.

.
Friday, May 29, 2015

na Mwandishi wetu - Arusha
Uongozi wa taasisi ya BIMO Media ya Mkoani Arusha. Umeelezea kuunga mkono hatua ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupendekeza kuwepo siku maalumu ya kuadhimisha umoja na amani kitaifa.
BIMO pia imeelezea kufurahishwa na hatua ya CCM kutaka kuanzisha matamasha maalumu ya umoja na Amani yanayolenga kudumisha mshikamano nchini bila kujali itikadi za wananchi.
Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Bertha Ismail Mollel amesema kuwa BIMO Media ilikuwa ya kwanza kuandaa matamasha haya ya Amani na kwamba tukio la kwanza lilifanyika jijini Arusha mnamo mwezi Desemba mwaka jana na kwamba kwa mwaka huu wako tayari kabisa kuungana na Chama Tawala katika kuhakikisha kuwa matamasha ya Amani yanafanikiwa kwa kiwango kikubwa hapo mwezi julai.

"Swala la amani ni jukumu la kila mtu hivyo sisi tulianza tukiwa na lengo kubwa la kuwakutanisha vijana pamoja na kuwaeleza umuhimu wa amani na wasikubali kugawanywa kwa misingi ya dini, ukabila wala siasa pia wasikubali kutumika kama magaidi katika nchi yao bali  wajenge uzalendo wa hali ya juu" alisema Bertha.

Wakati huhuo huo Msajili wa vyama vya siasa nchini, Jaji Francis Mutungi ameelezea kufurahishwa na matamasha ya Amani na hasa pale yanapowalenga vijana ambao ndio nguvu kuu ya taifa na ndio hasa wenye jukumu la kulinda Amani na kudumisha umoja nchini.
Hata hivyo Jaji Mutungi amebainisha kuwa, ni vizuri pia wanafunzi wa vyuo na shule zote nchini washirikishwe kikamilifu bila kusahasu viongozi wa dini na taasisi zake kwani huko ndiko wananchi huwakilishwa kwa wingi.
Hivi karibuni uongozi wa juu wa CCM ulipendekeza kuwepo na siku maalum kitaifa kwa ajili ya kuadhimisha umoja na Amani ambapo matuniko kadhaa yakiwemo ya michezo, matamasha ya muziki, sala maalum na mengineyo yangekuwa yanafanyika na kuwaleta pamoja wananchi katika maeneo yote nchini kujumuika bila kujali tofauti zao za kiitikadi na kisiasa.
Matamasha hayo yameelezewa kuwa ni hatua muhimu ya kuwaunganisha tena watanzania hususan katika kipindi hiki cha uchaguzi ambapo watu wengi hujikuta wamegawanyika kutokana na kampeni za wanasiasa wanaowania nafasi na nyadhifa kadhaa nchini huku wakitumia vijana kutishia uvunjifu wa amani.

mwisho........

0 comments:

Post a Comment