.

.
Tuesday, June 18, 2013


MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amefichua siri kuhusu tukio la mlipuko wa bomu lililotokea jusi katika viwanja vya Soweto, jijini Arusha.

Katika kauli yake jana, Mbowe ameibua tuhuma nzito dhidi ya Jeshi la Polisi, ambapo alidai kuwa askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) ndiye aliyerusha bomu hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa,baada ya kutembelea majeruhi katika Hosp

itali ya Selian, Mbowe alisema chama chake kina ushahidi wa kutosha juu ya askari huyo kurusha bomu.

Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni,alisema wamefanikiwa kupata ushahidi wa kutosha juu ya tukio hilo baya linalochafua taswira ya nchi.

Alisema chama chake kipo tayari kuweka ushahidi huo hadharani, iwapo Serikali itaendelea kufanya siasa na kuficha ukweli.

“Tunao ushahidi wa kutosha, ikiwamo wa picha za video unaoonyesha shambulio la bomu na risasi lilivyofanyika katika mkutano wangu jusi eneo la Soweto.

“Picha zinaonesha wazi aina ya silaha zilizotumika kwenye shambulio lile ni tatu, bomu la gurumeti ambalo lilitupwa na askari wa FFU aliyekuwa kwenye uniform.

“Kutokana na ushahidi huu tulikuwa tumewaeleza Polisi kama wataendelea kuficha tutaueleza umma na tutaiambia dunia, kwani aina ya silaha zilizotumika ni SMG na bastola.

“Makasha ya risasi kama ushahidi wa jambo hili zilizotumika tuliyaokota eneo la tukio na tayari tumeyarekodi na kuyakabidhi kwa askari waliokuwa wakichunguza tukio lile,” alisema Mbowe.

Hata hivyo Mbowe alipinga tamko la Serikali kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uratibu na Bunge), William Lukuvi na kusema kauli yake ni ya kitoto mbele ya jamii.

“Kauli ya Serikali kupitia kwa Lukuvi kwamba vurugu zilisababishwa na vikundi, wanasiasa na mashirika yasiyo ya kiserikali ambavyo havijulikani ni sawa na kuwadhihaki Watanzania,” alisema.

Kutokana na hali hiyo Mbowe alisema tayari wanasheria wa chama hicho akiwemo Mabere Marando, Tundu Lissu na Profesa Abdallah Safari wanashughulikia suala hilo.

Alisema baada ya polisi huyo kurusha bomu, alikimbilia katika gari ya Toyota Land Cruizer yenye rangi ya bluu akiongozana na askari mwenzake ambapo gari hilo liliondoka kwa kasi, huku likisindikizwa kwa kukingwa na gari ya TDI hadi kituo cha polisi.

SPIKA

Alisema anashangazwa na hatua ya Spika wa Bunge Anne Makinda, kushindwa kuguswa na jambo hilo ambalo limelitikisa taifa na kuruhusu Bunge liendelee.

Alisema Spika Makinda, ameendelea kuongoza Bunge licha ya Hotuba ya Waziri Kivuli wa Fedha kuwekwa kando kutokana na tukio hilo lililovuta hisisa za watu wengi.

“Kila linapotokea tukio kubwa la mauaji kama haya shughuli za Bunge husimama ili kulishughulikia, lakini Spika hakushtuka hata pale alipoona wabunge wote wa Chadema hawapo bungeni.

“Spika Makinda ameshindwa hata kunipigia simu hata ya kunipa pole kama mbunge niliyenusurika kuuawa …. Yaani hawajaona sababu sababu ya kufanya hivyo na huenda watu waliokufa hawana thamani kwao, wameona ni sawa na kuku.

“Jeshi la Polisi, wamekuwa na kazi ya kuchunguza mambo yasiyoisha, inakuwaje waue wenyewe halafu wajichunguze? msione misafara ya magari ya viongozi yanakuja hapa hospitali ni unafiki mtupu.

