.

.
Friday, May 29, 2015

3:24 AM
Timu ya Arusha mpira wa kikapu (wa kwanza kushoto ndie katibu wa mchezo huo Mkoa)

Bertha Ismail - Arusha
Timu ya mpira wa kikapu ya Jiji la Arusha ni miongoni mwa timu za majiji za Nchi za Afrika yanayoshiriki mashindano ya mpira wa kikapu kila mwaka, lakini kwa mwaka huu Ukata unaoindama timu hiyo imeshindwa kabisa kuwakilisha katika mashindano hayo ya mwaka huu yaliyoanza kutimua vumbi katika uwanja wa ndani wa Taifa jijini Dar es salaam jana.
Akizungumza kwa uchungu mkubwa, katibu wa Mpira wa kikapu mkoa wa Arusha Bariki Kilimba aliliambia gazeti hili kuwa wameshindwa kwenda kushiriki michuano hiyo kuwakilisha jiji la Arusha kutokana na kukosa kiasi kidogo cha pesa kilichopelea huku wadau wakishindwa kuwasaidia.
“Kiukweli imeniuma sana kushindwa kushiriki mashindano haya makubwa Afrika kwa sababu tu ya kukosa kiasi kidogo cha pesa kwani bajeti yetu ilikuwa ni milioni 1.6 hivyo tulitembea kwa wadau ikiwemo jiji la Arusha na kwa mkuu wa mkoa lakini tuliambulia patupu, ila kwa sababu tuna moyo tuliamua kuchangishana kwa wale wenye uwezo ambapo tulipata laki 8 na wachezaji wengine ni wanafunzi hivyo walishindwa kuchanga na fedha ikapelea”
“kUfuatia hali hiyo tulianza kutafuta marafiki wa karibu yetu lakini wengi hawakuwa na uwezo wa kutusaidia hivyo tukaamua tu kutulia na nafasi yetu bado ipo hewani hivyo tunaomba kwa watu wenye uwezo jamani watusaidie bado tuna nafasi ya kuwakilisha jiji letu kwenye nchi  za Afrika au kampuni na taasisi zitusaidie nasi tutawatangaza kwenye nchi hizi shiriki” alisema Kilimba.
Timu hiyo ya wanaume yenye jumla ya wachezaji 10 ilianza mazoezi makubwa tangu mwezi uliopita  huku wakifanya mashindano ya mara kwa mara za kirafiki kujifua kwa ajili ya mashindano hayo ya majiji wakiwa na matumaini makubwa ya kurudi na ushindi lakini ukata umekatisha ndoto zao.
Aidha michuano ya mpira wa kikapu kutoka majiji ya Afrika yameanza jiji Dar huku timu kutoka sehemu mbali mbali zikishiriki ikiwemo majiji ya Tanga, Mwanza, Kampala, Kigali Entebe, Nairobi Mombasa, Mogadishu, Hargeisa (Somalia), Bujumbura, Garowe, Diaspora, Bentieu, Malakal,Juba, Cairo n.k.
mwisho............

0 comments:

Post a Comment