuchunguza tuhuma hizo.
“Tusingefika hapa kwa Bunge kugeuka kichaka cha kuficha uozo kama sio Spika wa Bunge, Anne Makinda kulinda mafisadi na kukataa kuunda kamati teule. Tatizo hili lilianzia kwa Spika aliyepita, Samuel Sitta wakati wa sakata la EPA.
“Sasa ili kujisafisha katika tuhuma hizi, serikali inapaswa kutoa taarifa bungeni kueleza ni lini uchunguzi huo utakamilika na taarifa hiyo itawasiliwashwa lini bungeni,” alisema.
Dk. Slaa aliwataka wananchi wasigeuzwe kuwa mazezeta katika suala hilo na badala yake wanapaswa kupiga kelele ili serikali iseme ukweli na kuchukua hatua.
Alisema kuwa itakuwa ni jambo la ajabu Serikali ya Uingereza ambayo imesaini mpango wa kuisaidia Tanzania euro milioni 71 (sawa na sh bilioni 177) katika miradi ya umeme, inafuatilia kwa umakini tuhuma hizo wakati Watanzania wako kimya.
“Kama serikali inataka kujisafisha katika ufisadi huu, basi Rais Jakaya Kikwete hana budi kufanya kama alivyofanya kwenye sakata la EPA kwa kutafuta mkaguzi kutoka nje ili ukweli ujulikane kwa sababu hapa ndani kwa sasa hakuna anayemwamini mwingine.
“Katika hili wala tusidanganyane, serikali ni mtuhumiwa. Hivyo kusema kwamba inatumia taasisi zake za CAG na Takukuru kujichunguza hapo tayari tumepigwa chenga la macho,” alisema.
Pia alimtaka Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kuacha propaganda kwenye majukwaa ya kisiasa za kudai kwamba UKAWA hawana huruma na Watanzania, badala yake amemtaka asaidie kuishauri Serikali ya Kikwete isipoteze fedha za Uingereza.
“Hizi fedha za Uingereza euro milioni 71 wanazotaka kuzizuia endapo tuhuma hizi za ufisadi zisipowekwa wazi, ni fedha nyingi sana, zingesaidia kwenye masuala mengi ya kijamii kama nishati, elimu, afya na maji. Sasa badala ya Kinana kuona umuhimu huo, anaendeleza propaganda dhidi ya UKAWA,” alisema.
chanzo: tanzania daima

Tuesday, May 13, 2014

ZIMBABWE KUCHUANA VIKALI NA STARS JIJINI DAR JUMAPILI


Mechi ya kwanza ya raundi ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika 2015 nchini Morocco kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Zimbabwe (Mighty Warriors) itafanyika Jumapili (Mei 18 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Awali mechi hiyo tulipanga ichezwe Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya kwa nia ya kuhakikisha mikoa yote ya Tanzania inapata fursa ya kuwa mwenyeji wa mechi za kimataifa.
Ili Uwanja wa Sokoine uweze kuchezwa mechi za kimataifa za mashindano, Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) lilituma Mkaguzi (inspector) wake kwenye uwanja huo Jumamosi (Mei 10 mwaka huu) ambapo imeamua kuwa marekebisho yanayofanyika hayatamalizika katika muda stahili, hivyo mchezo huo kutochezwa Sokoine.
Tunatoa mwito kwa wamiliki wote wa viwanja kuwasiliana na TFF ili Idara ya Ufundi iwaelekeze maboresho ya kufanya ili viwanja vingi iwezekanavyo viweze kukidhi viwango vinavyotakiwa na CAF na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Taifa Stars ambayo ilikuwa kambini mkoani Mbeya itarejea Dar es Salaam keshokutwa (Mei 14 mwaka huu) kujiandaa kwa mechi hiyo.

*MAKAMU WA RAIS DKT. BILAL ASHIRIKI KUAGA MWILI WA MAREHEMU FROSSIE CHIYAONGA ALIYEKUWA BALOZI WA MALAWI NCHINI.

