.

.
Monday, March 23, 2015

3:36 AM
na Bertha Ismail - Arusha

Timu ya Tanzania veterani imewachabanga timu ya maveterani wa Kenya kwa jumla ya magoli 2-1 katika mechi ya kirafiki ya maveterani hao mapema mwishoni mwa wiki katika uwanja wa Sheik Amri Abeid ya jijini Arusha.

Timu ya Maveterani kutoka Kenya ijulikanayo kama Senious Footbal club walionesha uwezo mkubwa wa kusakata kandanda safi mithili ya Serengeti boy lakini pamoja na uwezo huo walishindwa kulinda lango lao vema na kuipa nafasi timu ya maveterani wa Tanzania “Arusha all stars” kutikisa nyavu zao dakika ya 35 kupitia kwa mchezaji wao Abdulrazaki Hussein matokeo yaliyodumu hadi mda wa mapumziko.

Kipindi cha pili kilianza huku mashambulizi makali yakielekezwa zaidi kwa lango ya Tanzania kwa mikwaju mikali ambayo hata hivyo iliokolewa na mlinda mlango mahiri wa Arusha all stars Godrich Samweli na baadae dakika ya 75 Kenya walisawazisha goli hilo kwa njia penalt iliyopigwa na Varees Aura, baada ya mchezaji wao kufanyiwa madhambi eneo la hatari.

Matokeo hayo yalionekana dhahiri kuwaamsha usingizini timu ya Arusha All stars na kuanza kuchangamkia lango la Senious fc ya Kenya ambapo mbali na mikwaju kadhaa kuchomolewa lakini dakika ya 80 Richard Lukas Manyika alifanikiwa kupiga shuti kali lililomuacha mlinda mlango wa Kenya na mpira huo kujaa nyavuni matokeo yaliyodumu hadi mwamuzi wa kati Gasper Ketto alipopuliza kipenga cha kuashiria mchezo kwisha.

Akizungumzia mechi hiyo, Katibu wa Arusha All stars alisema kuwa wameamua kuvuka mipaka ya Tanzania kwa kuwaalika maveterani wenzao wa Kenya wacheze pamoja huku ikiwa kama mazoezi kwao katika mashindano makubwa ya pasaka sambamba na kufahamiana lakini pia kujenga undugu wa kisoka baina ya nchi hizi.

“Sisi kama Arusha all stars tumevuka mipaka na kucheza na timu ya  Senious ya Kenya ambapo tunadumisha undugu wetu lakini pia ikiwa ni kama sehemu ya kutafuta marafiki wa soka ili kuendeleza soka la mkoa wetu na nchi kwa ujumla”

Mwisho……………………….

0 comments:

Post a Comment