.

.
Wednesday, July 3, 2013

Yatatimia? Alipokuja nchini na Al Nasir Juba kucheza na Azam FC, mpenzi wa Simba SC na mmiliki wa hoteli Sapphire Court, Abdulfatah Salim Saleh (kulia) alimkabidhi jezi yake James (kushoto) kuashiria kumkubali mchezaji huyo na akasema atapenda aje Msimbazi. Sasa leo anatua Dar es Salaam kwa majaribio ya kujiunga na Wekundu hao wa Msimbazi. Atafuzu? 
Na Mahmoud Zubeiry,
SIMBA SC inaendelea na jitahada za kuimarisha timu yake kwa kusaka wachezaji bora na jioni ya leo wachezaji wawili wa kimataifa wa Uganda na Sudan Kusini watatua nchini kwa ajili ya majaribio.
Kutoka Uganda, ni beki Assumani Buyinza aliyemaliza Mkataba wake katika klabu moja Vietnam wanakocheza pia Mtanzania Danny Mrwanda na mshambuliaji Mganda, Moses Oloya ambaye Simba walimtaka sana, lakini akawaambia wasubiri amalize Mkataba Oktoba.
Kutoka Sudan Kusini ni Kon James wa Al Nasir Juba ambayo ilitolewa na Azam FC katika Raundi ya Kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba wachezaji hao wanakuja kwa ajili ya majaribio na wakimvutia kocha Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’ watasajiliwa.
Poppe amesema kwamba Buyinza ni beki wa kati mwenye uzoefu ambaye wana matumaini anaweza kukidhi vigezo vya King Kibadeni, wakati James ni mshambuliaji mzuri ambaye walijionea wenyewe alipokuja na Nasir Juba kucheza na Azam.
Azam iliitoa Al Nasir Juba ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 8-1, ikishinda 3-1 Dar es Salaam na 5-0 ugenini, lakini James aling’ara katika mechi zote.
Tayari Simba ina wachezaji watatu wa Uganda katika kikosi chake, ambao ni kipa Abbel Dhaira, beki Samuel Ssenkoom na kiungo Mussa Mudde. Dhaira na Mudde wanaingia katika msimu wa pili Msimbazi, wakati Ssenkoom ndio kwanza amesajiliwa.  

0 comments:

Post a Comment