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisaini kitabu cha maombolezo ya msiba wa aliyekuwa Balozi wa Malawi nchini Tanzania, Balozi Frossie Chiyaonga, wakati wa shughuli za kuaga mwili wa marehemu zilizofanyika kwenye Ukumbi wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam, leo Mei 12, 2014. Mwili huo unatarajia kusafirishwa kuelekea Malawi kwa maziko.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akitoa heshima za mwisho mbele ya Jeneza lenye mwili wa Marehemu, Frossie Chiyaonga, aliyekuwa Balozi wa Malawi nchini Tanzania, aliyefariki ghafla Ijumaa ya wiki iliyopita, wakati wa shughuli za kuaga mwili wa marehemu zilizofanyika kwenye Ukumbi wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam, leo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwafariji baadhi ya wanandugu na familia ya aliyekuwa Balozi wa Malawi nchini Tanzania, Balozi Frossie Chiyaonga, wakati wa shughuli za kuaga mwili wa marehemu zilizofanyika kwenye Ukumbi wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam, leo. 
 Sehemu ya waombolezaji waliojitokeza kwenye shughuli hiyo ya kuagwa mwili wa marehemu.
 Marehemu, Balozi Frossie Chiyaonga, enzi za uhai wake.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwa na baadhi ya viongozi wa Serikali ya Tanzania na Malawi wakati wa shughuli ya kuaga mwili wa marehemu Balozi wa Malawi nchini Tanzania.
 Sehemu ya waombolezaji waliojitokeza kwenye shughuli hiyo ya kuagwa mwili wa marehemu.
 Sehemu ya waombolezaji waliojitokeza kwenye shughuli hiyo ya kuagwa mwili wa marehemu.
 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, akitoa heshima za mwisho mbele ya Jeneza lenye mwili wa Marehemu, Frossie Chiyaonga, aliyekuwa Balozi wa Malawi nchini Tanzania, aliyefariki ghafla Ijumaa ya wiki iliyopita, wakati wa shughuli za kuaga mwili wa marehemu zilizofanyika kwenye Ukumbi wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam, leo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, akitoa salamu za rambirambi, wakati wa shughuli hiyo.

SIMBA NA YANGA KUKIMBIA MKUTANO WA RAIS WA TFF

Mkutano wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na wenyeviti wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kupata maoni yao juu ya changamoto zilizojitokeza katika ligi hiyo umefanyika juzi (Mei 11 mwaka huu).
Klabu za VPL zilizohudhuria mkutano huo ni Azam, Coastal Union, JKT Ruvu, Mbeya City, Mgambo Shooting, Mtibwa Sugar, Polisi Morogoro, Ndanda FC, Ruvu Shooting, Stand United na Tanzania Prisons.
Simba na Yanga hazikuhudhuria mkutano huo, na wala klabu hizo hazikutoa udhuru wowote wa kutokuwepo.
Maazimio ya mkutano huo ni kuwa kwa misimu mitatu ijayo kuanzia msimu wa 2014/2015 klabu zimekubaliana ziruhusiwe kusajili wachezaji watano wa kigeni. Kamati ya Utendaji ya TFF itatoa uamuzi wa mwisho juu ya suala hilo katika kikao chake kijacho.
Pia klabu hizo zimekubali timu zao za U20 kuanzia msimu ujao zicheze ligi ya mkondo mmoja. Hata hivyo, utekelezaji wa hilo utategemea na upatikanaji wa mdhamini wa ligi hiyo ambapo TFF inafanya jitihada za kumpata mdhamini huyo.

Vilevile Mwenyekiti wa Kamati ya Mpira wa Miguu wa Wanawake, Lina Kessy amezishauri klabu za VPL kuanzisha timu za wanawake, ambapo klabu hizo zimesema zitaufanyia kazi ushauri huo

MISS MANYARA KUPATIKANA MAY 31, 2014

Walimbwende 15 wa Wilaya za Babati, Simanjiro, Hanang’ Mbulu na Kiteto, wanatarajia kushiriki kinyanganyiro cha kumsaka mnyange wa mkoa huo kwa mwaka 2014, kitakachofanyika May 31 mjini Babati.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi, mratibu wa kampuni ya Mirerani Entertainment ya mjini Babati, Akon Clement, ambao ndiyo waandaaji wa mashindano hayo alisema maandalizi ya mtanange huo yanaendelea vizuri.

Clement alisema hivi sasa maandalizi ya kufanyika kwa Miss Manyara, yanaendelea vizuri kwani washiriki kutoka kwenye wilaya hizo wanaendelea na mazoezi kwa ajili ya kupatikana kwa wawakilishi wa mkoa huo.