“Wanawajua wauaji, tutayaweka haya yote hadharani sura za wauaji zitaonekana na suala hili tutalipigania mpaka haki itendeke ikibidi hata mpaka umoja wa mataifa,” alisema Mbowe.

Hata hivyo, aliishauri serikali kwa kuiambia kuwa kama haitaki ushindani wa vyama vya upinzani ni vema ikavifuta vyama vya siasa vilivyopo kulikoni kuendelea kuwaua wananchi wasio na hatia wakiwemo watoto wadogo wanaposhiriki shughuli za siasa.

SHILINGI MILIONI 100

Katika hatua nyingine, Serikali imeamua kutenga Sh milioni 100 kama zawadi kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa zitakazofanikisha kunaswa kwa mhalifu au watu wenye mtandao wa ulipuaji mabomu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi, alisema bungeni mjini hapa jana, kuwa kila mtu mmoja atakayetoa taarifa za siri na za uhakika kufanikisha kukamatwa kwa mhalifu huyo, atapatiwa Sh milioni 10 “hadi fedha hizo ziishe na serikali ina uwezo wa kuongeza fedha zaidi hadi mtu huyo apatikane.”

Lukuvi,alikuwa akitoa kauli ya Serikali kuhusu mlipuko uliotokea katika mkutano wa hadhara wa kampeni za uchaguzi katika Kata ya Sowote, Arusha, Jumamosi iliyopita. Mkutano huo, ulikuwa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Alisema mtu yeyote atakayetoa taarifa hizo atahakikishiwa usalama wake na polisi.

Alisema watu wawili walikufa katika tukio hilo, ambao ni Judith William (48) na Ramadhani Juma (15), huku watu 70 wakijeruhiwa, watatu vibaya na kati yao wawili hali zao ni mbaya.

Alisema uchunguzi wa awali, umeonyesha mlipuko huo ulikuwa wa bomu la kurushwa kwa mkono, lililorushwa kutoka upande wa mashariki kuelekea magharibi, kulikokuwa na gari aina Fuso lililokuwa likitumika kuhutubia.

“Jaribio la polisi kutaka kumfuata aliyerusha bomu hilo lilizuiliwa na makundi ya wananchi, ambao walianza kuwashambulia polisi kwa mawe na kuwazomea na hivyo polisi kulazimika kuanza kujiokoa badala ya kumsaka mhalifu huo.

“Aina ya urushaji wa bomu hilo, hautofautiani na mbinu iliyotumika kwenye shambulio jingine la bomu lililotokea Mei 5, mwaka huu, katika Kanisa Katoliki la Olasiti katika jiji hilo hilo la Arusha,” alisema.

“Nataka niwaambie wahalifu hao kuwa njama zao za kutugawa kwa misingi ya dini, makabila, rangi, rasilimali na itikadi za vyama zitashindwa.

“Tutapambana nao usiku na mchana kwa silaha zote tulizonazo mpaka tutakapowashinda na kuwafikisha mbele ya mikono ya sheria,” alisema.

MBATIA

Naye Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), James Mbatia, ameitaka Serikali kuchukua hatua za haraka kukabiliana na hali ya uvunjifu wa amani iliyopo nchini.

Mbatia alitoa taarifa hiyo mjini Dodoma jana, wakati akizungumzia tukio la bomu lililotokea mkoani Arusha.

Alisema imekuwa kawaida ya Serikali yanapotokea matukio ya mauaji kama ya Arusha, kutoa majibu mepesi.

"Zamani ilikuwa nadra kutokea kwa matukio ya kuuana wenyewe kwa wenyewe, sasa imekuwa kama utamaduni.

“Hii inatokana na wenye mamlaka kutoa majibu mepesi ambayo hayana utekelezaji, tunapaswa kusema na kutenda, vinginevyo nchi inaelekea kubaya," alisema Mbatia.

“Kuanzia matukio ya Mtwara na matukio ya mabomu Arusha, kauli zinazotolewa na Serikali ni za kubabaisha.

CHANZO MTANZANIA

0 comments:

Post a Comment