.

.
Friday, August 2, 2013

4:18 AM


MKURUGENZI wa Mashitaka (DPP), Eliezer Feleshi, amesema haoni mantiki yoyote au uhalali wa Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), kumshitaki Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Alisema hayo janai wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari, baada ya kufungwa kwa mkutano wa siku tatu wa mawakili wa Serikali wafawidhi, wakuu wa upelelezi wa mikoa na vikosi vingine vya Polisi Alisema kauli aliyotoa Pinda bungeni, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu kuhusu Polisi kutumia nguvu kwa wananchi, ililenga wanaokaidi kukamatwa na kufikishwa mbele ya sheria na si kupiga na kuua kama ilivyotafsiriwa na wengi.
 
“Sijapata taarifa kwa maandishi juu ya azma ya kumshitaki Waziri Mkuu, lakini Pinda hajavunja sheria kwa kauli yake aliyotoa,” alisema.

Alisema kwa jinsi alivyosikia maelezo ya Waziri Mkuu bungeni, kama LHRC wanamshitaki kwa jinai Waziri Mkuu, haoni uhalali wa mashitaka hayo. 

Usahihi wa Pinda Alisema Waziri Mkuu alieleza hatua zinazochukuliwa dhidi ya mvunja sheria, na kufafanua kuwa Mtanzania yeyote ana haki kwa mujibu wa sheria, lakini pia ana wajibu, ndiyo maana vipo vyombo na kila chombo kimepewa mamlaka na wajibu wa kutekeleza.

Alifafanua, kwamba kilichoongelewa ni dhana ya mkusanyiko ambayo ni haki kwa mujibu wa Katiba, ikiwemo uhuru wa kukutana, kutoa mawazo na kufanya mawasiliano.

Hata hivyo, alikumbusha kuwa Sheria ya Jeshi la Polisi, inasema ili mkusanyiko ufanyike, lazima taarifa itolewe kwa kiongozi wa Polisi wa eneo husika.

 
Sheria hiyo inasema, kama mkusanyiko una nia ya kutenda kosa na ikafanyika hivyo, kuna chombo kilichopewa dhamana ya kuhakikisha mkusanyiko haramu unatawanyika na sheria hiyo inaruhusu Polisi kutawanya mkusanyiko haramu.

“Unatarajia nini kama kuna watu wanafanya fujo na polisi wana mamlaka ya kuwakamata waliofanya fujo?” Alihoji Feleshi na kuongeza kuwa dhana ya matumizi ya nguvu ni ya kisheria pia.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, akizungumza kwa simu na gazeti hili, alisema utaratibu wa Polisi kulazimika kutumia nguvu upo. Aliutaja utaratibu huo kwamba unatumika hasa katika mikusanyiko isiyotakiwa, ambapo Polisi hulazimika kutoa tangazo la angalizo mara kadhaa kutaka watu watawanyike.


“Tangazo linapotolewa, Polisi kwa kutumia kipaza sauti husema, tawanyikeni, tawanyikeni na kusisitiza hivyo mara kadhaa, hapo wanaopaswa kutawanyika wakikaidi, nguvu hutumika ingawa inaweza isiwe ya kupiga risasi, pengine virungu, yote hiyo si kupiga?


“Risasi ni kitu cha mwisho, labda uwe unashambuliwa wewe (polisi), hata ikiwa hivyo, ukipiga risasi kuna maeneo ya kupiga, si kichwani, polisi wana mafunzo ya kupiga maeneo ya miguuni, hivyo kutumia nguvu kwa polisi kupo,” alisema Jaji Werema.

0 comments:

Post a Comment