WIZARA ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, imewataka wazazi
kuacha tabia ya kuwageuza watoto walio chini ya umri wa miaka 18 kuwa
vitega uchumi vyao.
Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salam juzi na Waziri wa wizara
hiyo, Sophia Simba alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Alisema hivi sasa wazazi wengi wamekuwa wakiwafanya watoto wao vitega
uchumi kwa kuwatafutia kazi za ndani wakiwa chini ya miaka 18, jambo
ambalo ni kinyume cha sheria.
Waziri Simba alisema ni kosa kubwa kwa mzazi kumpeleka mtoto wake
mwenye miaka chini ya 18 kwenda kufanya kazi za ndani wakati anatakiwa
kupata elimu.
“Watoto ni taifa la kesho kwa hiyo tunapaswa kuwajengea msingi bora,
ili wasije kuwa tegemezi hapo baadaye. Tuhakikishe wanapata elimu
badala ya kuwageuza vitega uchumi kwa kuwatafutia kazi za ndani,”
alisema.
Katika hatua nyingine, Waziri Simba aliwataka Watanzania kuacha tabia
ya kuwanyanyasa wafanyakazi wa ndani kwa kuwatumikisha zaidi ya saa 12
na kuwalipa mshahara mdogo kwa kisingizio cha kula na kulala nyumbani
kwa mwajiri.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment