.

.
Friday, June 7, 2013

9:11 AM

Mr Abdulrahaman Kinana, CCM General Secretary.Katibu Mkuu CCM, Abdulrahman Kinana.
 CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema hakiungi mkono rasimu ya katiba mpya iliyozinduliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jumatatu wiki hii kwa asilimia mia moja.
Chama hicho kimesema kuwa wiki ijayo kitatoa msimamo wake kuhusu rasimu ya hiyo iliyoandaliwa na tume hiyo iliyoongozwa Jaji Joseph Warioba.

Kauli hiyo ya chama tawala ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wake, Abdulrah

man Kinana, baada ya kuulizwa na waandishi wa habari kuhusu msimamo wa chama chake juu ya rasimu mpya.
Kinana alisema uamuzi wa kutangaza msimamo wa chama utatokana na kikao cha Kamati Kuu (CC), kitakachokutana Jumatatu ijayo chini ya mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete.

“Kwa sasa hatuungi mkono rasimu hii kwa asilimia 100 wala kuipinga mpaka hapo tutakapokaa CC wiki ijayo na kuamua msimamo wetu ni upi katika hili,” alisema Kinana.

Alisema kila jambo ndani ya chama hicho huamuliwa kwa pamoja kupitia vikao na kwamba huo ndio utaratibu wao.

Miongoni mwa mambo ya msingi ambayo Tume ya Mabadiliko ya Katiba imeyapendekeza katika rasimu hiyo ni mfumo wa Muungano wa serikali tatu za Tanzania Bara, Zanzibar na Shirikisho.

Mfumo wa Muungano ni moja ya mambo ambayo serikali ya CCM imekuwa ikiyachukulia maamuzi kwa uangalifu mkubwa kwa kuwa ni sera ya chama hicho.

Hadi sasa sera ya CCM kuhusu Muungano ni mfumo wa serikali mbili za Muungano na ya Zanzibar.

Mapema miaka ya 90 suala la Muungano liliitikisa serikali ya awamu ya pili ya Alhaji Ali Hassan Mwinyi, ilijikuta katika mtikisiko mkubwa, baada ya kuridhia kuundwa kwa serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano.

Uamuzi huo ulitokana na shinikizo la kundi la wabunge 55 maarufu kwa jina la G55 ambalo lilikuwa linapinga uamuzi wa Zanzibar kuamua kujiunga na Jumuiya ya Kimataifa ya Kiislamu (OIC) kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Baada ya Bunge kupitisha hoja hiyo na serikali kuridhia, Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, aliingilia kati kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM  na kuwaambia wabunge wakiokuwa wakishinikiza kuundwa kwa serikali ya Tanganyika kusitisha hoja hiyo au kujitoa ndani ya CCM.

Mwalimu aliongeza kuwa viongozi wa kitaifa walioshauri vibaya Rais Mwinyi wawakibike au wawajibishwe.

Aidha, alitaka CCM kwenda kwa wanachama kuwauliza maoni yao kuhusu mfumo wa Muungano wanaoupendekeza kwa maelezo kuwa sera hiyo haiwezi kubadilishwa bila kuwauliza wanachama.
 Kufuatia uamuzi huo, NEC ilituma wajumbe katika maeneo mbalimbali ya nchi kukusanya maoni na wanachama wengi walisema wanataka mfumo wa serikali mbili uendelee.

Baada ya hapo aliyekuwa Waziri Mkuu na makamu wa kwanza wa Rais, John Malecela, aliondolewa katika nafasi hiyo na baadaye NEC ilimuondoa Hayati Horace Kolimba, katika nafasi ya ukatibu mkuu wa CCM.

Wakati wa uongozi wa awamu ya tatu wa Rais Benjamin Mkapa suala la mfumo wa Muungano liliibuka upya, lakini Mkapa alitumia nguvu kuzima mawazo ya kutaka serikali mbili.

Hata alipounda Tume ya kukusanya maoni chini ya uenyekiti wa Jaji Robert Kisanga kupitia utaratibu wa waraka maalum wa White Paper wa marekebisho ya katiba, Mkapa alikataa mapendekezo ya tume hiyo ya kupendekeza mfumo wa serikali tatu, akiwatolea lugha kali wajumbe wa tume kuwa hawakupewa adidu ya kutoa mapendekezo bali kukusanya maoni kuhusu Muungano.

Siala la mfumo wa Muungano huenda likazua mjadala mkubwa ndani ya CC kabla ya kutoa msimamo wa chama hicho.

TAMWA YALILIA HAKI

Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) kimewataka wajumbe wa Mabaraza ya Katiba kupigania kuondolewa kwa mapengo kuhusu haki za wanawake na watoto yaliyopo katika Rasimu ya Katiba ili kuleta haki, usawa na maendeleo nchini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Valerie Msoka, mchango wa wananchi ndiyo nguvu ya pamoja inayohitajika kuondoa unyanyasaji wa kijinsia na sheria kandamizi kwa mwanamke na mtoto wa kike.

Alisema Tamwa inaipongeza Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutoa rasimu, lakini rasimu hiyo haijaweka bayana misingi itakayomlinda mwanamke na mtoto wa kike dhidi ya vitendo vya ukatili vikiwamo ubakaji, ndoa za umri mdogo na ukeketaji wa watoto wa kike.

Aliongeza kuwa rasimu imeeleza haki za mtoto wa kike, lakini haijaweka bayana vipengele vya kumlinda ili kumwezesha kupata huduma za jamii ikiwa ni pamoja na elimu itakayomuwezesha kudai, kutetea na kumlinda dhidi ya ukatili wa kijinsia.

“Kuna ukimya pia kuhusu umri wa kuolewa, jambo ambalo linapelekea mtoto wa kike chini ya miaka 18 kuolewa kwa ridhaa ya wazazi au walezi wake,” alisema Msoka.

Msoka alisema Rasimu hiyo imebainisha kuwapo kwa haki sawa katika nafasi za uongozi wa bunge, lakini kumekuwa na ukimya katika ngazi nyingine za uongozi kama vile katika vyama vya siasa, mawaziri, serikali za mitaa, mabalozi na makatibu wakuu.

Alisema kwa kufanya hivyo kutapelekea ushiriki sawa wa wanawake katika nyanja zote za uongozi.

Alisema rasimu hiyo inatoa haki ya mwanamke ya huduma ya juu ya afya inapopatikana, lakini haijabainisha haki za uzazi salama wala kuiwajibisha serikali kuwekeza katika afya ya uzazi pamoja na kumlinda mwanamke katika jukumu zima la uzazi.

“Ingawa Rasimu imezungumzia kuheshimiwa kwa mikataba ya kimataifa kuhusu haki za binadamu, imeshindwa kuweka bayana utekelezwaji wa Kitaifa wa mikataba ambayo Tanzania imetia saini,” alisema Msoka.

Aliongeza kuwa katika kuleta mabadiliko yatakayoleta maendeleo nchini, fursa ya mabaraza ya kuiangalia rasimu ya katiba ni fursa ambayo itahakikisha kuondolewa kwa mapungufu yaliyopo ili kuwapo na usawa na haki kwa Watanzania wote.
 
chanzo: nipashe

0 comments:

Post a Comment