“Tupo kwenye mazungumzo na baadhi ya waadhamini waliotuahidi kutuunga mkono kwenye Missi Manyara 2014, kwani mdhamini mkuu ni kampuni ya Tanzania Breweries kupitia kinywaji chake cha Redds,” alisema Clement.

Alitaja baadhi ya wadhamini wanaotarajia kudhamini Miss Manyara 2014 ni Manyara Compyuta, Chuo kikuu huria Manyara, Motel Silver, Trimas Saloon, Mireranitanzanite.blogspot.com, Shambani Solution Green belt na Fear Deal.

“Wadhamini wengine wanaotarajia kutudhamini kwenye shindano letu ni Motel Silver, Tina Classic, Pole pole Coach, San Abima Classic, Alno Technology, Ziggy Supermarket na Code Marketing,” alisema Clement.

Alitoa ombi kwa wazazi na walezi wa wilaya za mkoa huo, kuwapa ruhusa mabinti wao ili waweze kushiriki mashindano hayo, kwani mabinti wa jamii za wairaqw, wadatoga, wamasai, wambugwe na wafyomi wana uzuri wa asili.

“Pia tunaendelea na mazungumzo na baadhi ya wasanii wakubwa wa muziki kutoka jijini Dar es salaam na wasanii wengine chipukizi wa hapa hapa Babati na mkoa mzima wa Manyara kwa ujumla watashiriki,” alisema Clement.

Sunday, May 11, 2014

DPGP JANJA KURUDI NYUMBANI ARUSHA KIKAZI

KINDA wa muziki wa kizazi kipya nchini, Abdulaziz Abubakari ‘Dogo Janja’, amesema kwa sasa atakuwa anafanya kazi zake za muziki jijini Arusha kutokana na mashabiki wengi wa Dar es Salaam kutomthamini.
Dogo Janja, alisema jana kuwa kuanzia sasa akitaka kufanya kazi zake atasafiri kwenda Arusha maana amegundua kama ndiko anakokubalika zaidi kuliko mikoa mingine.
“Sio kwamba sitafanya kazi kabisa Dar es Salaam, nitafanya, lakini asilimia nyingi nitazifanyia nyumbani maana kule nathaminiwa sana, huku dharau nyingi na watu tunachukuliana poa tu, lakini mimi nataka kufanya kazi zangu nyumbani na sio Dar es Salaam tena.
“Unajua mwenye asili haachi asili na akiacha asili hana akili, nyumbani nakubalika sana hivyo sina budi kwenda kuwafurahisha mashabiki pamoja na familia yangu,” alisema msanii huyo mwenyeji wa Arusha.
Dogo Janja ni kati ya wasanii ambao wanatamba kupitia kazi zao kutokana na uwezo walionao pamoja na kukubalika katika jamii inayowazunguka

MVUA ZATARAJIWA KULETA NEEMA YA CHAKULA NCHI ZA MASHARIKI

SHARE THIS STORY
0
Share

Dodoma. Uzalishaji wa chakula Ukanda wa Nchi za Afrika Mashariki, unatarajiwa kuongezeka msimu wa kilimo wa 2014/2015, hivyo kupunguza soko la mazao ya chakula yanayozalishwa nchini.
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chizza alisema kama hali itakuwa hivyo, Serikali inawashauri wakulima na wafanyabiashara nchini kutafuta masoko ndani na nje ya nchi.
Akiwasilisha makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2014/2015 bungeni jana yanayofikia Sh318.7 bilioni, Chizza alisema wakulima na wafanyabiashara wataruhusiwa kuuza mazao nje ya nchi.
Chizza alisema taarifa za awali zinaonyesha kuwa, mvua zimenyesha vizuri katika nchi nyingine za Afrika Mashariki, hali inayoashiria kuwapo kwa mavuno mazuri katika nchi hizo.
Kwa muda mrefu, Serikali imekuwa ikizuia mazao ya chakula, hususan mahindi ambayo yana soko kubwa nchi za Kenya na Somalia kuuzwa nje.
“Hali ikiwa hivyo kwa maana ya kuongezeka mavuno nchi nyingine za Afrika Mashariki, Serikali inawashauri wakulima na wafanyabiashara kutafuta masoko nje ya nchi,” alisema Waziri Chizza na kuongeza:
“Napenda kusisitiza kwamba, Serikali haizuii uuzaji halali wa chakula cha ziada nje ya nchi kwa sababu tunatarajia kupata mavuno mengi msimu huu wa kilimo,” alisema waziri huyo katika bajeti yake.
Hata hivyo, Waziri Chizza alisema hali halisi ya chakula kitakachovunwa nchini msimu huu wa kilimo itajulikana baada ya kufanya tathmini Juni, 2014.
Alisema ingawa dalili ziko hivyo, lakini watakuwa na uhakika zaidi wa hali ya chakula kufikia katikati ya mwaka huu.
Wakati huohuo, Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA), imepanga kununua kutoka kwa wakulima tani 200,000 za nafaka, zikiwamo tani 190,000 za mahindi na tani 10,000 za mpunga kwa msimu wa kilimo wa 2014/2015.

