Rais Kikwete aomba Ujerumani kusaidia Tanzania katika kukuza uchumi
Rais wa Ujerumani, Joachim Gauck (kushoto) na mwenyeji wake, Rais Jakaya Kikwete wakiwasalimia watoto na wananchi baada ya kuwasili Ikulu, Dar es Salaam jana kwa ziara ya siku tano. (Na Mpigapicha Wetu).
RAIS Jakaya Kikwete na mgeni wake, Rais wa Ujerumani, Joachim Gauck wamekubaliana katika kukuza ushirikiano wa kiuchumi, huku Rais Kikwete akiitaka Serikali ya Ujerumani kuenedelea kuisaidia Tanzania katika kukuza uchumi kwa kutoa misaada ya maendeleo na kuwekeza zaidi.
Aidha, Rais Gauck ameipongeza Tanzania kutokana na juhudi za kusaidia kuleta amani katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Sudan Kusini. Akizungumza jana akiwa na mgeni wake, Rais Kikwete alisema Ujerumani imekuwa na mchango mkubwa kwa Tanzania, lakini kuna haja ya kuongeza misaada hiyo.
Alisema pamoja na kuwapo ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Ujerumani hususani kuwa na uhusiano mzuri kisiasa, lakini pia kuna haja kuimarisha uhusiano wa kiuchumi kwa lengo la kukuza uchumi. Kikwete alisema katika kuimarisha uchumi, Ujerumani inaweza kuisaidia Tanzania kwa njia mbili, ikiwa ni misaada ya maendeleo na uwekezaji katika sekta mbalimbali.
Alisema kwa sasa Ujerumani ina miradi 151 ya uwekezaji yenye thamani ya Euro milioni 300 (Sh bilioni 630) na kuwa wanaweza kuwekeza zaidi ya hapo hadi kufikia zaidi ya Euro bilioni moja (Sh trilioni 2.1) hasa kutokana na Tanzania kugundua nishati ya gesi asilia.
“Ujerumani imekuwa ikiisaidia Tanzania. Tanzania iko kama ilivyo leo kwa sababu ya misaada kutoka Ujerumani. Katika mkutano wetu wa faragha tumejadili na kuweka wazi dhamira ya kushirikiana. Uhusiano wetu wa kisiasa uko vizuri na kwa sasa tuelekeze nguvu katika kuimarisha uhusiano wa kiuchumi.”
Kikwete aliongeza: “Nina furaha kwa sababu umekuja na ujumbe wa wafanyabiashara, hasa kutokana na kuwa tumegundua gesi, maeneo ambayo mnaweza kuwekeza pia.” Kwa upande wake, Gauck aliipongeza Tanzania kwa kudumisha amani katika ukanda huu na kusema:
“Tunaheshimu kile ambacho Tanzania imekifanya katika kuleta amani na usalama katika ukanda huu, kupambana na maharamia na kuleta amani katika nchi za DR Congo na Sudan Kusini, huo ukiwa ni mfano wa utawala wa sheria.”
Akizungumzia ushirikiano wa kiuchumi, Rais Gauck alisema kuna fursa ya kuboresha uhusiano wa nchi hizo mbili na kuwa amekuja na ujumbe wa wafanyabiashara ili waweze kuona maeneo ya uwekezaji. Gauck pia aliipongeza Tanzania kwa kupiga hatua katika kukuza uchumi ambao umekuwa kwa asilimia saba.
“Mafanikio haya yameifanya Tanzania kuwa nchi ya mfano kwa Afrika.” “Mmeonesha kuwa mko tayari kwenda mbali zaidi, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kunakuwa na utawala bora kama kupambana na rushwa na tutakuwa nayi,” alisema.
Aidha, akijibu swali kuhusu kufungiwa kwa gazeti la The East Afrika, Kikwete alisema gazeti hilo lilikuwa likifanya shughuli zake bila kufanya usajili na kwa sasa wamiliki wa gazeti hilo wamefanya taratibu za kuomba na mamlaka husika zinashughulikia hilo.
“Serikali haizuii uhuru wa vyombo vya habari hapa nchini, na hii ndio maana tumekuwa na orodha ndefu ya magazeti yanayomilikiwa na watu binafsi huku serikali ikiwa na magazeti mawili tu,” alisema.
Kuhusu swali la polisi kuwapiga viongozi wa vyama vya upinzani wanapofanya maandamano, Kikwete alisema nchi ina sheria na kanuni ambazo vyama vya siasa vinatakiwa kufanya kabla ya kuandamana.
Kuhusu kudumisha amani hapa nchini na mikakati ya kupambana na mashambulizi ya al-shabab, Kikwete alisema Tanzania imeweza kudumisha amani pamoja na kuwapo watu wenye dini tofauti kunatokana kuwa na kamati ya amani inayoundwa na viongozi wa dini ambao wanakutana kuzungumzia tofauti zao.
Kuhusu ugaidi, Kikwete alisema: “Siwezi kusema kuwa Tanzania itaendelea kuwa salama na haitakumbwa na mashambulizi ya kigaidi kwa asilimia 100, kinachofanyika ni kuimarishwa kwa ulinzi vya ndani pamoja na kushirikana katika kubadilishana taarifa za kiintelejensia na mataifa mengine.
Rais Gauck aliyewasili nchini juzi kwa ziara ya siku tano, jana alifanya mazungumzo ya faragha na mwenyeji wake na kisha kuzungumza na wadau kutoka katika asasi za kiraia.
Leo Rais Gauck atakuwa Zanzibar, ambako atakutanana na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein na pia kukutana na viongozi wa madhehebu.
0 comments:
Post a Comment