KAMATI ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Mbeya
limepiga marufuku maandamano yoyote kufanyika Mkoani hapa yenye lengo la
kushinikiza Raisi Kikwete kumfukuza kazi Waziri wa Elimu kutokana na matokeo
mabaya ya kidato cha nne.
Maandamano hayo yalipangwa kufanywa na Chama cha
Demokrasia na Maendeleo( CHADEMA) Machi 25, Mwaka huu, ambayo yamepangwa
kuhusisha Mikoa yote ya Nyanda za Juu Kusini na kufanyika Jijini Mbeya kwa
lengo hilo.
Akitoa taarifa ya Kamati hiyo kwenye Mkutano wa
ushauri wa Mkoa (RCC),Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Dk. Norman Sigalla amesema
kamati hiyo ilikaaa Machi 19, mwaka huu na kuamua kuwa hakuna mantiki ya
kufanyika kwa maandamano hayo.
Amesema sababu iliyoonekana ni kwamba tayari tume
imeshaundwa kuchunguza madai hayo hivyo hamna sababu ya watu kuandamana
kushinikiza waziri kujiuzulu ili hali kamati itakuja na majibu juu ya kile
kilichosababisha matokeo kuwa mabaya.
Sigalla amesema kamati ya Ulinzi na Usalama
imeona kuwa kuendelea kufanya maandamano soyo ufumbuzi wa matatizo bali
yataathiri shughuli za kujitafutia kipato kwa wananchi wa kawaida pamoja na
usalama wa mali.
Ameongeza kuwa usalama wa Wananchi wa Mkoa wa
Mbeya utaathirika kutokana na wanaotarajiwa kufanya maandamano hayo
wamehamasishwa kutoka mikoa ya Iringa, Njombe, Ruvuma ambako kutajaza
idadi kubwa ya watu.
Amesema kamati pia inaamini kuwa maandamano ya
aina hiyo yanaweza kusababisha uvunjifu wa amani hivyo kamati inapiga
marufuku maandamano ya aina yoyote kufanyika Mkoani Mbeya na kuongeza kuwa
yapelekwe maeneo mengine.
Aidha ametoa rai kwa vikundi vya kisiasa, kijamii
na vikundi vya dini kuweka mbele maslahi ya wananchi kwa kuhimiza kujitafutia
vipato kutokana na fursa za maendeleo zilizopo.
Hata hivyo Mwenyekiti huyo wa kamati ya Ulinzi na
Usalamaya Mkoa ameviagiza vyombo vyote vya Ulinzi na usalama kuendelea
kuhakikisha kwamba Mkoa wa Mbeya unaendelea kuwa tulivu na amani ambayo
itawezesha wananchi kuendelea na shughuli za kujiongezea kipato bila bugudha
yoyote.
Maandamano hayo yamepangwa kufanyika Machi 25,
Mwaka huu kufuatia Mkutano wa Hadhara uliofanyika hivi karibuni wa Chadema
katika Viwanja vya Shule ya Msingi RuandaNzovwe Ilomba Jijini Mbeya Februari
28, Mwaka huu, ambapo Mwenyekiti wa Chama hicho taifa Freeman Mbowe aliagiza
kufanyika kwa maandamano hayo kwa namna yoyote ile.
Pia katika kuhakikisha dhana hiyo inatimia
Mwenyekiti huyo pia alichangisha zaidi ya Shilingi Milioni Tatu ambazo alidai
kuwa zitasaidia wakati wa maandamano katika kununulia maji ya kunawa baada ya
kupigwa na mabomu pia kununulia dawa za huduma ya kwanza kwa watakaoathirika na
maandamano hayo.
|
0 comments:
Post a Comment