Tumsaidie Lanjui aliyelazwa hospitali miaka 45


Lanjui aliyelazwa katika Wodi Namba Nne katika hospitali hiyo tangu Januari Mosi, 1971, awali alilazwa katika Hospitali ya Sekou Toure, Mwanza kuanzia mwaka 1969 mara baada ya kupata ajali.
Siku mbili zilizopita tulichapisha picha na habari katika ukurasa wa mbele wa gazeti hili kuhusu mgonjwa anayejulikana kwa jina la Abdi Lanjui ambaye amelazwa wodini katika Hospitali ya Singida kwa miaka 45 sasa, kutokana na ajali mbaya aliyopata mwaka 1971. Mgonjwa huyo mwenye miaka 75 alikuwa dereva wa Mamlaka ya Pamba na kupata ajali hiyo mkoani Mwanza baada ya lori alilokuwa akiendesha kuchomoka gurudumu la mbele na kupinduka.
Kusikiliza maelezo yake kuhusu mkasa huo uliompata kunatia uchungu mkubwa. Maelezo yake yanaleta hisia kwamba dunia siyo tu haina huruma, bali pia ni katili na ndiyo maana imemsahau na kumtosa kwa muda mrefu hivyo. Jambo la ajabu ni kuwa, ni mtulivu na mvumilivu kwa kiwango cha juu na bado anaishi kwa matumaini. Hana hasira wala kinyongo na dunia au jamii iliyomwacha katika upweke na maumivu makubwa kwa miaka yote hiyo 45.
Akizungumza huku akionekana kuwa katika mateso makubwa, anasema sababu ya kugeuza wodi kuwa makazi yake ya kudumu ni ajali iliyomsababishia kupooza kuanzia kiunoni hadi kwenye nyayo. Anasema kwa kuwa hanyanyuki kitandani, amepata vidonda kuanzia makalioni hadi miguuni na kuongeza kwamba anaishi maisha magumu mno.
Kutokana na hali hiyo, anaiomba Serikali na jamii kwa jumla imwonee huruma kwa kumsaidia chakula kwa kuwa hana ndugu wa kumpatia msaada wowote. Anasema, kwa miaka mingi uongozi wa hospitali ya Mkoa ulikuwa ukimhudumia kwa kumpa chakula, lakini baadaye huduma hiyo ilisitishwa, hivyo kumfanya awe ombaomba na maisha yake kuwa ya mlo mmoja kwa siku.
Kwa kuwa hawezi kunyanyuka kitandani na hana ndugu yeyote, amekuwa akiwaomba msaada manesi na watumishi wengine wa hapo hospitalini. Anawashukuru kwa kufanya hivyo bila kuchoka na kumwezesha angalao kupata mlo mmoja kwa siku, lakini pia anaomba msaada wa fedha ili aweze kwenda Hospitali ya KCMC au hospitali nyingine yoyote inayofaa ili apate huduma zaidi ya matibabu.
Mgonjwa huyo aliyelazwa katika Wodi Namba Nne katika hospitali hiyo tangu Januari Mosi, 1971, awali alilazwa katika Hospitali ya Sekou Toure, jijini Mwanza kuanzia mwaka 1969 mara baada ya kupata ajali. Akiwa katika hospitali hiyo mwishoni mwa mwaka 1970, hali yake ilibadilika na kuwa mbaya na ndipo alipomwomba mwajiri wake amrudishe nyumbani katika Kijiji cha Mhintiri katika Wilaya ya Ikungi, mkoani Singida mwaka 1971. Bahati mbaya ni kuwa, wakati anapata ajali na kulazwa hospitalini, wazazi wake na ndugu yake pekee walikuwa tayari wamefariki dunia.
Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Mussa Kamala anasema hivi sasa mgonjwa huyo anahudumiwa na hospitali kama watu wengine wenye ulemavu. Anasema uongozi wa hospitali hiyo uliwahi kumkabidhi kwa Idara ya Ustawi wa Jamii ili ifanye mpango wa kumrudisha nyumbani, lakini haikuwezekana.
Wakati huohuo, Ofisa Ustawi wa Jamii mkoani Singida, Zuhura Kalya anasema walishindwa kumrejesha nyumbani kwao, kwani walipofuatilia ilibainika kwamba hana ndugu na hakukuwa na mtu anayemfahamu kwa kuwa aliondoka kijijini hapo mwaka mmoja baada ya Uhuru.
Sisi hatuna la zaidi, isipokuwa kuwaomba wananchi kumsaidia mgonjwa huyo ambaye ameteseka vya kutosha kwa takribani nusu karne sasa. Ni matumaini yetu kwamba Serikali pia itachukua hatua stahiki haraka iwezekanavyo.

