.

.
Wednesday, April 9, 2014

Yanga yaipumulia Azam FCMABINGWA wa soka Tanzania Bara, Yanga, jana walizidi kujiweka karibu na vinara wa ligi hiyo, Azam FC, baada ya kuifunga Kagera Sugar katika mechi ngumu iliyopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Katika mchezo wa jana, Yanga iliuanza kwa kasi na kuwachukua dakika tatu tu kujipatia bao, likifungwa na Hamis Kiiza, baada ya kutokea piga ni kupige baada ya krosi ya Mrisho Ngasa.
Baada ya bao hilo, wachezaji wa Kagera walimvamia mshika kibendera, wakidai mpira ulikuwa umetoka, kabla ya mwamuzi wa kati, Maalim Abbas kuwataka warejee uwanjani.
Dakika ya 34, Didier Kavumbagu, aliongeza bao la pili akimalizia pasi safi ya Simon Msuva.
Kagera Sugar, walijibu dakika ya 38, baada ya George Kavila kupiga shuti kali nje ya 18 na Dida kupangua kabla ya dakika ya 45, mpira wa Themi Felix kudakwa na Dida.
Hadi Mwamuzi anaashiria mapumziko, Yanga walitoka kifua mbele kwa mabao 2-0.
Kipindi cha pili, timu zote ziliingia kwa kushambuliana kwa zamu na baada ya kosa kosa kadhaa, Kagera Sugar walijipatia bao dakika ya 62 likifungwa na Daudi Jumanne, baada ya uzembe wa mabeki kurudishiana mpira na mfungaji kuupitia.
Timu zote ziliendelea na kosa kosa kwa zamu, huku ikishuhudiwa dakika ya 90, Kavumbagu na Ernest Mwalupani wakizozana na mwamuzi kuingilia kati na kuwaachanisha. Hadi filimbi ya mwisho, Yanga 2, Kagera Sugar 1.
Baada ya mechi kumalizika, Paul Ngwai wa Kagera Sugar alimnasa kibao Juma Abdul na kuwafanya baadhi ya wachezaji wa Yanga kuvamia benchi la Kagera. Mwamuzi wa akiba ilibidi aingilie na kumsindikiza Ngwai kuingia vyumba vya kubadilishia.
Katika mchezo wa jana, mshambuliaji wa kimataifa wa Yanga, Mganda, Emmanuel Okwi, alionekana jukwaani huku akiwaangalia wenzake, akiwa amejifunika sweta lenye kofia.
Yanga: Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Canavaro’, Mbuyu Twite, Frank Domayo, Simon Msuva, Hassan Dilunga, Didier Kavumbagu, Mrisho Ngasa/Hussein Javu na Hamis Kiiza/Nizar Halfan.
Kagera Sugar: Agaton Anthony, Salum Kanoni, Mohamed Hussein,  Ernest Mwalupani, Maregesi Mwangwa, George Kavila, Benjamin Asukile/Juma Mpola, Daudi Jumanne, Adam Kingwande/Zuber Dadi, Themi Felix/Hamis Kitagenda na Paul Ngwai.
Kwa ushindi huo, Yanga imefikisha pointi 52 ndani ya mechi 24 na kuwasogelea Azam FC yenye pointi 53 ikiwa na mechi 23.
Azam FC jana ilikuwa iumane na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Mabatini Mlandizi, Pwani, lakini kutokana na mvua kubwa iliyonyesha, mechi ilibidi iahirishwe hadi leo kutokana na kujaa maji.

0 comments:

Post a Comment