Arusha.Polisi mkoani
Arusha imekamilisha uchunguzi wake kuhusiana na kuungua kwa Ofisi za
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kusema wanachama wa chama
hicho ndio waliohusika.
Hata hivyo, Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema amepinga
kauli hiyo na kulipa jeshi hilo siku nne kuwakamata na kuwahoji
watuhumiwa watano baada ya kulipatia majina hayo akidai kuwa ndio
wanaohusika na uchomaji moto ofisi za chama hicho.
“Tumewapatia polisi majina... tunaamini walihusika moja kwa moja la
sivyo, chama kitatumia vijana wetu wa Red Brigade kuwakamata na
kuwafikisha polisi,” Lema aliwaambia waandishi wa habari jana.
Ofisi cha Chadema zilizoko katika eneo la Ngarenaro, zilinusurika
kuteketea kwa moto juzi baada ya watu wasiojulikana kuwasha moto katika
moja ya vyumba vyake.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Japhet Lusinga alisema:
“Katika uchunguzi wetu, tumebaini kuwa hakuna mahali palipovunjwa kutoka
nje ya uzio na kuruhusu watu kuingia ndani... tumegundua kuna tundu
dogo darini eneo la kuelekea bafuni la upana wa futi moja na nusu kiasi
haliwezi kuruhusu mtu kupita.
“Tumejiridhisha kuwa hakuna mtu anayeweza kupita hapo na ndani tulikuta majivu na baadhi ya vitu vilivyoungua na vifaa vingine.”
Lema akiwa na Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Arusha, Ephata Nanyaro
alisema: “Tumebaini polisi wanataka kulifanya jambo hili kama la siasa
ndiyo sababu juzi badala ya kuanza kuchunguza waliohusika, waliwakamata
Mtunza Ofisi na mlinzi wetu na kuwalaza rumande hadi leo (jana) asubuhi
kwa madai eti wanawahoji.
“Hatukubaliani na taarifa yao, hii ni siasa. Kulitokea mauaji ya bomu,
wakasema Chadema wamejilipua, leo ofisi imechomwa wanasema Chadema
wenyewe, hili hatukubali, “ alisema.
Msajili alaani
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi amelaani tukio
la kuchomwa moto ofisi hizo za Chadema na kusisitiza kuwa wananchi
hususan wanasiasa wasiwe wepesi kuingiza hisia kwenye makosa ya kijinai.
Alisema kuwa tukio hilo linapaswa kukemewa kwa hali yoyote ile kwa kuwa linavuruga na kuhatarisha amani ya nchi.
0 comments:
Post a Comment