Thursday, May 8, 2014

JKT Oljoro yapania daraja la kwanza


TIMU ya JKT Oljoro imepania kukabili ushindani wa ligi Daraja la Kwanza kwa kuanza maandalizi mapema ikiwemo kuingia kambini na kujifua kwa mazoezi magumu ili waweze kurejea Ligi Kuu ya Vodacom.
JKT Oljoro imeshuka daraja msimu huu baada ya kudumu Ligi Kuu kwa takribani miaka minne.
Akizungumza, Mwenyekiti wa timu hiyo, Meja Sijaona Myala, alisema kuwa timu itaingia kambini Mei 25 na watajifua kisawasawa mfululizo, sambamba na mechi mbalimbali za kirafiki.
“Suala la kushuka daraja kutoka Ligi Kuu Bara hadi Ligi Daraja la Kwanza halitukatishi tamaa, bali ni kuangalia tu yapi yalisababisha ili turekebishe na changamoto ni zipi tuzitatue ili kuhakikisha tunapanda na kubaki juu, kwa sababu hata sisi tuko fiti kisoka na wapinzani wetu wanatukubali,” alisema.
Alisema kwa sasa wanachokifanya ni kuboresha timu, benchi la ufundi na kutafuta makocha wa makipa, sambamba na kuziba mapengo ya wachezaji waliomaliza mikataba, yote ikiwa ni mikakati ya kutimiza malengo waliyojiwekea ya kupanda na kubaki kung’ara kwenye soka.
Katika hatua nyingine, uongozi huo pia umejipanga kuboresha michezo mingine kama netiboli, ngumi, riadha, wavu n.k.

Riadha lawamani

KOCHA maarufu wa riadha, Samwel TupaKOCHA maarufu wa riadha, Samwel Tupa, ameulalamikia uongozi wa Riadha Tanzania (RT), kwa kutumia jina lake kama kocha aliyeondoka na wanariadha waliokwenda nchini New Zealand kwa maandalizi ya mashindano ya Jumuiya ya Madola yanayotarajia kufanyika Glasgow, Scotland, Julai mwaka huu.
Akizungumza kwa njia ya simu akiwa jijini Arusha, Tupa alisema hajui sababu iliyofanya uongozi huo kufanya hivyo, na kwamba mara ya mwisho aliwasiliana na Katibu Mkuu wa RT, Suleiman Nyambui, ambaye alimtaka wabaki ili waandae mashindano ya taifa yanayotarajiwa kufanyika Juni.
“Nyambui aliponiambia hivyo, nilimwambia mimi kama kocha siwezi nikabaki wakati wanariadha wangu wanakwenda, huko watafundishwa na nani, akadai watakuwa na kocha wa China, lakini mimi sikuafiki hilo na nikajua watakuwa wamebadilisha jina la kocha anayeenda, ila cha kushangaza naona kwenye vyombo vya habari kwamba nimeenda huko,” alisema.
Alisema mbali na yeye kuachwa, pia wamemuacha mwanariadha mwingine, Michael Damson, ambaye naye alikuwepo katika orodha ya kwenda na aliambiwa apeleke pasipoti, ila kaachwa bila taarifa yoyote.
“Baniani mbaya kiatu chake dawa na kidole kidogo kinashika mpini wa jembe, lakini hakiingii kwenye bakuli ya mboga, mimi siwezi kulalamika sana, lakini ninachohoji kwanini watangaze jina langu kwamba nimekwenda wakati nimeachwa bila kupewa taarifa yoyote?” alihoji kocha huyo wa kimataifa ambaye ni mkufunzi pekee Tanzania wa mchezo huo aliyethibitishwa na Shirikisho la Riadha la Kimataifa (IAAF).
Alisema kwa kuonyesha kwamba uongozi huo unakubali kazi zake, waliamua kuondoka na mwanariadha wake, Michael Gwandu bila kumpa taarifa na kuamua kuwasiliana na kocha msaidizi.
Alipotafutwa Rais wa RT, Anthony Mtaka, alitaka atafutwe makamu wake,  William Kallaghe, ambaye alidai ahusiki na benchi la ufundi, hivyo atafutwe Kaimu Katibu Mkuu wa RT, Ombeni Zavalla, ambaye pia alisema anayejua utaratibu wa safari hiyo ni Nyambui, yeye hajui lolote

