MIKUTANO miwili ya hadhara ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA),
iliyofanyika Unguja na Pemba visiwani Zanzibar, na ujumbe uliotolewa na
viongozi wa umoja huo, umeitia kiwewe Chama cha Mapinduzi (CCM)
ambacho kimepanga kujibu mapigo.
Mbali ya kutaka kujibu mapigo, CCM pia inahaha kutumia vyombo vya
dola na ofisi ya msajili kuusambaratisha umoja huo unaoonekana kuungwa
mkono na wananchi wengi.
UKAWA inaundwa na vyama vinavyounga mkono rasimu ya katiba ya
serikali tatu ambavyo ni Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (CHADEMA), NCCR- Mageuzi, UDP na vyama vingine ambavyo
wajumbe wake walisusia mjadala wa Bunge Maalumu la Katiba baada ya
kutoridhishwa na namna Bunge hilo lilivyokuwa linaendeshwa.
Ujumbe unaoelezwa kuivuruga CCM kwenye mikutano hiyo ya UKAWA
visiwani Pemba na Unguja, ni ule unaoeleza mkakati wa umoja huo kutaka
kusimamisha mgombea mmoja wa urais na katika ngazi nyingine za
uwakilishi.
Duru za siasa zinasema kuwa tayari viongozi wa juu wa CCM wamepanga
kuanza kufanya mikutano ya hadhara kujibu mapigo ya UKAWA, na pia
kueleza umuhimu wa kuwa na serikali mbili na ubaya wa serikali tatu.
Habari zinasema kuwa CCM leo imepanga na tayari imeomba kibali
kufanya mkutano wa hadhara visiwani Zanzibar, katika uwanja ule ule
waliotumia UKAWA wa Kiembesamaki.
Mkutano huo ambao unaelezwa kwamba utawashirikisha baadhi ya viongozi
wa CCM kutoka Tanzania Bara, pamoja na mambo mengine utajibu kauli za
UKAWA, hasa kuhusu serikali tatu, lakini pia kuelezea mkakati wao wa
kutaka kuungana 2015.
“CCM leo wana mkutano hapa hapa Kiembesamaki walipofanyia UKAWA.
Wamepanga kutoa ufafanuzi wa hoja za UKAWA ambazo kama zikiachwa,
zinaweza kuleta athari kubwa kwa taifa,” alisema mmoja wa viongozi wa
CCM Zanzibar.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Nape Nnauye, alisema kuwa
wamelazimika kwenda kujibu mapigo kwa madai kuwa UKAWA wameamua
kupotosha umma na hawana nia njema na taifa.
Alisema UKAWA wamevunja sheria ya mabadiliko ya katiba ambayo
inakataza kwenda kwa wananchi sasa wakati hakuna jambo
lililokwishaamuliwa bungeni.
Duru za siasa toka ndani ya chama hicho tawala, zinasema kuwa moja ya
njia hizo ni kutumia ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kuhoji
uhalali wa UKAWA kubadilisha hoja ya mchakato wa katiba mpya na
kuzungumzia harakati za kutaka kusimamisha mgombea mmoja wa urais.
Alisisitiza kuwa watazunguka nchi nzima katika kila eneo ambalo UKAWA
watapita ili kutoa ufafanuzi wa ajenda zao ambazo alidai zina nia ya
kusaka madaraka.
Wakati CCM wakijipanga kwenda kujibu mapigo, upande mwingine chama
hicho kinadaiwa kutumia vyombo vya dola na ofisi ya msajili kutaka
kuusambaratisha umoja huo na kuzima mikutano yao Tanzania Bara.
Tayari Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, juzi
alikaririwa na gazeti moja akionyesha kukerwa na jinsi UKAWA
wanavyofanya mikutano ya hadhara kwa kutumia jina la umoja huo, huku
wakijua fika kwamba sio chama cha siasa kilicho na usajili.
Jaji Mutungi katika taarifa hiyo, alisema mikutano ya hadhara
iliyoombewa kibali Zanzibar ni ya CUF, lakini alieleza kushangazwa
kwake, kwamba katika mikutano hiyo wazungumzaji walikuwa
wakijitambulisha kwa jina la UKAWA na kusalimiana kwa jina la umoja
huo.
Pia alihoji sababu za umoja huo kutumia UKAWA kisiasa kwa kutangaza
kusimamisha mgombea mmoja wa urais mwakani badala ya kuzungumzia
mchakato wa katiba na sababu zilizowatoa nje ya Bunge.
Habari zaidi zinasema kuwa kuna mpango wa vyombo vya dola kutumia
kauli ya msajili kuzuia mikutano ya UKAWA Tanzania Bara kwa madai kuwa
umoja huo umevunja sheria.
Habari za kiintelijensia zinasema kuwa polisi watazuia mikutano ya
UKAWA kama itaombewa kibali cha umoja huo, lakini kama kibali hicho
kitaombwa kupitia moja ya vyama vinavyounda UKAWA, jeshi hilo
litalazimika kujiridhisha mkutano huo utakuwa wa chama husika na si
vinginevyo.
Akizungumza na maelfu ya wananchi visiwani Pemba, Mwenyekiti wa
UKAWA, Freeman Mbowe, alielezea nia ya umoja huo kutaka kusimamisha
mgombea mmoja wa urais na katika nafasi nyingine za uwakilishi.
Katika mkutano huo wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Gombani
Kongwe mjini Chakechake Pemba, juzi, Mbowe alisema UKAWA umeanzishwa
kwa ajili ya mchakato wa katiba mpya, lakini baada ya kuona faida yake,
sasa wanakusudia kusimamisha mgombea mmoja kwenye uchaguzi mkuu
mwakani.
“Je, wananchi wa Pemba mko tayari kuwa na mgombea mmoja kuanzia
uwakilishi hadi rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?” alihoji Mbowe
na kuitikiwa kwa kuungwa mkono na maelfu ya wananchi waliofurika
kwenye uwanja huo.
Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), alisema nguvu ya pamoja na mshikamano walioukosa zamani,
ilisababisha CCM kuwa jeuri, hivyo hawawezi kurudia kosa hilo.
Mbowe ambaye pia ni mbunge wa Hai, alisema wapinzani wanapaswa
kujilaumu wenyewe kwa kujitenga kwani walikosa nguvu ya pamoja katika
chaguzi zilizopita.
0 comments:
Post a Comment