TIMU ya JKT Oljoro imepania kukabili ushindani wa ligi Daraja la
Kwanza kwa kuanza maandalizi mapema ikiwemo kuingia kambini na kujifua
kwa mazoezi magumu ili waweze kurejea Ligi Kuu ya Vodacom.
JKT Oljoro imeshuka daraja msimu huu baada ya kudumu Ligi Kuu kwa takribani miaka minne.
Akizungumza, Mwenyekiti wa timu hiyo, Meja
Sijaona Myala, alisema kuwa timu itaingia kambini Mei 25 na watajifua
kisawasawa mfululizo, sambamba na mechi mbalimbali za kirafiki.
“Suala la kushuka daraja kutoka Ligi Kuu Bara hadi Ligi Daraja la
Kwanza halitukatishi tamaa, bali ni kuangalia tu yapi yalisababisha ili
turekebishe na changamoto ni zipi tuzitatue ili kuhakikisha tunapanda
na kubaki juu, kwa sababu hata sisi tuko fiti kisoka na wapinzani wetu
wanatukubali,” alisema.
Alisema kwa sasa wanachokifanya ni kuboresha timu, benchi la ufundi
na kutafuta makocha wa makipa, sambamba na kuziba mapengo ya wachezaji
waliomaliza mikataba, yote ikiwa ni mikakati ya kutimiza malengo
waliyojiwekea ya kupanda na kubaki kung’ara kwenye soka.
Katika hatua nyingine, uongozi huo pia umejipanga kuboresha michezo mingine kama netiboli, ngumi, riadha, wavu n.k.
0 comments:
Post a Comment