MAPIGANI YA NGORONGORO YAUA 11

MAPIGANO ya kuwindana yanayotokana na mgogoro wa ardhi unaohusisha makabila ya Sonjo na Maasai katika tarafa za Sale na Loliondo, wilayani Ngorongoro, Arusha hadi sasa yameshaua wananchi 11.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Ngorongoro jana, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Eliasi Wawalali, alisema katika jitihada za kukomesha mapigano hayo, wamefanikiwa kukamata silaha tatu za kivita aina ya AK 47, SMG na SR ambazo zimesalimishwa na makundi hasimu katika mgogoro huo.
Wawalali alisema mgogoro huo ambao ni wa muda mrefu sasa unashindwa kumalizika kutokana na kutokuwepo kwa utashi kwa viongozi wa maeneo yenye mgogoro na pia kukiukwa baadhi ya maagano ya kale baina ya makabila hayo yaliyofanywa kwa kusimamiwa na hayati Edward Sokoine, aliyekuwa Waziri Mkuu katika kipindi hicho.
“Mgogoro huu na uhasama baina ya makabila haya hususani Wasonjo na koo ya Loita kwa upande wa Masai ulianza tangu mwaka 1975 na kuhusika kwa matumizi ya silaha nzito za kivita na hadi mimi nimeukuta mgogoro huo na tunajitahidi kuumaliza bila mafanikio,” alisema.
Alisema kwa kipindi cha miaka mitano tangu afike Ngorongoro, katika mgogoro huo wameshakamata silaha za kivita zaidi ya 80 ambazo zinaaminika hununuliwa kutoka nchi jirani kwa wananchi wa jamii hizo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ngorongoro, Eliasi Ngorisa, alisema wao kama madiwani ambao ni wawakilishi wa wananchi hawatakuwa na ujasiri wa kujisifu kuwa ni viongozi bora kama hawatajitoa kwa pamoja kuhakikisha mgogoro huo unamalizika.
chanzo,tanzania daima

