BAADHI ya wananchi wilayani Hanang’, Manyara wameanzisha biashara ya
uuzaji vyuma chakavu na kusababisha uharibifu wa miundombinu hasa ya
barabara.
Mkuu wa Wilaya ya Hanang’, Christine Mndeme, alibainisha hayo juzi
alipozungumza kwenye baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya na
kueleza kuna watu wameanzisha biashara hiyo ambayo imekuwa ikichangia
uharibifu wa miundombinu.
“Biashara ya vyuma chakavu imeanza kushamiri mjini kwetu, serikali
inahangaika kuboresha miundombinu ya barabara, watu wanaiharibu kwa
kung’oa vyuma katika maeneo kadhaa na kwenda kuuza. Tusaidiane
kudhibiti hali hii, ili kukomesha uharibifu wa miundombinu,” alisema.
Mndeme alibainisha kwamba kuna watoto walioanzisha zoezi la kulenga
shabaha kwenye nguzo za umeme, jambo ambalo ni hatari kwao na kwa mji
mzima kutokana na athari za umeme zitakapotokea pindi wanapolenga
shabaha vikombe vinavyoshikilia kwenye nguzo hizo.
Mbali na hilo, alihimiza suala la usafi na kusema mazingira ya mji
huo ni machafu hasa maeneo ya katikati ya stendi ambapo mapipa ya
kuhifadhia takataka yanajaa bila wahusika kuyafanyia usafi na
kusababisha harufu mbaya.
0 comments:
Post a Comment