.

.
Thursday, May 8, 2014

11:57 AM
MAPIGANO ya kuwindana yanayotokana na mgogoro wa ardhi unaohusisha makabila ya Sonjo na Maasai katika tarafa za Sale na Loliondo, wilayani Ngorongoro, Arusha hadi sasa yameshaua wananchi 11.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Ngorongoro jana, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Eliasi Wawalali, alisema katika jitihada za kukomesha mapigano hayo, wamefanikiwa kukamata silaha tatu za kivita aina ya AK 47, SMG na SR ambazo zimesalimishwa na makundi hasimu katika mgogoro huo.
Wawalali alisema mgogoro huo ambao ni wa muda mrefu sasa unashindwa kumalizika kutokana na kutokuwepo kwa utashi kwa viongozi wa maeneo yenye mgogoro na pia kukiukwa baadhi ya maagano ya kale baina ya makabila hayo yaliyofanywa kwa kusimamiwa na hayati Edward Sokoine, aliyekuwa Waziri Mkuu katika kipindi hicho.
“Mgogoro huu na uhasama baina ya makabila haya hususani Wasonjo na koo ya Loita kwa upande wa Masai ulianza tangu mwaka 1975 na kuhusika kwa matumizi ya silaha nzito za kivita na hadi mimi nimeukuta mgogoro huo na tunajitahidi kuumaliza bila mafanikio,” alisema.
Alisema kwa kipindi cha miaka mitano tangu afike Ngorongoro, katika mgogoro huo wameshakamata silaha za kivita zaidi ya 80 ambazo zinaaminika hununuliwa kutoka nchi jirani kwa wananchi wa jamii hizo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ngorongoro, Eliasi Ngorisa, alisema wao kama madiwani ambao ni wawakilishi wa wananchi hawatakuwa na ujasiri wa kujisifu kuwa ni viongozi bora kama hawatajitoa kwa pamoja kuhakikisha mgogoro huo unamalizika.
chanzo,tanzania daima

0 comments:

Post a Comment