.

.
Sunday, April 20, 2014


TIMUATIMUA ya askari wa Jeshi la Polisi iliyotangazwa wiki iliyopita na  Kamanda wa  Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani  nchini, Mohamed Mpinga, imemuibua Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei, na kusema hatambui kama kuna askari wake wamefukuzwa kazi.
Kauli ya Kamanda Matei imekuja huku kukiwa na malalamiko kutoka kwa askari waliofukuzwa kuwa baadhi ya viongozi wao wa mikoa wamefikia uamuzi huo kinyume cha sheria na mapendekezo ya waendesha mashitaka wa Jeshi la Polisi waliosikiliza mashitaka yao.
Matei alisema anachojua kwa askari wa mkoa wake kuna kesi inaendelea na bado haijamalizika.
“Kwangu hakuna aliyefukuzwa, waliopo kesi zao bado zinaendelea. Lakini mbona mnaandika sana mambo ya jeshi letu? Tunahangaika usiku na mchana kwa ajili ya ulinzi na taarifa kama hizi zinawakatisha wengine tamaa, kwani hata majeshi mengine yanafukuza, lakini hawaandikwi kama sisi,” alisema Matei.
Askari hao walioomba wasitajwe majina walisema uamuzi wa kuwaondoa kazini umefanywa kwa lengo la makamanda kujikosha kwa mkuu wa jeshi hilo nchini, IGP Ernest Mangu, hivyo kumuomba atumie busara kuhakikisha haki inatendeka dhidi yao.
Hivi karibuni Kamanda Mpinga akizungumza na waandishi wa habari, alisema kikosi chake kimewafukuza kazi askari 10 kwa tuhuma za kwenda kinyume na maadili ya jeshi hilo ikiwa ni pamoja na kubainika kufanya vitendo vinavyoashiria rushwa.
Ingawa katika mkutano huo Kamanda Mpinga hakutaja majina ya  askari hao, Tanzania Daima imedokezwa kuwa waliokuwa katika mkumbo huo ni 15 na si 10, kwamba hali ya kupunguza idadi na kuacha kutaja majina ilikuwa na lengo la kuwaokoa baadhi ya askari wenye undugu na baadhi ya viongozi wa juu wa jeshi hilo.
Majina ya askari waliotimuliwa ni Koplo Japhari, Koplo, Swaumu, Koplo Zua Koplo Johari, Pc Prisca, Pc Charles  na Pc Christina ambao wanaotoka Mkoa wa Kipolisi Temeke na wengine ni Pc Hawa, Pc Evarist Pc Athumani,  Pc Johanes Cp Frank,  Sg Robison  na Cp  Salehe wanaotoka Mkoa wa Pwani.
Polisi waliofukuzwa kutoka Mkoa wa Temeke walisema msingi wa tuhuma zao zilianza Machi mwaka huu katika kikao cha makamanda wa polisi Tanzania kilichofanyika mkoani Kilimanjaro na kuhudhuriwa na IGP Mangu.
Chanzo cha habari kilieleza katika mkutano huo, mikanda mbalimbali ya video ilitolewa kwa ajili ya kujiridhisha juu ya mienendo ya askari wanapofanya kazi huku mikoa ya Temeke, Pwani na Morogoro makamanda wake wakitakiwa kuzipitia kwa umakini taarifa zilizoonyeshwa na kufanya uamuzi wa haki kwa watakaobainika kufanya makosa.
“Temeke kulikuwa na mikanda miwili, mmoja ulikuwa  haueleweki na kwa kweli ulikuwa mbaya na  mwingine ulikuwa unaonyesha askari wakiwa wanaongea na dereva wa daladala na kisha kuanza kuandika kwenye kitabu cha malipo, na haya ndiyo yaliyozingatiwa na mwendesha mashitaka katika kesi ya kipolisi mpaka akapendekeza adhabu ya wengine kushushwa vyeo na wengine kukatwa mishahara ya siku saba,” kilisema chanzo chetu ndani ya jeshi hilo.
Hata hivyo, inadaiwa mapendekezo yaliyotolewa na mwendesha mashitaka wa mahakama ya kipolisi Mkoa wa Temeke yalipuuzwa na Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Englibert Kiondo, na kuamua kuwafukuza kazi askari nane.
Alipoulizwa Kamanda Kiondo sababu ya kupuuza mapendekezo ya hukumu ya wanasheria walioendesha kesi katika mahakama ya kijeshi, alisema mahakama hiyo inaendeshwa kwa siri na kwamba anayetoa uamuzi ni yeye.
“Unazungumziaje uamuzi wa mahakama ya kijeshi? Nani kakwambia habari hizo wakati kesi zinaendeshwa kwa siri? Mimi siwezi kuzungumzia mambo hayo, na kama kuna mtu anaona ameonewa akate rufaa milango ipo wazi kwa Afande IGP,” alisema Kamanda Kiondo.
tanzania daima

0 comments:

Post a Comment