.

.
Wednesday, May 6, 2015

Bertha Ismail - Arusha

Wakati matani ya hapa na pale yakiendelea baina ya mashabiki wa timu kongwe nchini Simba na Yanga, mashabiki hao  Arusha wameamua kufuta ubishi wa nani Mb’abe wa kandanda safi, ambapo Simba wamedhiirisha umwamba wao baada ya kuwabugiza Yanga mabao 6-3.

Mchezo huo wa kirafiki uliowakutanisha mashabiki wa simba na yanga Arusha, uliopigwa katika uwanja wa shule ya msingi Moshono kwa lengo la kutaka kujua nani m’babe wa soka, Simba ilidhiirisha umwamba wake baada ya kuwapiga mashabiki wa Yanga jumla ya mabao 6-3.

Mchezo huo ulioanza kwa kasi ya aina yake na kujaza mamia ya mashabiki, Timu ya Simba ndio ilianza kupata mabao mawili ya haraka haraka ambapo bao la kwanza liliingizwa dakika ya sita mwa mchezo kupitia kwa Wilfred Kadege na Robert Boniface akipiga bao la pili dakika ya nane na kupelekea mashabiki kujigawa kwa ushangiliaji.

Wachezaji wa Yanga walionekana kujawa makali zaidi na kuongeza kasi ya kupambana kuligusa lango la Simba ambapo dakika ya 25 Frank Shapi alifanikiwa kuipatia timu ya Yanga bao la kwanza ambapo hata hivyo kipigo kwao kiliendelezwa na Robert Boniphace aliyeiandikia timu yake ya Simba bao la Tatu dakika ya 34 hali iliyozidisha hasira za wana-Yanga hao ya kulisakama lango la Simba ambapo hata hivyo Frank Kamili alijifunga katika harakati za kuokoa na kuiandikia timu ya Yanga bao la pili dakika ya 39 hadi mapumziko.

Kipindi cha pili kilianza huku timu ya Simba ikionekana na mabadiliko ya hali ya juu na mashambulizi ya iana yake na dakika ya 68 Wilfred Kadege aliiandikia samba bao la nne na  Robert Boniphace kuandika bao la tano dakika ya 75 hali iliyonyamazisha kelele za mashabiki wa nje wa Yanga na shangwe za mashabiki wa samba zikitawala na kuzidi kuvuta umati wa watu kushuhudia mtanange huo.

Baada ya mabao hayo wachezaji wa Yanga walionekana dhahiri kujawa na ghadhabu na jazba za hapa na pale huku wengi wakikoswa koswa na kadi za mwamuzi Gasper Getto lakini dakika ya 78 Mrope Mrope alibahatisha bao la tatu kwa timu yake ya Yanga baada ya kupiga shuti lisilo na matumaini ya kupata bao na dakika ya 86 Frank Kamili alifunga wingu la mvua ya mabao kwa timu ya Simba, na kuleta matokeo ya 6-3 hadi hadi dakika 90 kutia nanga.

Wakizungumza na gazeti hili, Kaptein wa timu ya Mashabiki wa simba Arusha, Wilfred Kadege alisema kuwa wameamua kutumia week end hiyo kuwafunga mdomo mashabiki wa Yanga kwamba wao ndio wababe wa kandanda baada ya kuweka matambo mengi kwa mdomo hivyo wakaamua kuwaonesha kazi ya Simba uwanjani.

“Tumeamua kutumia jumapili hii kuwafunga mdomo hawa watani wetu maana wamekuwa wanatamba sana mdomoni hasa baada ya kufanikiwa kucheza Kamari ya ligi kuu na kuwa mabingwa lakini wajue kuwa hawatufikii kwa lolote kwani kama ni zawadi ya kucheza mpira tunawazidi baada ya kucheza mtani jembe na kombe la Zanzibar tumeingiza zaidi ya watakachopewa kwenye ligi kuu milioni 75 sisi tumeshinda mechi mbili tuna milioni 120.”alijitamba Kadege.

Kwa upande wa msemaji wa timu ya mashabiki wa Yanga, Joram George alisema kuwa ingawa mchezo huo wamepoteza lakini wanaamini Simba hawajawazidi kitu zaidi ya kubahatisha mchezo huo baada ya wachezaji wengi wa timu yake kuwa majeruhi ikiwemo mlinda mlango namba moja ambapo amesema ili kudhihirisha hilo wataomba mechi ya marudiano wadhihirishe ubabe wao wa ligi kuu.

“tumepoteza kwa bahati mbaya tu huu mchezo lakini sisi yanga ndio kila kitu na ndio maana wanatupigia saluti tukiingia uwanjani na huu mchezo wamebahatisha baada ya wachezaji wetu wengi kuwa majeruhi lakini tutaomba mchezo wa marudiano na ukweli utajitenga na uongo”

Kwa upande wake kocha wa timu ya mashabiki hao wa Yanga kwa ujumla waliounga umoja wao wa mwangaza maveterani, Patson Mambete alisema kuwa mchuano huo wa kirafiki ulilenga kutoa burudani ya aina yake lakini pia kumaliza ubishi wa kila siku wa ubabe wa watu wa Simba na Yanga hapa mkoani Arusha.

Mwisho……………………..

0 comments:

Post a Comment