Mbowe, Profesa Lipumba, Mchungaji Mtikila wahutubia.
ZANZIBAR.
Viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa), wameapa kuendelea kudai mfumo wa Muungano wa serikali tatu nje
ya Bunge la Katiba kwa nguvu zote, ikiwamo kufanya maandamano ya amani
nchi nzima.
Msimamo huo ulielezwa
na viongozi hao kwa nyakati tofauti katika mkutano wa hadhara
uliofurika mashabiki kwenye Viwanja vya Kibandamaiti, Unguja jana.
Mwenyekiti
Ukawa, Freeman Mbowe alisema wameamua kuliacha Bunge la Katiba kutokana
na harufu za rushwa, vitisho na matusi huku baadhi ya wabunge
wakiahidiwa vyeo. Mbowe ambaye hata hivyo hakufafanua zaidi, alisema
Ukawa wameamua kwenda kwa wananchi kuwaeleza dhamira chafu walionayo
wabunge wa CCM katika mpango wao wa kukataa Rasimu ya Tume ya Mabadiliko
ya Katiba iliyowasilishwa na Jaji Joseph Warioba.
“Ni jambo
la hatari katika mchakato wa Katiba wananchi kuwa waoga au hofu...
Lazima tuwe tayari kuwaonyesha watawala kuwa tuna umoja imara,
tunayapigania mataifa huru ya Tanganyika na Zanzibar, Rais Kikwete
(Jakaya) asiwatishe wananchi kwa kivuli cha jeshi kuchukua madaraka,”
alisema Mbowe.
Lipumba anena
Mwenyekiti Mwenza wa
Ukawa, Profesa Ibrahim Lipumba alisema wajumbe wa Ukawa wameamua
kujitoa bungeni kutokana na kauli ya Rais Jakaya Kikwete ambayo alidai
kuwa iliibeza na kuidhalilisha Tume ya Warioba.
Alisema hawatarudi bungeni na kwamba hawawezi kujadili Katiba ambayo siyo maoni ya wananchi.
Alidai
kwamba kwa makusudi Rais Kikwete aliamua kutetea sera za chama chake na
kupingana na maoni yaliyotolewa na wananchi kupitia Tume ya Mabadiliko
ya Katiba.
“Rais Kikwete ameharibu nia ya kupatikana Katiba
Mpya, amekuwa akijulishwa kila hatua na jinsi maoni ya wananchi
walivyokuwa wakipendekeza serikali tatu katika Rasimu ya Kwanza na ya
Pili naye akawa anaafiki, inashangaza amegeuka na kukataa maoni ya
wengi,” alisema Profesa Lipumba.
Mtikila akumbushia jela
Mwenyekiti
wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila alisema aliwahi kufungwa jela mara
tatu, kuwekwa mahabusu mara 43 kwa kudai lipatikane Taifa la Tanganyika
huku watawala wakikataa matakwa ya wengi kwa sababu na hoja dhaifu.
Mchungaji
Mtikila aliongeza kusema kwamba wanachokitaka CCM na Serikali zake ni
kuendelea kuwabana wananchi wa Tanganyika na Zanzibar wasiweze kuwa huru
na kujivunia mataifa yao.
MWANANCHI
Home
»
»Unlabelled
» UKAWA WAAPA KUENDELEA KUDAI MFUMO WA MUUNGANO WA SERIKALI TATU NJE YA BUNGE LA KATIBA KWA NGUVU ZOTE.
Friday, May 2, 2014
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment