.

.
Sunday, August 25, 2013


NIMEWAHI kuandika hivi karibuni kuhusu uzembe uliopo serikalini katika udhibiti dawa za kulevya. Nilieleza kwa kina jinsi nchi yetu ilivyotumbukia kwenye lindi la uchafu wa dawa hizo.
Leo nchi yetu imekuwa uchochoro wa wauzaunga, vijana wamejiajiri kwenye biashara haramu ya kusafir
isha dawa hizo! Imefika mahali sasa Mtanzania akisafiri nje ya nchi anakaguliwa mara mbili tatu, yaani hatuaminiki tena. Aibu gani hii ?.
Vyombo vya dola vimebaki na visingizio vilevile kila siku, eti hii ni biashara ya kimataifa. Wenye biashara ni vigogo, mara wana fedha nyingi na visingizio kibao.
Visingizio hivyo hivyo utavisikia kwenye ujangili wa meno ya tembo, eti ni vigogo wenye fedha nyingi. Utamsikia waziri mzima anajipiga kifua bila hata aibu, eti ninayo majina yao, lakini hata siku moja hayataji.
Lakini wiki iliyopita, Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe aliufurahisha umma wa Watanzania kwa ujasiri wake wa kutaja majina ya wafanyakazi saba wa serikali aliodai kuwa walihusika katika kupitisha mabegi tisa ya dawa za kulevya yenye uzito wa kilo 180 katika Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, kwa kuwa siku hiyo walikuwa zamu, na hivyo walitakiwa kubaini mzigo huo.
Huu ndiyo ujasiri unaotakiwa. 

Kama kweli tumeamua kupambana na dawa hizo, basi kila kiongozi aige mfano wa Dk Mwakyembe.
Hata hivyo, kilichofanywa na Dk Mwakyembe ni kama tone tu ndani ya maji ya bahari. Ilitakiwa Serikali nzima ionyeshe msimamo kama huo.
Mwakyembe yeye amegusia upitishaji wa dawa kwenye viwanja vya ndege, lakini dawa hizo pia hupitia baharini na nchi kavu. Bado hatujawa na nia ya dhati ya kupambana nazo.
Ni kweli kwamba biashara hii ni ya mitandao ya kimataifa, lakini walau tunaweza kupambana ili kuiepusha nchi yetu na balaa au aibu hii.
Mfano aliouonyesha Dk Mwakyembe siyo kwenye dawa tu za kulevya tu, bali hata katika utendaji wake. Tumeshuhudia mambo kadhaa ya mafanikio katika wizara yake, kwa mfano kuongezeka kwa mapato bandarini, unazishwaji wa treni ya abiria na mengineyo mengi.
Uthubutu huu ndiyo unatakiwa kwa mawaziri wote katika Serikali hii. Maendeleo yanataka uthubutu wa hali ya juu. Tatizo mawaziri wengi hawana uthubutu huo, wengine wanatafuta masilahi yao, wengine ni uzembe tu umetawala.
Hata hivyo, inatia moyo kuona mawaziri wanaothubutu kama Dk Mwakyembe. Tunahitaji mawaziri na watendaji wote wa serikali wenye ujasiri kama huo.
chanzo, jumamtanda

0 comments:

Post a Comment