.

.
Tuesday, July 28, 2015

6:50 AM
Timu ya Arusha fc inayoshiriki ligi daraja la pili msimu ujao wa ligi ya Tanzania bara imejikuta ikihitaji zaidi ya milioni 28 kwa ajili ya kugharamia timu hiyo hadi kumalizika kwa SDL msimu wa 2015/2016, hivyo kuwaomba wadau watoe ushirikiano wao kuhakikisha fedha hizo zinapatikana.

Zaidi ya hayo wamewaomba wadau wa soka mkoani Arusha, kujitokeza katika kudhamini chochote katika timu hiyo ili kuwezesha kuwatangaza katika mikoa yote watakayocheza lengo ikiwa ni kutimiza azma yao ya kupanda hadi ligi daraja la kwanza.

Hayo yamejiri katika mkutano maalum wa wadau wa timu hiyo iliyofanyika hivi karibuni katika viwanja vya Sheik Amri Abeid uliokuwa na lengo la kujadili namna ya kuanza maandalizi ya ligi yao ya daraja la pili ikiwemo kufanya usajili, kutafuta kocha sambamba na benchi la ufundi na viongozi.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na wadau mbali mbali, Katibu Omari Kombo alisema kuwa hadi kumalizika kwa ligi timu inahitaji milioni 28 kwa ajili ya kugharamia usajili, malazi, usafiri pamoja na posho za wachezaji hivyo wadau watoe ushirikiano wao kuhakikisha hili linafanikiwa ikiwemo kutafuta wafadhili wa ndani na nje ya mkoa.

Katika mkutano huo wadau pia waliamua kuteua viongozi watakao isimamia timu hiyo hadi watakapo chagua viongozi wapya kwa mujibu wa katiba ya timu hiyo ambapo Abass Utanga alipewa nafasi ya mwenyekiti, Wille Mollel makam mwenyekiti, Salim Kombo katibu mkuu, Charles Mwaimu katibu msaidizi, Dr Kilavu mweka hazina.

Pia kamati ya usajili na ufundi walioteuliwa ni Denis Shemtoi, Denis Nyambele, John Change, Idd Mkulu, Azizi Nyoni, na Ally Wingi ambao Ndio watakao hakikisha AFC inakuwa katika hali ya ushidani zaidi ya msimu ulipita na kufanikiwa kupanda ligi daraja la kwanza.

SDL msimu wa 2015/2016, inayotarajia kuanza kutimua vumbi mwezi wa kumi tarehe 17 kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TFF huku AFC ikiwa imepangwa kundi B pamoja na Alliance FC [Mwanza], Madini FC [Arusha], Bulyanhulu FC [Shinyanga], JKT Rwankome [Mara], na Pamba ya Mwanza.

Mwisho…………….

0 comments:

Post a Comment