.

.
Friday, January 30, 2015

12:39 AM
na Bertha Ismail  - Arusha
Chama cha mchezo wa baiskeli Taifa (CHABATA) kinatarajia kupeleka wachezaji 10 nchini Afrika kusini kuwakilisha nchi kwenye mashindano ya kusaka bingwa wa bara la Afrika yanayotarajiwa kuanza kutimua vumbi February tisa hadi 14 mwaka huu huku wakikabiliwa na changamoto lukuki.
Akizungumza na gazeti hili mwenyekiti wa Chama cha mchezo huo nchini Godfrey Jax Mhagama amesema kuwa mashindano hayo yanayoshirikisha nchi zaidi ya 30 za bara la Afrika yanafanyika kila mwaka ambapo kwa Tanzania wachezaji hawa watakuwa wanaifanya nchi kuwa mara ya tano kushiriki.
Mhagama alisema kuwa wachezaji hao wanatarajia kuondoka nchini February sita mwaka huu kulingana na upatikanaji wa fedha wa dola 12,000 (milioni 20) ambapo amesema kuwa kwa sasa chama hicho kina nusu ya fedha hizo.
“Kwa mwaka huu tunatarajia kupeleka wachezaji 10 miongni mwao wasichana wakiwa ni wawili na wanaume nane, lakini hilo litafanikiwa endapo wadhamini watajitokeza kutusaidia kupunguza gharama kwani hadi sasa tuna dola 6000 na bajeti yetu kwa hao watu 10 ni dola 12,000 hivyo kama tukikosa itabidi tuangalie namna ya kupunguza idadi” alisema mhagama.
“Kwa sasa nitumie fursa hii ya chombo chenu kinachosomwa na watu wengi nchini kuliko vyombo vyovyote kuwaomba wadau wajitokeze kusaidia timu hii ikafanye vema huko Afrika kusini kwani endapo tukifanikiwa kupeleka wachezaji wengi zaidi ndio tutakuwa katika nafasi nzuri ya kushinda lakini watu wachache huwa rahisi kuachwa”
Miongoni mwa wachezaji hao wane wanaotoka mkoani Arusha akiwemo msichana mmoja imebainika kuwa bado hawajaingia kambini hadi leo ambapo kila mmoja anafanya mazoezi mkoani kwake huku vifaa vyao ikiwemo baiskeli kutokuwa na uimara wa mashindano.
Akijibu swala hilo Mhagama alisema kuwa ni kweli hadi leo wachezaji hawajaingia kambini kufanya mazoezi kutokana na kutokuwa na fedha za kugharamia mahitaji yao hali iliyosababishwa na ukosefu wa ufadhili kwa kupatiwa ahadi na makampuni mbalimbali zisizotekelezeka.
“Ni kweli kama ulivyowaona hawajaingia kambini kutokana na kukosa fedha za kugharamia kambi, huku wadau wakituahidi tu bila kutekeleza lakini naomba niwahakikishie wadau kuwa hilo pamoja na kuwa kama sehem ya madhara kwetu lakini wasiwe na wasiwasi kwani tutajitahidi kuwa katika nafasi nzuri”
mwisho..................

0 comments:

Post a Comment