.

.
Tuesday, April 22, 2014

9:18 PM

SHARE THIS STORY
0
Share


Ni bahati mbaya kwamba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linalotarajiwa kuanza kikao chake Mei 6, mwaka huu mjini Dodoma litalazimika kuendeshwa ‘fastafasta’ kutokana na kutengewa siku chache kukamilisha shughuli zake. Kama inavyofahamika kwa wengi, utaratibu wa sasa unalitaka Bunge hilo kuwa limejadili na kupitisha Bajeti ya Serikali pamoja na Sheria za Fedha ifikapo mwishoni mwa Juni kila mwaka, ili kuruhusu bajeti husika kuanza kutumika Julai Mosi, ambayo ndiyo siku ya kwanza ya mwaka mpya wa fedha.
Tunazo sababu mbili za msingi tunaposema ni bahati mbaya Bunge la Bajeti kulazimika kuendeshwa ‘fastafasta’. Kwanza ni ukweli kwamba mijadala kuhusu Bajeti Kuu ya Serikali na bajeti za wizara mbalimbali haitakuwa ya kina kutokana na ufinyu wa muda. Pili, kutokana na ufinyu huo wa muda, kuna uwezekano mkubwa Bajeti Kuu ya Serikali na za wizara nyingi kubwa na nyeti kama Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo inatumia zaidi ya theluthi moja ya bajeti nzima ya Serikali, zikapitishwa zikiwa na takwimu za kupikwa na za kufikirika zilizobuniwa na watumishi wasio waaminifu wanaoendesha mitandao ya wizi wa fedha za Serikali.
Hatari itakayotokana na hali hiyo ni kupatikana kwa bajeti zisizokuwa na uhalisia, kwani hata Kamati za Bunge zimepewa wiki moja tu kujadili bajeti husika, badala ya wiki tatu. Matokeo ya kazi za kurashiarashia namna hiyo ni kulifanya Bunge kuwa mhuri wa kupitisha madudu na kuhalalisha vitendo vya wizi, ufisadi na ubadhirifu wa fedha za Serikali. Ratiba ya Bunge hilo inaonyesha kuwa, Bunge la Bajeti litakutana kwa siku 52, zikiwa pungufu kwa siku 28, ikilinganishwa na mkutano kama huo mwaka jana.
Swali la kujiuliza hapa ni hili: Kwanini Bunge limefikia hali hiyo? Pamoja na Uongozi wa Bunge kusema siku nyingi zimetumika kwenye shughuli za Bunge Maalumu la Katiba, halisemi kwanini mamlaka husika haikushauriwa kuahirisha Bunge hilo la Katiba ambalo limetumia siku 67 katika malumbano na mijadala isiyokuwa na tija kwa taifa. Bunge la Bajeti lingepewa kipaumbele kwa sababu ndilo uti wa mgongo wa shughuli za Serikali na taasisi zake.
Sisi tunadhani kwamba yalikuwa makosa makubwa kuwaacha mawaziri na wabunge wa Bunge la Muungano wakijikita katika siasa na itikadi za vyama ndani ya Bunge Maalumu la Katiba, huku wakijua fika kwamba Bunge la Bajeti lazima liwe limepitisha Bajeti na kumaliza mkutano wake ifikapo mwishoni mwa Juni. Pamoja na kutambua kwamba kutofanya hivyo kunaweza kusababisha majanga kwa taifa, bado waliona kipaumbele ni siasa na malumbano yasiyoisha kuhusu ‘kura iwe ya siri au ya wazi’ na ‘muundo wa serikali mbili au tatu’. Hayo ndiyo matokeo ya kuweka siasa mbele na kudidimiza uchumi.
Sasa nini kifanyike? Spika anaweza kujaribu kuokoa jahazi kwa kutoruhusu porojo bungeni. Mawaziri wawasilishe bajeti fupi lakini zilizosheheni takwimu sahihi na tafakuri jadidi. Michango ya wabunge ilenge kwenye hoja na wasipewe muda wa kupongezana na kuwatambulisha marafiki, mashemeji na kadhalika. Iwapo kanuni na ratiba vitapanguliwa ili vikao vifanyike mchana na usiku, siku za kazi na za mapumziko, itawezekana kupatikana kwa bajeti zilizochambuliwa barabara, zenye mwelekeo na endelevu.
mwananchi

0 comments:

Post a Comment