Monday, May 5, 2014

Milioni 42 zakamilisha usajili wa straika Simba

Na Nicodemus Jonas
TIMU ya Simba imeonesha jeuri ya fedha na kuuhakikishia umma kuwa haitaki mzaha msimu ujao, baada ya kumwaga kitita cha Sh milioni 42 kumnyakua straika wa Mbeya City, Saady Kipanga.
Habari za kina kutoka kwa rafiki wa nyota huyo zinadai kuwa, Simba imempatia kitita cha Sh milioni 30 ‘keshi’, kama njia ya kumshawishi pamoja na kumuahidi mshahara wa Sh milioni moja kwa mwezi.
Mshahara huo unamfanya Kipanga kukunja kibindoni Sh milioni 12 kwa mwaka, hesabu inayoleta jumla ya Sh milioni 42 ukijumlisha fedha za ushawishi.
Mbali na hiyo, Simba tayari wanahaha kumtafutia nyumba kwani ni moja ya masharti aliyowahi kuwapa viongozi wa Simba kama wanahitaji huduma yake.
Lakini licha ya yote, bado nyota huyo wa zamani wa Rhino Rangers ya Tabora, hajasaini rasmi mkataba, ingawa wamemalizana kila kitu.
“Jamaa ameishamalizana na Simba kwa kila kitu. Amepewa milioni thelathini keshi na wamemwambia atakuwa akilipwa kiasi cha Sh milioni moja kwa mwezi.
“Hata jamaa mwenyewe anasema asingeweza kuacha bahati hiyo. Zaidi ya yote, kwa sasa Simba wanahaha kumtafutia nyumba ya kuishi maana aliwahi kuwambia kuwa lazima ahakikishiwe malazi,” alisema mtoa taarifa wetu.
Simba imekuwa kwenye rada za kumnasa Kipanga tangu kumalizika kwa ligi kuu msimu uliokwisha ambapo alikodiwa hadi ndege kutoka Mbeya kuja Dar kwa ajili ya kuonana na Simba kuzungumzia suala la usajili wake.

watoto wasifanywe vitega uchumi

WIZARA ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, imewataka wazazi kuacha tabia ya kuwageuza watoto walio chini ya umri wa miaka 18 kuwa vitega uchumi vyao.
Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salam juzi na Waziri wa wizara hiyo, Sophia Simba alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Alisema hivi sasa wazazi wengi wamekuwa wakiwafanya watoto wao vitega uchumi kwa kuwatafutia kazi za ndani wakiwa chini ya miaka 18, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Waziri Simba alisema ni kosa kubwa kwa mzazi kumpeleka mtoto wake mwenye miaka chini ya 18 kwenda kufanya kazi za ndani wakati anatakiwa kupata elimu.
“Watoto ni taifa la kesho kwa hiyo tunapaswa kuwajengea msingi bora, ili wasije kuwa tegemezi hapo baadaye. Tuhakikishe wanapata elimu badala ya kuwageuza vitega uchumi kwa kuwatafutia kazi za ndani,” alisema.
Katika hatua nyingine, Waziri Simba aliwataka Watanzania kuacha tabia ya kuwanyanyasa wafanyakazi wa ndani kwa kuwatumikisha zaidi ya saa 12 na kuwalipa mshahara mdogo kwa kisingizio cha kula na kulala nyumbani kwa mwajiri.
Chanzo: Tanzania Daima

