Jeshi la polisi mkoani Arusha limemshikilia na kisha kumwachia
“chapchap” mtoto wa mwenyekiti wa CCM
wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro na mfanyabiashara maarufu nchini,Oscar Themi kwa kosa
la kumpiga risasi ya kichwa mhudumu wa bar ya Empire iliyopo eneo la
Shoprite jijini Arusha.
Mtuhumiwa huyo ,Dereck Themi alishikiliwa na polisi mwishoni mwa wiki
iliyopita mara baada ya kutofautiana na mhudumu huyo wakati alipompatia bili ya
vinywaji aliyokuwa akitumia ndani ya bar hiyo kabla ya kumtandika risasi.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa mashuhuda wa tukio hilo
walidai kuwa mnamo novemba 29 mwaka huu majira ya saa 7.30 usiku mtoto huyo wa
kigogo alimfyatulia risasi mhudumu huyo aliyetambulika kwa jina la Witness
Erasto wakati alipompatia bili ya vinywaji.
Mashuhuda walidai kuwa kulitokea na hali ya tofauti kati yao
ambapo Themi alikubali kulipa bili hiyo
ambapo alichukua fedha na kisha kumwekea katika matiti yake na ghafla kuchomoa
bastola yake na kisha kumtandika eneo la kichwa.
Kwa mujibu wa mashuhuda
wa tukio hilo walisema kuwa mara baada ya tukio hilo ndipo mtuhumiwa alijaribu
kukimbia nje ya bar hiyo kuelekea usawa wa eneo la maegesho la magari lakini
kabla hajafika alifyatua risasi nyingine zaidi ya tano hali iliyopelekea
tafrani katika eneo la Shoprite.
Hatahivyo,taarifa hizo zimedai kuwa askari mmoja aliyekuwa
akilinda benki ya Exim iliyopo ndani ya eneo hilo la Shoprite alimvizia kimafia
na kisha kumnyang”anya bastola hiyo mtuhumiwa kabla ya kuwataarifu polisi
waliofika eneo hilo na kisha kumfikisha katika kituo kikuu cha polisi cha kati.
Mtuhumiwa huyo alifikishwa katika kituo hicho na kisha kukabidhi
bastoa hiyo pamoja na maganda matano ya risasi ambapo baada ya muda aliwasili
mdogo wake aliyetambulika kwa jina la Bernad Themi aliyechukua mali zake na
fedha.
Akihojiwa na gazeti hili majeruhi wa tukio hilo Erasto
alisema kuwa hawezi kuongea chochote kwa kuwa hali yake ni sio nzuri lakini
alipotafutwa mmiliki wa bar hiyo,Tumaini Ulomi alikiri kutokea kwa tukio hilo
na kusema kuwa tayari wameshafungua mashtaka mbalimbali ikiwemo hasara
aliyoipata siku ya tukio.
Mmiliki huyo alisema kuwa mara baada ya milio ya risasi
kuanza kurindima ndani ya bar yake wateja mbalimbali wakiwemo watalii
walitokomea kusikojulikana bila kulipa hali ambayo imemtia hasara kubwa.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Arusha,Liberatus Sabas alikiri
kutokea kwa tukio hilo na kusema kwa kifupi kwamba bado wanafanya uchunguzi wa
kina kabla ya kulifikisha suala hilo mahakamani.
0 comments:
Post a Comment