Makadinali wa kanisa katoliki la
Roma wameanza shughuli ya kumchagua papa mpya. Misa maalum imeandaliwa
katika makao makuu ya kanisa hilo Vatican, St. Peter's Basilica. Baada
ya misa makadinali wote walio na umri wa zaidi ya miaka 80 wataingia
hekalu ya Sistine ambako upigaji kura utafanyika.
Makadinali hao 115 watafungiwa ndani ya hekalu,
bila mawasiliano na yeyote nje na wataapishwa kuweka siri ya matukio
yote wakati wa uchaguzi huo. Inaaminiwa kuwa shughuli hiyo huenda
ikadumu siku kadhaa.
Mwandishi
wa BBC mjini Roma anasema kuwa hakuna mgombea wa wazi anayetazamiwa
kuchukua mahala pa Papa mtakatifu Benedikt wa kumi na sita.
Papa huyo
aliwashangaza wengi alipotangaza kujiuzulu baada ya kuhudumu miaka
minane. Yeye ndiye papa wa kwanza kujiuzulu katika miaka 600 iliyopita.
Maelfu ya waumini wa madhehebu ya katoliki
wamekusanyika nje ya kanisa la St. Peter's Basilica, kufuatilia kwa
karibu shughuli hii muhimu ya kumteua kiongozi mpya wa kanisa.
Makadinali waliochaguliwa watapiga kura mara nne kwa siku hadi pale Papa
mpya atakapo patikana.
Kwingineko maelfu ya waumini wanatizama kwenye
televisheni na kusikiliza kwenye redio matukio ya Roma kujua iwapo
wamepata Papa.
0 comments:
Post a Comment