Chadema
kimepinga kauli ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji
Joseph Warioba kuhusu hatima ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 kikisema mchakato
wa sasa wa Mabaraza ya Katiba, usiwe kikwazo cha mjadala wa muundo wa
Serikali Tatu.
Mkurugenzi
wa Mawasiliano wa Chadema, John Mnyika alisema Dar es Salaam jana kuwa
hatima ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 utakaotokana na mchakato wa mabadiliko
ya Katiba unaoendelea, siyo suala la kusubiri.
Akizungumza
na mwandishi wetu juzi kuhusu kauli ya Waziri wa Katiba na Sheria
Mathias Chikawe kwamba endapo mapendekezo ya Serikali Tatu yatapitishwa,
kuna hatihati ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 kufanyika, Jaji Warioba alisema:
“Tuachieni muda… hayo mengine ni hisia tu. Ni kweli tunayajua lakini
acheni tumalize hili kwanza ( la Mabaraza ya Katiba). Hii ndiyo hatua
tuliyopo sasa.”
Lakini
jana Mnyika alisema: “Hatuwezi kusubiri hadi Mabaraza ya Katiba
yakamilishe mchakato kama alivyoeleza Jaji Warioba katika gazeti lenu la
Mwananchi toleo la leo, (jana),” alisema Mnyika kwa simu.
Jaji
Warioba alitaka suala la muundo wa Serikali Tatu utakavyokuwa lisiwe
hoja kwa sasa kwa kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba inachokifanya ni
kukusanya maoni kupitia Mabaraza ya Katiba na kisha kuandaa rasimu
itakayopelekwa bungeni kwa ajili ya majadiliano na kwamba mjadala huo
utawachanganya wananchi endapo utaingizwa katika hatua hii ya ukusanyaji
maoni.
Lakini
Mnyika alisema: “Mijadala hii haiwezi kusubiri mpaka hatua ya Mabaraza
ya Katiba, inapaswa kuanza wakati huu kupitia mabaraza yanayosimamiwa na
Tume na Mabaraza yanayoendeshwa na makundi ya kijamii. “Pia, masuala
hayo ya mpito pamoja na marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,
ni mambo ambayo yanapaswa kutolewa ufafanuzi wa ziada na Serikali zaidi
ya kauli ambayo Waziri wa Sheria na Katiba Mathias Chikawe ameitoa
kupitia gazeti la lenu la leo (jana).”
Alisema
kimsingi bado kunahitajika mjadala wa masuala ya mpito kwa sababu kuna
uwezekano kwamba Katiba Mpya, ya Muungano au ya Zanzibar na ya
Tanganyika, isiwe tayari kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015, endapo suala la
Serikali tatu litapita.
Alisema
kwa upande mwingine, rasimu ya Katiba iliyotolewa imeibua mjadala juu ya
mkwamo wa kikatiba (constitutional stalemate), ambao ni muhimu upatiwe
suluhisho akisema chama chake kinapendekeza mchakato wa Katiba Mpya ya
Tanganyika uanze mara moja ili uende sambamba na huu wa Katiba Mpya ya
Muungano. Alisema ilikuwa vyema yote yakajadiliwa katika Bunge la Agosti
27, mwaka huu.
Waziri
Chikawe alikaririwa na gazeti hili juzi akisema: “Uwepo wa Serikali tatu
utafumua mfumo mzima wa utendaji ndani ya Serikali. Hatuwezi tena
kufanya uchaguzi wa Rais na wabunge 2015, hatuwezi kufanya chochote nje
ya Katiba ya Serikali Tatu kwa kuwa kinachofuata ni kuunda Katiba
nyingine inayohusiana na Serikali tatu.
Waziri Chikawe afafanua
Juzi,
Waziri Chikawe alitoa ufafanuzi juu ya utata wa hoja zake kwa kuipongeza
Tume ya Jaji Warioba kwa kazi inayofanya huku akisema anaunga mkono
msimamo wa CCM wa kutaka kuendelea na muundo wa Muungano wa Serikali
mbili.
Alisema mchakato wa kuandika Katiba Mpya unapaswa kuangaliwa kwa jicho pana zaidi ya lile la Uchaguzi Mkuu wa 2015.
0 comments:
Post a Comment