Siku mbili zilizopita tulichapisha picha na
habari katika ukurasa wa mbele wa gazeti hili kuhusu mgonjwa
anayejulikana kwa jina la Abdi Lanjui ambaye amelazwa wodini katika
Hospitali ya Singida kwa miaka 45 sasa, kutokana na ajali mbaya
aliyopata mwaka 1971. Mgonjwa huyo mwenye miaka 75 alikuwa dereva wa
Mamlaka ya Pamba na kupata ajali hiyo mkoani Mwanza baada ya lori
alilokuwa akiendesha kuchomoka gurudumu la mbele na kupinduka.
Kusikiliza maelezo yake kuhusu mkasa huo uliompata
kunatia uchungu mkubwa. Maelezo yake yanaleta hisia kwamba dunia siyo
tu haina huruma, bali pia ni katili na ndiyo maana imemsahau na kumtosa
kwa muda mrefu hivyo. Jambo la ajabu ni kuwa, ni mtulivu na mvumilivu
kwa kiwango cha juu na bado anaishi kwa matumaini. Hana hasira wala
kinyongo na dunia au jamii iliyomwacha katika upweke na maumivu makubwa
kwa miaka yote hiyo 45.
Akizungumza huku akionekana kuwa katika mateso
makubwa, anasema sababu ya kugeuza wodi kuwa makazi yake ya kudumu ni
ajali iliyomsababishia kupooza kuanzia kiunoni hadi kwenye nyayo.
Anasema kwa kuwa hanyanyuki kitandani, amepata vidonda kuanzia makalioni
hadi miguuni na kuongeza kwamba anaishi maisha magumu mno.
Kutokana na hali hiyo, anaiomba Serikali na jamii
kwa jumla imwonee huruma kwa kumsaidia chakula kwa kuwa hana ndugu wa
kumpatia msaada wowote. Anasema, kwa miaka mingi uongozi wa hospitali ya
Mkoa ulikuwa ukimhudumia kwa kumpa chakula, lakini baadaye huduma hiyo
ilisitishwa, hivyo kumfanya awe ombaomba na maisha yake kuwa ya mlo
mmoja kwa siku.
Kwa kuwa hawezi kunyanyuka kitandani na hana ndugu
yeyote, amekuwa akiwaomba msaada manesi na watumishi wengine wa hapo
hospitalini. Anawashukuru kwa kufanya hivyo bila kuchoka na kumwezesha
angalao kupata mlo mmoja kwa siku, lakini pia anaomba msaada wa fedha
ili aweze kwenda Hospitali ya KCMC au hospitali nyingine yoyote inayofaa
ili apate huduma zaidi ya matibabu.
Mgonjwa huyo aliyelazwa katika Wodi Namba Nne
katika hospitali hiyo tangu Januari Mosi, 1971, awali alilazwa katika
Hospitali ya Sekou Toure, jijini Mwanza kuanzia mwaka 1969 mara baada ya
kupata ajali. Akiwa katika hospitali hiyo mwishoni mwa mwaka 1970, hali
yake ilibadilika na kuwa mbaya na ndipo alipomwomba mwajiri wake
amrudishe nyumbani katika Kijiji cha Mhintiri katika Wilaya ya Ikungi,
mkoani Singida mwaka 1971. Bahati mbaya ni kuwa, wakati anapata ajali na
kulazwa hospitalini, wazazi wake na ndugu yake pekee walikuwa tayari
wamefariki dunia.
Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Mussa Kamala
anasema hivi sasa mgonjwa huyo anahudumiwa na hospitali kama watu
wengine wenye ulemavu. Anasema uongozi wa hospitali hiyo uliwahi
kumkabidhi kwa Idara ya Ustawi wa Jamii ili ifanye mpango wa kumrudisha
nyumbani, lakini haikuwezekana.
Wakati huohuo, Ofisa Ustawi wa Jamii mkoani
Singida, Zuhura Kalya anasema walishindwa kumrejesha nyumbani kwao,
kwani walipofuatilia ilibainika kwamba hana ndugu na hakukuwa na mtu
anayemfahamu kwa kuwa aliondoka kijijini hapo mwaka mmoja baada ya
Uhuru.
Sisi hatuna la zaidi, isipokuwa kuwaomba wananchi
kumsaidia mgonjwa huyo ambaye ameteseka vya kutosha kwa takribani nusu
karne sasa. Ni matumaini yetu kwamba Serikali pia itachukua hatua
stahiki haraka iwezekanavyo.
0 comments:
Post a Comment