Na Bertha Ismail- Arusha
Imebainika kuwa migomo ya daladala inayotokea mara kwa mara
hapa mkoani Arusha inasababishwa na vitendo vya rushwa vilivyoota mizizi baina
ya madereva wa daladala hizo na askari wa kikosi cha usalama barabarani hali
inayoleta usumbufu mkubwa kwa wananchi wa kawaida wanaotegemea usafiri huo.
Hayo yamebainika hivi karibuni kwenye mgomo wa madereva wa
daladala uliotokea mkoani hapa, ikiwa ni siku chache tu tangu yatokee tena
miezi ya katikati ya mwaka jana huku yakihusishwa na siasa ambapo hali hiyo
ilisababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi wa kawaida wanaotegemea usafiri huo
wakiwemo wanafunzi.
Aidha katika mgomo wa wiki iliyopita, gazeti hili
lilifankiwa kuzungumza na baadhi ya madereva wa kisongo, kwa mrombo na Usa
ambao hawakuwa tayari kutajwa majina yao, ambapo walisema kuwa wameamua kugoma
kushinikiza jeshi la polisi na serikali kwa ujumla kuchukua hatua juu ya askari
wa usalama barabarani ambao wamekuwa wakiwaonea kila kukicha kwa kudai fedha
zisizo na sababu.
Walisema kuwa askari hao wa usalama barabarani wamewafanya
madereva hao kama chanzo cha mapato yao kwani wamekuwa wakiwatoza fedha kila
siku kuanzia 150,000 hadi 300,000 bila hata kosa la kimsingi wala onyo hali
ambayo imekuwa ikiwatia hasara katika kazi zao wao na wamiliki wa magari hayo
bila askri hao kujali hilo.
Waliongeza kuwa endapo wakikataa kulipa fedha hizo
barabarani au hata kutoa rushwa ili kusamehewa, hupelekwa kituo cha polisi kwa
ajili ya kwenda kuandikiwa karatasi ya madai (notisification) lakini wafikapo
hulazimishwa kuwanunulia askari hao chakula au kifungua kinywa ili kupewa
karatasi hiyo,
“Endapo ndugu yangu ukishindwa kuwapa hiyo rushwa
wanakukamata na kukupeleka kituo cha polisi kati (central) na ukifika kule
hataki tena kuandika hadi ukamnunulie kifungua kinywa kama ni asubuhi ambayo
unalazimishwa kununua mayai, kuku, chapatti na chai ya maziwa, au kama ni
mchana ukamnunulie chakula wakati wewe tangu asubuhi hata hujala muhogo wa
kuchoma licha ya kumnunulia askari na kitambi chake kuku…, hii ni haki?”
alisema kwa kuuliza mmoja wa madereva hao.
Mbali na hilo walilalamikia pia ukosefu wa vituo maalum vya
kupaki magari pamoja na stendi ya kupakia na kushusha abiria kwani ukosefu wa
vituo hivyo vimekuwa kama mradi wa kujipatia fedha kwa askari hao endapo dereva
akipaki mahala ambapo siyo kituo.
Aidha baada ya mgomo huo uliodumu kwa takribani masaa tisa
(9) kuanzia alfajiri ya tarehe 18 hadi saa saba mchana, mkuu wa wilaya ya
Arusha John Mongela alikutana na madereva na wamiliki wa magari hayo na
kusikiliza kero zao ambapo aliwaahidi kushughulikia na kuwataka kuendeleza
huduma hiyo ya usafiri huku yakiendelea kushughulikiwa.
Pia baada ya hapo Mongela alizungumza na waandishi wa habari
na kukiri swala la rushwa kuwa chanzo cha mgomo huo kutokana na malalamiko
aliyoyapata kutoka kwa madereva na wamiliki wa magari hayo,
“Ukweli usiopingika ni kuwa ukweli rushwa ndio chanzo cha
mgomo huo ingawa kunasababu ndogo ndogo pia zimeingia hapo ndani ikiwemo
ukosefu wa vituo, miundombinu ya barabara iboreshwe kwani barabara ni chache
ikizingatiwa na ongezeko la idadi ya watu
pia kuwepo na stendi ya kupakia na kushusha abiria” alisema Mongela.
Mongela aliongeza kwa
kusema kuwa “ingawa ni kweli rushwa imesababisa mgogoro huo lakini sio jeshi la
polisi zima linahusika bali ni tabia ya askari mmoja mmoja ambapo serikali
inafanya uchunguzi wa kuwabaini waliohusika ili sheria ichukue mkondo wake
kwani hao niwahalifu kama wahalifu wengine.”
Sanjari na hayo pia watu 20 walikamtwa na jeshi la polisi kwa
tuhum za kufanya fujo na kuharibu mali
za watu, na pia kuuchochea mgomo huo, ikiwemo kuvunja vioo vya gariaina Toyota hiace lenye namba
T. 171 BBE mali ya Edward Clegori, pia wanashikilia gari Nissan Caravan namba T
499 CFV mali ya Gabriel Thomas ambalo lilikuwa likitumika kusambaza vijana
waliokuwa wanafanya fujo katika maeneo mbalimbali ya jiji la Arusha.
0 comments:
Post a Comment