UKAWA waitesa CCM


MIKUTANO miwili ya hadhara ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), iliyofanyika Unguja na Pemba visiwani Zanzibar, na ujumbe uliotolewa na viongozi wa umoja huo, umeitia kiwewe Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho kimepanga kujibu mapigo.
Mbali ya kutaka kujibu mapigo, CCM pia inahaha kutumia vyombo vya dola na ofisi ya msajili kuusambaratisha umoja huo unaoonekana kuungwa mkono na wananchi wengi.
UKAWA inaundwa na vyama vinavyounga mkono rasimu ya katiba ya serikali tatu ambavyo ni Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), NCCR- Mageuzi, UDP na vyama vingine ambavyo wajumbe wake walisusia mjadala wa Bunge Maalumu la Katiba baada ya kutoridhishwa na namna Bunge hilo lilivyokuwa linaendeshwa.
Ujumbe unaoelezwa kuivuruga CCM kwenye mikutano hiyo ya UKAWA visiwani Pemba na Unguja, ni ule unaoeleza mkakati wa umoja huo kutaka kusimamisha mgombea mmoja wa urais na katika ngazi nyingine za uwakilishi.
Duru za siasa zinasema kuwa tayari viongozi wa juu wa CCM wamepanga kuanza kufanya mikutano ya hadhara kujibu mapigo ya UKAWA, na pia kueleza umuhimu wa kuwa na serikali mbili na ubaya wa serikali tatu.
Habari zinasema kuwa CCM leo imepanga na tayari imeomba kibali kufanya mkutano wa hadhara visiwani Zanzibar, katika uwanja ule ule waliotumia UKAWA wa  Kiembesamaki.
Mkutano huo ambao unaelezwa kwamba utawashirikisha baadhi ya viongozi wa CCM kutoka Tanzania Bara, pamoja na mambo mengine utajibu kauli za UKAWA, hasa kuhusu serikali tatu, lakini pia kuelezea mkakati wao wa kutaka kuungana 2015.
“CCM leo wana mkutano hapa hapa Kiembesamaki walipofanyia UKAWA. Wamepanga kutoa ufafanuzi wa hoja za UKAWA ambazo kama zikiachwa, zinaweza kuleta athari kubwa kwa taifa,” alisema mmoja wa viongozi wa CCM Zanzibar.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Nape Nnauye, alisema kuwa wamelazimika kwenda kujibu mapigo kwa madai kuwa UKAWA wameamua kupotosha umma na hawana nia njema na taifa.
Alisema UKAWA wamevunja sheria ya mabadiliko ya katiba ambayo inakataza kwenda kwa wananchi sasa wakati hakuna jambo lililokwishaamuliwa bungeni.
Duru za siasa toka ndani ya chama hicho tawala, zinasema kuwa moja ya njia hizo ni kutumia ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kuhoji uhalali wa UKAWA kubadilisha hoja ya mchakato wa katiba mpya na kuzungumzia harakati za kutaka kusimamisha mgombea mmoja wa urais.
Alisisitiza kuwa watazunguka nchi nzima katika kila eneo ambalo UKAWA watapita ili kutoa ufafanuzi wa ajenda zao ambazo alidai zina nia ya kusaka madaraka.
Wakati CCM wakijipanga kwenda kujibu mapigo, upande mwingine chama hicho kinadaiwa kutumia vyombo vya dola na ofisi ya msajili kutaka kuusambaratisha umoja huo na kuzima mikutano yao Tanzania Bara.
Tayari Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, juzi alikaririwa na gazeti moja akionyesha kukerwa na jinsi UKAWA wanavyofanya mikutano ya hadhara kwa kutumia jina la umoja huo, huku wakijua fika kwamba sio chama cha siasa kilicho na usajili.
Jaji Mutungi katika taarifa hiyo, alisema mikutano ya hadhara iliyoombewa kibali Zanzibar ni ya CUF, lakini alieleza kushangazwa kwake, kwamba katika mikutano hiyo wazungumzaji walikuwa wakijitambulisha kwa jina la UKAWA na kusalimiana kwa jina la umoja huo.
Pia alihoji sababu za umoja huo kutumia UKAWA kisiasa kwa kutangaza kusimamisha mgombea mmoja wa urais mwakani badala ya kuzungumzia mchakato wa katiba na sababu zilizowatoa nje ya Bunge.
Habari zaidi zinasema kuwa kuna mpango wa vyombo vya dola kutumia kauli ya msajili kuzuia mikutano ya UKAWA Tanzania Bara kwa madai kuwa umoja huo umevunja sheria.
Habari za kiintelijensia zinasema kuwa polisi watazuia mikutano ya UKAWA kama itaombewa kibali cha umoja huo, lakini kama kibali hicho kitaombwa kupitia moja ya vyama vinavyounda UKAWA, jeshi hilo litalazimika kujiridhisha mkutano huo utakuwa wa chama husika na si vinginevyo.
Akizungumza na maelfu ya wananchi visiwani Pemba, Mwenyekiti wa UKAWA, Freeman Mbowe, alielezea nia ya umoja huo kutaka kusimamisha mgombea mmoja wa urais na katika nafasi nyingine za uwakilishi.
Katika mkutano huo wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Gombani Kongwe mjini Chakechake Pemba, juzi, Mbowe alisema UKAWA umeanzishwa kwa ajili ya mchakato wa katiba mpya, lakini baada ya kuona faida yake, sasa wanakusudia kusimamisha mgombea mmoja kwenye uchaguzi mkuu mwakani.
“Je, wananchi wa Pemba mko tayari kuwa na mgombea mmoja kuanzia uwakilishi hadi rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?” alihoji Mbowe na kuitikiwa kwa kuungwa mkono na maelfu ya wananchi waliofurika kwenye uwanja huo.
Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), alisema nguvu ya pamoja na mshikamano walioukosa zamani, ilisababisha CCM kuwa  jeuri, hivyo hawawezi kurudia kosa hilo.
Mbowe ambaye pia ni mbunge wa Hai, alisema wapinzani wanapaswa kujilaumu wenyewe kwa kujitenga kwani walikosa nguvu ya pamoja katika chaguzi zilizopita.