.

.
Tuesday, June 18, 2013


KIKONGWE Somoe Issa, anayekadiriwa kuwa na umri zaidi ya miaka 90, ambaye aliwahi kutishia kuigeuza gesi kuwa maji iwapo serikali itaendelea kulazimisha kusafirisha kwenda Dar es Salaam, sasa hajulikani alipo. 
Taarifa zilizoifikia MTANZANIA Jumapili ambayo ipo mkoani Mtwara, zilidai kuwa bibi huyo baada ya kutoa tishio hilo sasa amefichwa, ili asiweze kutekeleza lengo lake hilo. 
Bibi Somoe, anayeaminika kama Mkuu wa Kaya ya Msimbati, kijiji ambacho gesi asilia iligundulika, sasa hajulik
ani alipo, huku ndani ya kijiji hicho ulinzi mkali ukiwa umeendelea kutawala.
Ulinzi umeimarishwa katika kijiji hicho, lengo likiwa ni kuhakikisha hakuna mtu anayefika karibu na nyumba aliyokuwa akiishi bibi huyo.
MTANZANIA Jumapili, lilifika katika kijiji hicho juzi, ambako liliweza kuzungumza na Mwenyekiti wa Kijiji cha Msimbati, Salum Athuman Tostao, ambaye alikiri kuwa bibi huyo hayupo na wala haifahamiki alikopelekwa.
“Ni kweli bibi huyu hajaonekana tangu palipotokea vurugu na watu wa usalama waliokuwa wakitaka kumuiba, kama unavyofahamu kulikuwa na mtu aliyejifanya mwandishi wa habari alitaka kumuiba bibi huyu, lakini wanakijiji wakamshtukia na kuchoma gari lake moto.
“Kutokana na hali hiyo, mpaka sasa hatufahamu alipo na hatujui kama ni serikali au wanafamilia wamemficha, kwa sababu kwanza hawaturuhusu hata sisi ambao ni viongozi kufika maeneo ya nyumba aliyokuwa akiishi kwa sababu wanadhani tutaleta watu wengine wasiokuwa waaminifu kwa familia hiyo,” alisema Tostao.
Gazeti hili lilipomtafuta mtoto wa bibi huyo, Manzi Faki, alikataa kuzungumza chochote kuhusu mama yake, lakini aliitaka serikali kutekeleza ahadi zake kwa Wanamtwara.
“Hilo suala la mama sitaki kulizungumzia kabisa… jambo la muhimu serikali inapaswa kufahamu kuwa sisi wana Mtwara tunataka itekeleze ahadi ilizotuahidi ndipo waje kuchukua hicho kidogo wanachokitaka, zaidi ya hapo kijumla gesi haitoki,” alisema Faki.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mtandi, Salum Waziri, alieleza kuwa bibi huyo anaaminiwa na wanakijiji wenzake kutokana na uwezo wake wa kuzuia mambo yasiyotakiwa ndani ya jamii, sambamba na kuleta riziki pale wanapokwenda kumuomba.
“Kwa kweli sasa ulinzi mkali umeimarishwa na wanakijiji, hakuna mtu anayefika nyumbani kwake, hata sisi wenyewe hatuthubutu, ndiyo maana hatufahamu alikopelekwa.
“Nakumbuka bibi aliwahi kutumiwa na kampuni ya Artumas kukwamua mashine iliyokuwa imenasa katika mchakato wa uchimbaji wa gesi hiyo baharini, ambapo wazungu hao walihangaika kuita wahandishi nje ya nchi, lakini wote wakashindwa, ndipo waliponong’onezwa kuhusu bibi huyo wakamwendea na akaja kunasua.
“Wakampa zawadi ya kumjengea nyumba, haya ni mambo ambayo yalitokea mwaka 1994, kiujumla yapo mengi ambayo yametufanya tumwamini sana,” alisema Waziri.
Januari mwaka huu, Afisa usalama mmoja anayedaiwa kufahamika kwa jina la babu alijikuta katika wakati mgumu kiasi cha gari lake kuchomwa moto huku yeye mwenyewe akikimbilia kusikojulikana baada ya kuzuka vurugu kubwa wakati akimshawishi bibi huyo asizuie gesi kwenda Dar es salaam. 
Inadaiwa kuwa mwanausalama huyo alitumwa na viongozi wa juu wa serikali baada ya bibi huyo kutamka wazi kuwa gesi haitoki Mtwara kauli ambayo iliwafanya viongozi kupata wasiwasi na hivyo kumtuma mtu huyo ili amshawishi bibi huyo.
Wakati bibi huyo akizungumza na mwanausalama huyo inadaiwa kuwa aliwaita wajukuu zake wamsikilize ndipo vurugu kubwa zilipoibuka na kusababisha mwanausalama huyo atimue mbio huku akilitelekeza gari lake.
Juzi na jana baadhi ya wakazi wa kijiji hicho wakizungumza na gazeti hili walisema wao hawazuii gesi kutumiwa na Watanzania, ila wanataka gesi hiyo ichakatwe hapohapo mkoani Mtwara na ndipo isafirishwe kuelekea sehemu nyingine.
Vurugu kuhusu gesi hii ya Mtwara zilianza kuibuka Novemba mwaka jana, wananchi wa mkoa huo walikuwa wakipinga ujenzi wa bomba la gesi kwenda Dar es Salaam. 
Pamoja na vurugu hizo kuzimwa mara kadhaa na Jeshi la Polisi, ambao sasa wanashirikiana na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), lakini bado MTANZANIA Jumapili imeshuhudia hali ya amani haijaweza kurejea mkoani humo.
Baadhi ya watu mkoani hapa, bado wanaendeleza visasi kwa kuchoma nyumba za wenzao, huku JWTZ wakidaiwa kuwapiga raia kila mara hata inapotokea kuwa wamezomewa.

0 comments:

Post a Comment