.

.
Sunday, August 25, 2013

3:57 AM

MABINGWA Yanga, jana walianza safari ya kutetea taji lao kwa kishindo baada ya kuionea Ashanti United kwa ‘kuisigina’ na kipigo cha mabao 5-1, huku mahasimu wao, Simba wakipelekwa puta na vijana wapya Ligi Kuu, Rhino Rangers na kuponea chupuchupu kwa kulazimisha sare ya kufungana mabao 2-2 mjini Tabora. 


Katika mechi ya Yanga iliyopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Vijana wa Jangwani walitawala mchezo tangu mwanzo mpaka mwisho, huku Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora Rangers wakilazimika kukomboa mabao baada ya kutangulia kufungwa mara mbili.
 
Iliwachukua Yanga dakika 10 tu tangu kuanza mchezo kufunga bao la kwanza lililowekwa kimiani na Jerryson Tegete aliyemalizia kwenye kamba pasi nzuri ya Simon Msuva na kumtungua kipa wa Ashanti, Ibrahim Abdallah.
 
Hussen Sued kuzuiwa na Tegete kabla ya kuvuka mstari huku tayari Kipa Ally Mustapha akiwa ameshapitwa na mpira.
 
Ashanti walikuwa na nafasi nyingine ya kusawazisha dakika ya 24 kufuatia shuti kali la Sued kumlazimisha Mustapha kufanya kazi ya ziada kulipangua na kuwa kona.
 
Dakika tatu baada ya kuanza kipindi cha pili, Msuva aliipeleka Yanga mbele na kufanya matokeo kuwa 2-0, kabla ya Tegete kufunga bao la tatu dakika ya 57, na kisha Haruna Niyonzima kufanya matokeo kuwa 4-0 dakika ya 73.
 
Ashanti walifunga bao la kufutia machozi dakika ya 90 kupitia kwa Shaaban Juma, kabla ya Nizar Khalfan kufunga nao la tano.
Akijitetea na kipigo hicho, Kocha wa Ashanti Hassan Banyai alisema kikosi chake kinahitaji muda zaidi.
 
Tabora:
Mjini Tabora, Simba wakishangiliwa na umati mkubwa, walibanwa vilivyo na wageni wa Ligi Kuu, Rhino Rangers na kulazimisha sare ya mabao 2-2 kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.
 
Katika mechi hiyo iliyochelewa kuanza kufuatia utata wa vibali vya wachezaji, Joseph Owino, Abel Dhaira na kukosekana kwa leseni ya Betram Mwombeki, timu zote zilishambuliana kwa zamu.
 
Iliwachukua Msimbazi dakika 8 tangu kupulizwa filimbi ya kuanza mchezo kufunga la kwanza kupitia Jonas Mkude aliyeunganisha kwenye kamba kwa kichwa kona maridadi ya Issa ‘Baba Ubaya’ Rashid.
 
Wenyeji Rangers walisawazisha bao hilo dakika ya 35 kupitia Iman Noel.
 
aliyepiga mpira wa adhabu ndogo na kwenda moja kwa moja wavuni, kabla ya dakika moja baadaye Simba kuongeza bao la pili likifungwa na Mkude kwa kiki ya penalti.
 
Penalti hiyo ilitokana na kiungo Amri Kiemba kuchezewa faulo ndani ya eneo la hatari na beki wa Rangers, Daniel Manyenya, aliyeishia pia kuonyesha kadi ya njano kwa kosa hilo.
 
Sekunde chache kabla ya mapumziko, Rangers walifunga bao la kusawazisha, ambalo lilikataliwa na Mwamuzi Amos Paul kutoka Mara kwa madai kuwa kabla ya bao hilo, kipa wa Simba alifanyiwa madhambi.
 
Kipa wa Rangers, Abdul Mtumwa alifanya kazi kubwa kuokoa mpira wa kichwa kutoka kwa Joseph Owino kufuatia kona iliyochongwa na Baba Ubaya dakika ya 20.
 
Kipindi cha pili, Rangers walibadilika na kufanya mashambulizi makali na kufunga bao la kusawazisha dakika ya 70 kupitia Stanslaus Mwaktos aliyefunga kwa kiki ya adhabu ndogo iliyomponyoka kipa wa Simba.
MWANANCHI

0 comments:

Post a Comment